IDARA YA KATIBA YAANZA KUKUSANYA MAONI UANZISHWAJI MFUMO WA TAKWIMU
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
IDARA ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, inafikiria kuja na mfumo wa kisasa wa ukisanyaji wa takwimu, kwa watoa msaada wa kisheria, ili kuwa na takwimu za uhakika na zilizosalama.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 15, 2026 na Wakili wa serikali kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, Moza Rajab Baraka, alipokuwa akifungua kikao kazi, cha ukusanyaji maoni, kuelekea upatikanaji mfumo huo, kilichofanyika Gombani Chakechake.
Alieleza kuwa, ujio wa mfumo huo, utawawezesha watoa msaada wa kisheria na na wadau wengine wingine, wanaohitaji takwimu sahihi za elimu, ushauri na msaada wa kisheria, kuzipata kwa uhakika na haraka.
Alifafanua kuwa, kwa sasa upatikanaji wa takwimu hizo, umekuwa sio wa uhakika, na wakati mwingine hata kucheleweshwa kwa wanaozihitaji, kwa matumizi mbalimbali.
‘’Kwa sasa takwimu za wanaopata msaada au elimu ya kisheria, zipo ingawa sio katika eneo salama, kama zilivyo takwimu nyingine,’’alieleza.
Mapema Wakili wa serikali kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, Yusfa Abdalla Said, alisema mfumo huo ni tegemeo la utunzaji wa takwimu na zikiwa salama zaidi.
Alisema, Idara inaendelea kukusanya maoni kwa wadau wake mbalimbali, ili kuhakikisha inakuwa na mfumo maalum wa upatikanajiwa takwimu.
Alisema, lengo la Idara kutaka kuanzisha mfumo huo wa kidigital, ni kuwa na takwimu sahihi na za uhakika, zikiwa zinalindwa kisheria.
Jingine, alisema ni kubaini makundi ambayo hayajafikiwa au yanataka kufikiwa kwa ajili ya kupatiwa elimu, ushauri na msaada wa kisheria.
‘’Mfumo huu ambao tunaendelea kupokea maoni, ya jinsi gani uwe, tunategemea utatusaidia pia, kupata takwimu za mwaka, ambazo zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kazi nyingine,’’alifafanua.
Akitoa maoni yake, Afisa kutoka Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa serikali Pemba Mussa Alawi Mohamed, amewakumbusha kuwa, bado takwimu zote ziko chini ya ofisi hiyo.
Alisema, lazima Idara irudi tena kwa ofisi hiyo, kwa ajili ya kuungana pamoja, ili zinapotoka kwa ajili ya matumizi ziwe zinanasibishwa moja kwa moja na ofisi ya Mtakwimu mkuu wa serikali.
Nae Msaidizi wa sheria kutoka Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani Shaban Juma Kassim, alisema kama mfumo huo ukianza, takwimu ziwe zinaangalia kijiografia, kuanzia kijiji, shehia hadi ngazi ya taifa.
Wakili wa serikali kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali Pemba Safia Saleh Sultan, alisema jambo hilo ni jema, linalokusudiwa kufanywa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria.
Mwanasheria kutoka Chuo cha Mafunzo Pemba, Amir Iddi Omar, alishauri kuongezwa idadi ya wajumbe kwenye timu ya kitaalamu ya uanzishwaji wa kuelekea mfumo huo.
Afisa sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Salma Suleiman Abdulla, alisema hawakupenda kuwa na mfumo wa majaribio, kabla ya kupokea maoni ya wajumbe.
‘’Tuliona kuwa, kwanza tukusanye maoni ya wadau, ili tuone wanataka uweje mfumo huo, na kisha tutakwenda kuuanzisha na kuuleta tena kwa wadau kwa maoni zaidi,’’alifafanua.
Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar iliyoanzishwa chini ya sheria nambari 13 ya mwaka 2018, ina kazi ya kuratibu, kusimamia na kuendesha huduma za masaada wa kisheria Zanzibar, ambapo kwa sasa inakusanya maoni juu ya uanzishwaji wa mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na usimamizi wa takwimu za msaada wa kisheria.
Mwisho
Comments
Post a Comment