AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA
NA HAJI NASSOR, PEMBA @@@@
AFISA Mdhamini wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Pemba, Halima Ali Khamis, ameitaka Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar ‘AGCZ’ kurudi tena kwa wadau, baada ya kuyachakata maoani ya sheria nambari 13 ya mwaka 2018 ya Msaada wa Kisheria Zanzibar.
Mdhamini huyo aliyasema hayo leo Novemba 13,
2025, ukumbi wa wizara ya Fedha Pemba, alipokuwa akifungua kikao kazi, cha
kukusanya maoni ya sheria ya Msaada wa Kisheria, mbele ya wadau wakiwemo
wasaidizi wa sheria, Polisi, Masheha na wadau wa haki za binaadamu.
Alisema
itapendeza zaidi, baada ya kukusanya maoni hayo kwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu
kurudi tena kwa wadau, ili kujadiliana kabla ya kuandikwa, kama sheria ya msaada
wa kisheria.
Alieleza kuwa,
wadau wanataka kuona maoni yao, ikiwa yamezingatiwa kwa kiasi gani, kwenye uandikwaji
wa sheria hiyo upya hapo baadae.
‘’Niwaombe
sana wenzetu wa ofisi ya 'AGCZ', mkumbuke kurudi tena kwa wadau, baada ya
kukusanya maoni, ili kabla haijapelekwa hatua nyingine, kwanza wajiridhishe,’’alifafanua.
Katika hatua
nyingine Afisa Mdhamini huyo, alisema, msingi wa usaidizi wa sheria, utaendelea
kuwa mwarubaini wa upatikanaji wa haki kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa
kifedha wala uwelewa wa sheria.
Alieleza kuwa,
kazi hiyo kwa sasa, inasisimiwa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria
Zanzibar, na hasa ndani ya awamu ya nane, inayoongozwa na Dk. Hussein Ali
Mwinyi.
Alieleza kuwa,
mazingira ya upatikanaji wa msaada wa kisheria bila ya malipo, umesaidia ndani
ya uongozi wa Dk. Mwinyi, kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria.
‘’Msingi wa
usaidizi wa sheria kwa wananchi, imekuwa ni sehemu ya kuimarisha utawala bora,
na leo tunajivunia kwa kazi kubwa iliyofanywa na Mkurugenzi wa Idara ya Katiba
na Msaada wa Kisheria Zanzibar,’’alifafanua.
Wakati huo
huo, Afisa Mdhamini huyo, alitumia nafasi hiyo, kumpongeza Rais wa Zanzibar Dk.
Hussein Ali Mwinyi, kwa kuchaguliwa tena, kuiongoza Zanzibar kwa awamu ya pili.
Aidha,
aliwataka wadau wa kikao hicho kazi, kuwa huru kutoa maoni yao kwa maslahi mapana
ya taifa, ili kuwa na sheria rafiki kwa watoa msaada wa kisheria, na wasimamizi
wa haki jinai na madai.
‘’Kwa mfano
ndani ya mapendekezo ya sheria hiyo, limo, suala la kuanzishwa kwa mfuko wa msaada
wa kisheria ‘Legal Aid Fund’, ili kuonesha umuhimu wa kuwepo
kwake ama kutokuwepo,’’alishauri.
Alisema,
wamekuwa na utaratibu wa kuzipitia sheria kadhaa, ambapo kwa sasa ni hiyo ya
Msaada wa Kisheria Nambari 13 ya mwaka 2018.
Akiwasilisha
mapendekezo ya sheria hiyo, Wakili wa serikali kutoka ofisi ya AGCZ, Sumaiya Awadhi
Hassan alisema, wameona kuangalia, kuna uwezekano wa kupatikana msaada wa
kisheria kwa makosa ya madai, ikiwa mtu ameishtaka serikali.
Alisema jingine
ni kuanzishwa kwa vituo vya msaada wa kisheria ‘legal aid clic’,
ambapo sheria ya sasa haijaeleza kuhusu kuvitambua hivyo, jambo ambalo kama
wadau watahisi linauhimu watalisemea.
Akichangia kwenye
sheria hiyo, mjumbe kutoka Mwemvuli wa Asasi za Kiraia Pemba ‘PACSO’ Mohamed
Najim Omar, alisema kuwa, suala la kukosekana kwa mfuko wa wasaidizi wa
sheria ni tatizo.
Nae Said Rashid
Hassan, kutoka Shirika la Msaada wa Kisheria na Haki za Binaadamu Zanzibar ‘ZALHO’ alishauri kuwa,
makosa ya dawa za kulevya na yanayofanana na hayo, yasiingizwe kwenye makosa
yanayopewa msaada wa kisheria.
Afisi ya
Mwanasheria Mkuu Zanzibar ambayo imeanzishwa chini ya sheria nambari 6 ya mwaka 2013
ambapo miongoni mwa majukumu yake makuu ni kuzifanyia marekebisho sheria mbali
mbali.
Mwisho
Comments
Post a Comment