WAJUMBE SHEHIA MVUMONI WAPIGWA MSASA ELIMU YA KISHERIA
NA MWANDISHI WETU, PEMBA
Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilayani humo ‘CHAPO’
Mohamed Hassan Abdall, aliyasema hayo leo Disemba 7, 2025 wakati akiwasilisha
mada ya haki za binaadamu, kwa wajumbe hao, kwenye mafunzo ya siku moja.
Alisema, haki za binaadamu, ni haki zote anazostahiki mtu,
kwa sababu ya kuwepo kwake duniani, ikiwemo uhai, matibabu, afya, elimu, utaifa
na uzalendo.
‘’Niwaombe sana wajumbe wetu wa shehia ya Mvumoni, kwanza
elimu hii mkawafikishie na wingine, maana haki za binaadamu ni zote,’’alieleza.
Akizungumzia faida za kufanya sulhu kwa kesi za madai kama
vile, huduma za mke, watoto, migogoro ya ardhi, mirathi na madeni, alisema inaondosha
visasi.
Alifahamisha, kuwa ndio maana, wamempeleka msaidizi wa
sheria katika eneo lao, ili migogoro hiyo kabla haijafikishwa mbele ya vyombo vya
sheria, kwanza wakutane na kuangalia ufumbuzi.
‘’Hapa tukumbushane kuwa, kesi za jinai kama udhalilishaji,
wizi, dawa za kulevya, utoroshaji wa watoto na yanayofanana na hayo, yapelekwe Polisi
moja kwa moja,’alifafanua.
Nae Msaidizi wa sheria shehiani humo, Haji Nassor Mohamed, ambae
amehamishiwa hapo, akitokea shehia ya Wawi, alisema suala la msaada wa kisheria
ni haki ya kikatiba.
Alieleza kuwa, sasa serikali inawatambua wasaidizi wa sheria,
kupitia Sheria nambari 13 ya mwaka 2018, na kwamba wapo kwa ajili ya
kuwahudumia wananchi bila ya malipo.
‘’Sisi wasaidizi wa sheria, tunaisaidia jamii, iwe ni elimu
ya kisheria, msaada na ushauri wa kisheria tena bila ya malipo, na hasa kwa wale
wasiokuwa na uwezo,’’alieleza.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Katiba na
Msaada wa Kisheria Pemba, Ali Salum Hamad, alisifu juhudi za ‘CHAPO’ katika
kusambaaza elimu ya kisheria kwa jamii.
Alieleza kuwa, mfano uliooneshwa na Msaidizi wa sheria wa
Mvumoni, ni vyema ukaenea katika shehia nyingine za Pemba, kwa mafunzo ya aina
hiyo.
‘’Mafunzo haya naamini ni matunda ya kufanyakazi vyema kwa
pamoja, baina ya uongozi wa shehia ya Mvumoni na CHAPO, jambo ambalo Idara inajivunia
nalo mno,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, amewakumbusha wananchi wa Mvumoni na
maeneo mingine, kuendelea kuwatumia wasaidizi wa sheria, kwa ajili ya kupata
ufumbuzi wa changamoto zao, za kisheria.
Wakichangia mada kwenye mafunzo, mmoja wa wajumbe hao Khamis
Juma Mohamed, alisema mafunzo hayo yamewasaidia, kujua baadhi ya mambo ya
kisheria.
‘’Kwa mfano nimeshajua tofauti baina ya Msaidizi wa sheria
na Mwanasheria, kupata faida ya kufanya sulhu nje ya mahkama kwa kesi za majadi,’’alifafanua.
Nae Asia Juma Khamis,
alisema watamtumia vyema Msaidizi huyo wa sheria, ili kujua haki na wajibu wao
kisheria.
Kwenye mafunzo hayo ya siku moja, mada tatu, ziliwasilishwa
ikiwemo dhana ya msaada wa kisheria, haki za binaadamu na namna ya utatuzi wa
migogoro wa ya madai nje ya mahkama.
MWISHO.

Comments
Post a Comment