CHAPO: 'WANAFUNZI WAIBUWENI WANAOTAKA KUWADHALILISHA'
NA
MWANDISHI MAALUM, CHAPO
WANAFUNZI
wa chuo cha Qur-an cha kijiji cha Vikutani shehia ya Wawi wilaya ya Chake chake
Pemba, wametakiwa kuwaibua ndugu na jamaa zao, wanaoashiria kutaka kuwafanyia
vitendo vya udhalilishaji.
Ushauri huo umetolewa Januari 29, 2023 na Msaidizi wa
sheria Jimbo la Wawi Haji Nassor, wakati akitoa elimu ya kupambana na matukio
ya ukatili na udhalilishaji, hasa kwa watu wao wa karibu, kwenye mkutano
uliofanyika chuoni hapo.
Alisema, tafiti kadhaa zinaonesha kuwa, sasa watoto
wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo na watu wao wa karibu, na kushindwa kutoa
taarifa hizo, katika maeneo husika.
Alieleza kuwa, wakati umefika sasa kutowafumbia macho
watu hao, kwani wamekuwa wakishindwa kuonesha upendo wa kweli kwao, jambo
ambalo linaweza kusababisha kupoteza mwelekeo wa maisha yao.
‘’Wanafunzi niwasihi sana kuwa, iwapo kuna kaka, baba,
ami, mjombo ameanza kukufanyia vitendo vya udhalilishaji, mseme kwa wenzako au
wetu wengine wa karibu,’’alifafanua.
Aidha Msaidizi huyo wa sheria alisema, eneo moja ya
kuripoti matukio hayo ni kwa mratibu wa wanawake na watoto, katibu wa sheha,
wajumbe wake au kwa msaidizi wa sheria katika eneo wanaloishi.
Mapema Afisa sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Unguja Ali Haji Hassan, aliwataka wazazi na walezi kukataa kufanya sulhu kwa makosa ya ukatili na udhalilishaji.
‘’Haiwezekani, mtoto ameshaharibiwa kwa ubakaji au ulawiti, kisha wazazi wakubali kukaa chini, eti kuyamaliza kienyeji, kwani makosa haya uamuzi wake ni mahakamani,’’alieleza.
Hata hivyo amewataka wanachi Wawi, kuendelea kuwatumia
wasaidizi wa sheria waliomo, kwa ajili ya kupata elimu, ushauri na msaada wa
kisheria.
Nae Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya
ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema kama jamii haijaamua
kuyakataa matendo hayo, watoto wataendelea kudhalilika.
Alieleza kuwa, watoto wanaofanyiwa ukatili na
udhalilishaji, wanawategemea mno wazazi na walezi wao wawasimamie katika vyombo
vya sheria, hivyo wakishindwa kufanya hivyo ni kuwaumiza mara mbili.
‘’Wazazi sote tuungane katika kupiga vita matendo haya,
maana wanaowaumiza kiakili, mwili ni watoto wetu sasa kama hatuko makini,
tutawavunjia ndoto zao za baadae,’’alieleza.
Mapema mjumbe wa sheha wa shehia ya Wawi Nassor Rashid,
aliwataka wasaidizi hao wa sheria, kuendelea kukutana na jamii ya Wawi, kwani
kumekuwa na shida ya elimu ya kutosha.
Baadhi ya wanafunzi walisema, elimu walioyoipata
imewaongezea maarifa katika kupambana na matukio ya ukatili na udhalilishaji.
Mwisho

.jpg)




Comments
Post a Comment