MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

 


  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

MKURUGENZI wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said, amewataka wananchi wa shehia ya Wawi wilaya ya Chake chake, kulindiana haki zao za binaadamu, ili kujengeana heshima baina yao.

 

Hayo aliyasema leo August 11, 2025 eneo la Kwa Gerei shehiani humo, wakati akizungumza na wananchi hao, kwenye mkutano wa wazi wa kutoa elimu ya haki za binaadamu.

 

Alisema kila mmoja anawajibu wa kumlindia haki za binaadamu mwenzake, na kufanya hivyo kutajengeana heshima miongoni mwao.

 

‘’Haki za binaadamu ni pamoja na ile ya kuishi na kupata faragha, sasa kama kila mmoja atamlindiana mwenzake, heshima kwa wananchi, itaongezeka,’’alisema.

 

Hata hivyo Mkurugenzi huyo wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, amewakumbusha wananchi hao, kuwatumia wasaidizi wa sheria, waliomo ndani ya shehia, ili kupata ufafanuzi wa changamoto zao za kisheria.

 

Mapema Afisa sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Pemba Safia Saleh Sultan, alisema haki za binaadamu ni zile alizomwanadamu kwa sababu ya ubinaadamu wake.

 


‘’Kwa mfano haki za kisiasa, uchumi, faragha, haki za kujikusanya na kwenda mtu atakapo bila ya kuvunja sheria, ni sehemu ya haki za binaadamu,’’alifafanua.

 

Aidha, alisema kila mmoja ana haki ya kuheshima haki za mwingine, na sio sahihi kuwa ni kwa mamla za serikali pekee, ndio zinapaswa kuheshima haki za binaadamu.

 

Akijibu baadhi ya maswali yalioulizwa na wananchi, alisema kisheria mtoto chini ya miaka 18 hana ridhaa, hivyo hata kama kuna makubaliano, huitwa tendo la ubakaji.

 


‘’Kwa mfano mtoto ametoka kilomita 100 na kumfuata mwanamme nyumbani kwake, bado kwa mujibu wa sheria huo huitwa ubakaji, pindi likifanyika tendo,’’alifafanua.

 

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan, aliwataka wananchi, kufuatilia nyaraka kwa watoto wao, na sio kusubiri mpaka wakiwa wanazitaka kwa matumizi.

 


‘’Mtoto akizaliwa tu afuatiliwe cheti chake, na akifia miaka 18 familia zifike ofisi za vitambulisho ili taratibu zianze,’’alisema.

 

Mkuu wa Divisheni Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Pemba Bakar Omar Ali, alisema mikutano hiyo ni kwa ajili ya wananchi, kupata elimu ya sheria na hasa eneo la haki za binaadamu.


 



Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, Nassor Said Rashid, alisema elimu zaidi ya kisheria inahitajika kwa jamii.

 

Akifunga mkutano huo, sheha wa Wawi Khamis Mohamed Khamis, aliwataka wananchi wasisite kuhudhuria wanapoitwa kwenye mikutano mbali mbali.



 


Aidha aliipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, kwa uamuzi wake wa kuziacha shehia nyingine na kuitisha mkutano huo, shehiani mwake.

                       Mwisho   

   

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’