‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WANANCHI wa shehia ya Mchakwe na Mwambe wilaya ya Mkoani, wamekumbushwa kuwa, ni kosa la kisheria, kujichukulia sheria mikononi, kwa kuondoa uhai wa mtu, kwani kufanya hivyo, ni kuzipokonya kazi mamlaka zilizopo kisheria.

Hayo yalielezwa jana August 12, 2025 na Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali Safia Saleh Sultan, wakati akizungumza na wanachi hao, kwenye mkutano wa wazi, ulioandaliwa kwa pamoja na Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar na kufanyika shehiani humo.

Alisema, zipo mamlaka ikiwemo mahakama, ndio ambayo inaweza kutoa adhabu ya kifo, ikiwa mshitakiwa atatiwa hatiani.

Alieleza kuwa, imezoeleka kuona wananchi wanajichukulia sheria mikononi, mara wanapomkamata mtuhumiwa, jambo ambalo, wajibu wao ni kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria.



Wakili huyo wa serikali, alisema mahkama pekee ndio ambayo kisheria imepewa nguvu za kisheria, kuondoa uhai wa mtu, ikiwa nae amebainika kuua kwa maksudi.

‘’Imekuwa ni rahisi siku hizi, kuvunjwa kwa haki za binaadamu ikiwemo mtuhumiwa kuuawa, jambo ambalo kisheria ni kosa la jinai,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine Wakili huyo wa serikali, alisema kuwa chimbuko la haki za binaadamu, lilikuja baada ya vita vya kwanza na vya pili vya dunia, ambapo haki nyingi zilivunjwa ikiwemo watu kuuliwa na kunyang’anywa mali zao mbali mbali.


Alieleza kuwa baada ya hapo, mataifa yalikutana na kuunda tamko la haki za binaadamu duniani, ili kila nchi iunge mkono kwa nafasi yake.



Aidha alifafanuwa kuwa, kwa upande wa Zanzibar kulikuwa na katiba ya kwanza 1963 ndani yake kulikuwa na haki za binaadamu, na kisha kuendelezwa kuingizwa kwa ile ya mwaka 1984, zikiwekwa kwenye sehemu ya tatu.

 


Nae Afisa sheria kutoka Idara  ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar Salma Suleiman Abdulla, amesema mikutano hiyo ni muendelezo wa majukumu ya Idara, katika kuifikia jamii yenye uwelewa wa sheria.

Alieleza kuwa, kwa kushirikiana na wasaidizi wa sheria waliomo ndani ya shehia zao, wanaweza kupata ufafanuzi wa changamoto zao, bila ya malipo.

Sheha wa Mchakwe Fatma Khamis, alisema ziara ya watendaji wa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria, ni muhimu kwa wananchi wake, katika kupata uwelewa.



Wananchi wa Mwambe akiwemo Haku Mossi Haji, alisema wanakabiliwa na uvamizi wa ardhi, hasa zinapokuja kampuni kwa uchukuaji wa rasilimali za ujenzi wa barabara.

Nae Kheir Sheha Ali, alisema ipo mgogoro ya ardhi, ambayo inaweza kuepukika, ingawa changamoto ni uwelewa wa jinsi gani ya kuidhibiti kisheria.



 


‘’Huku Mwambe sisi tunavamiwa ardhi zetu, kisa hatuna nyaraka, ingawa tumeshaendesha kilimo kwa zaidi ya miaka 50, jambo linalotupa wasi wasi,’’alisema.

Wakati huo huo Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, imewataka wanafunzi wa skuli ya sekondari ya Dk. Samia Suluh Hassan, kuhakikisha wanawahimiza wazazi wao, kuwapatia vyeti vya kuzaliwa.

Mikutano hiyo ya wazi kwa wananchi, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa upatikanaji haki Zanzibar unaotekelezwa na Idara hiyo, ambapo kesho ni zamu za shehia zilizomo ndani ya wilaya za Micheweni na Wete.

                             Mwisho   

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU