CHAPO: ‘WAZAZI CHAKE CHAKE MSIWARUHUSU WATOTO KUOMBA 'MKONO WA IDD’

 

 

NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

JUMUIYA ya wasaidizi wa sheria, wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’, imewataka wazazi na walezi wilayani humo, kuwakataza watoto, kuacha utamaduni wa kuomba fedha za sikukuu ‘mkono wa idd’ katika maeneo ya mbali na wanapoishi.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 26, 2026 na Mkurugenzi wa Jumuiya hiyo jana, Mohamed Hassan Abdalla, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, kuelekea sherehe ya sikukuu ya kiislamu.

Alisema, utamaduni wazazi kuwaruhusu watoto wao kuomba fedha kipindi cha sikukuu, huwa ni chanzo kikuu cha udhalilishaji ambao unaepukika.

Alieleza kuwa CHAPO, inawapenda mno watoto wa wilaya hiyo, na ndio maana, inaendelea kuwasisitiza wazazi na walezi wao, kuondokana na mpango huo.

Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa, kwani wapo baadhi ya vijana na hata watu wazima, wanaweza kuchukua fursa hiyo ya kuwadhalilisha watoto hao.

‘’Wapo baadhi ya watoto wanatoka kijiji kimoja hadi chingine, kisa ni siku ya sikukuu, hugonga kila nyumba kuomba fedha ‘mkono wa idd’ hii ni hatari, wanaweza kudhalilishwa mara moja,’’alisisitiza.



Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo wa CHAPO, aliwataka wazazi kutowafuatanisha mtoto na wenzake zaidi ya mmoja, kwani huwa vigumu kumlinda.

Alieleza kuwa, sikukuu ya mwaka jana, kulikuwa na mtoto mmoja wa miaka 10, alifuatanishwa na wenzake wanne, na mmoja kumpotea.

Alisema, hilo linaweza kusababisha athari kadhaa, ikiwemo mtoto kupotea, kuibiwa, kupata ajali na kuibiwa vitu vyake kwa kukosa uangalizi.

‘’Ni kweli watoto wanayohaki ya kucheza na kujumuika na wenzao, hata kwenye sherehe kama hizi za sikukuu, lakini ni vyema wakawa na uangalizi wa hali ya juu,’’alifafanua.



Akizungumzia wajibu wa wazazi na walezi kisheria, alisema sheria ya Mtoto nambari 6 ya mwaka 2011, imeeleza wazi wajibu huo, ikiwemo kumkinga na majanga.

Alieleza kuwa, katika baadhi ya vifungu vinamtaka mzazi au mlezi huyo, hata kuongeza ulinzi wa mtoto wake, ikiwemo kumpa taaluma ya kutambua vihatarishi.

Mapema Msaidizi wa sheria shehia ya Wesha Khadija Said Khalfan, aliwashauri wazazi na walezi, kuambatana na watoto wao, kwenye sherehe mbalimbali.

‘’Wapo baadhi ya wazazi huwafunganisha watoto wao na watoto wingine, wao wakiwa nyumbani na kurudi muda wanaoujua wao, hii ni hatari kwao,’’aliwakumbusha.

Mapema Katibu wa Kamati ya kupambana na udhalilishaji wilayani humo, Rashid Said Nassor, alisema watoto ndio rasilami ya familia na taifa, hivyo suala la kuwalinda ni wajibu.



Wakili wa serikali Asia Ibrahim Mohamed, aliwataka wazazi na walezi,  hasa wenye watoto wenye ulemavu, kuongeza ulinzi mara mbili, kwani wadhalilishaji huegemea kwao.

Hivi karibuni akizungumza na masheha wilayani humo, Mkuu mpya wa wilaya hiyo Zuhura Mgeni Othman, aliwakumbusha masheha hao, wasijiingize kwenye usuluhishi wa kesi hizo.

Msaidizi wa Katibu Ofisi ya Mufti Pemba sheikh Said Ahmad Mohamed, alikuwambusha waislam, kuwafundisha watoto wao, namn bora ya kuzitembelea familia na wagonjwa na sio kuomba fedha.

Katibu wa kamati ya muda ya kuzuia ombaomba Pemba Tatu Abdalla Msellem, alisema tabia ya kuomba omba, huanzia kwa baadhi ya watu ambao hawapendi kujishughulisha na kazi na kisha kuwarithisha watoto wao.

Mzazi Hidaya Haji Makame wa Mvumon wilaya ya Chakechake, alisema dawa ya kupunguza matukio hayo, ni kufuata sheria ya Adhabu yam waka 2018, kama ilivyo juu ya kifungo cha maisha au isiyopungua miaka 30 kwa mkosaji.

Mtoto Khairat Muhidin Juma wa Msingini, alisema bado hakuna adhabu kali kwa wanaowabaka na kuwadhalilisha na ndio maana matendo hayo yaripotiwa kila siku.



Takwimu zilizokusanywa na Ofisi ya Mtakwimu mkuu wa serikali Zanzibar, iliripoti matukio 1,809 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, kwa mwaka 2024, ambapo waathirika walikuwa 1,809 na wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 84.3.

 

Wilaya ya Chake chake, ilishika nafasi ya nne, kwa kuripoti matukio 113, kati ya wilaya 11 za Unguja na Pemba, huku wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, ikiwa ya mwanzo kwa matukio 431.

 

Kwa mwaka jana, matukio hayo kwa Unguja na Pemba, yalipungua 581, maana yalikua 1,228, kinyume na yake 1,809 ya mwaka 2024, jambo hata baadhi ya wilaya, ikiwemo ya Chake chake, nako yaliripotiwa kushuka.

 



Wilaya iliyoongoza kwa mwaka jana ni Magharibi ‘A’ kwa matukio 247, na wilaya ya Chake chake safari hii, ilipanda hnafsi moja, ingawa iliripoti matukio kiduchu 93, tofauti na matukio 113 ya mwaka 2024.

 

Waathirika wakubwa kwa mwaka 2025, ni watoto, waliokuwa 1,050 sawa na asilimia 85.4 kwa Unguja na Pemba, wakifuatiwa na wanawake 162 asilimia 13.2 na wanaume 18, sawa na asilimia 1.5.  

                         Mwisho

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’