SHEHIA YA MVUMONI YAPATA MSAIDIZI MPYA WA SHERIA

 



NA SAIDA ALI, PEMBA@@@@

MSAIDIZI mpya wa sheria shehia ya Mvumoni wilaya ya Chake chake Pemba, Haji Nassor Mohamed, ameuomba uongozi wa shehia hiyo, kumpa kila aina ya uhirikiano, ili kufanikisha majukumu yake.

 

Ameyasema hayo Novemba 29, 2025 alipokuwa akijitambulisha kwa wajumbe wa sheha, mara baada ya kuhamishiwa shehia hiyo akitokea Wawi, kwa lengo la kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria bila ya malipo.

 

Alisema kuwa, kubwa analohitaji ni ushirikiano kuanzia kwa sheha, wajumbe na wananchi wa Mvumoni, ili lengo la kuwahudumia wananchi lifikiwe.

 

Alieleza kua, ataendelea kuwa tegemeo kwa wananchi wa Mvumoni, kwani anaamini wapo ambao hawana uwelewa mpana, wa masuala ya kisheria.

 

‘’Kwanza nishukuru kwa kupokelewa, na ninachotaka kubwa zaidi ni umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwenu,’’alieleza.

 

Aidha Msaidizi huyo wa sheria, aliwakumbusha wajumbe hao wa sheha, kutokubali kuzifanyia sulhu kesi za jinai na hasa za udhalilishaji, na badala yake wawaelekeze wananchi kwenda mbele ya vyombo vya sheria.

 


Wakati huo huo Msaidizi huyo mpya wa sheria, alitumia fursa hiyo, kuwaelezea wajumbe hao kuwa, kesi za jinai na madai, zinatofauti kubwa, katika uendeshaji wake.

 

‘’Kwa kesi za madai, huwa baina ya mtu mmoja na mwingine, na lazima anaelalamika aandike madai yake, ingawa kwenye jinai husimamiwa na ofisi ya Mwendesha Mashtaka,’’alifafanua.

 

 Mapema Kaimu sheha wa Mvumoni Fatma Ali Khamis ameishukuru Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’, kwa kuwapelekea msaidizi wa sheria, kwani ilikuwa ndio kilio chao cha muda mrefu.

 

"Kuwepo kwa msaidizi huyu wa sheria shehiani mwetu, ni jambo kubwa kwetu, kwani utatuzi wa migogoro sasa utakuwa wa kisheria, ni tofauti na zamani tukitumia uzoefu tu,’’alisema.



Kwa upande wake Katibu wa sheha Khamis Mohamed na mjumbe wa shehiani humo Khamis Juma Mohamed walisema kuwa, ni jambo jema na faraja kupatiwa msaidizi huyo wa sheria.

 

Walisema kuwa, kujua sheria ni jambo muhimu sana  na kuahidi, kumtumia msaidizi huyo, ili kupata uwelewa wa haki zao hasa pale zinapoashiria kuvunjwa.

 

Wakati huo huo, uongozi wa shehia hiyo, umekubaliana na Msaidizi huyo wa sheria, kuendesha mafunzo wa siku moja, ya kuijengea uwezo kamati hiyo, yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii.

 


Ambapo mada tatu zilizopendekezwa ni haki za binaadamu, nani Msaidizi wa sheria pamoja na namna bora ya utatuzi wa migogoro ya mdai nje ya mahkama.

 

   MWISHO.

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’