WAGOMBEA CCM JIMBO LA CHAKE CHAKE, KUANZISHA WIKI YA MSAADA WA KISHERIA

 



 

NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

MGOMBEA Ubunge na Uwakilishi jimbo la Chake chake, wamesema kama wakipata ridhaa ya wananchi, wataanzisha wiki ya msaada wa kisheria jimboni humo, ili kuwasaidia wananchi, wenye changamoto za kisheria.

 

Walisema, wanayodhamira ya dhati kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo, wanaondokana na changamoto za kisheria, kwa kuanzisha wiki ya msaada wa kisheria, kila baada ya muda.

 

Wakizungumza na baadhi ya watendaji wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’, wakati walipofika ofisini hapo, walisema wanachosubiri ni ridhaa tu ya wananchi.

 

Wagombea hao walisema, wamebaini kuwa, ipo haja ya kuongeza nguvu ya kutoa elimu, msaada na ushauri wa kisheria kwa wananchi, na hilo litawezekana kwa kuanzisha wiki ya msaada wa kisheria.

 

Mgombea Uwakilishi Abdulla-wahabi Said Abubakar, alisema kwa kushirikiana na viongozi wenzake, na baada ya kukaa na uongozi wa ‘CHAPO’, azma hiyo wanayo.

 

Alieleza kuwa, kama Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, inayo wiki ya msaada wa kisheria kila mwaka, nalo jimbo la Chake chake, litaanzisha ya kwake kwa madhumuni yanayofanana.

 

Alisema, wapo wananchi wenye changamoto za kisheria kama vile watu wenye ulemavu, wazee, wanawake na hata vijana, hivyo kupitia wiki ya msaada wa kisheria, watapata ufumbuzi.

 

‘’Leo (jana), tuliseme tuitembelee ‘CHAPO’ na kufanya mazungumzo na baadhi ya watendaji na kisha kuonesha hisia zetu za kufanyakazi nao hapo baadae, kwa lengo lile lile la kuwasaidia wananchi,’’alifafanua.

 

Katika hatua nyingine, Mgombea huyo uwakilishi, alisema atakaa na viongozi wenzake, kuona CHAPO wanaisaidia baadhi ya vitendea kazi, ili iwahudumie wananchi kwa ufanisi.

 

Nae Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo Nassor Said Nassor ‘Maro’, alisema hataki kusikia hapo baadae, kuwa kuna mwananchi ndani ya jimbo hilo, analalamikia kukuosa msaada wa kisheria.

 

Alisema, anaifahamu vyema ‘CHAPO’ na utendaji wake wa kazi katika sheria za jimbo la Chake chake, hivyo kama akipata ridhaa, ataiunga mkono.

 

‘’Lengo letu ni kuona wananchi wale ambao wameshakata tamaa ya kukosa haki zao, waliomo jimbo la Chake chake, sasa wanasimama wima na kuzipata,’’alisema.

 

Aidha ‘Maro’, aliwaomba watendaji hao wa CHAPO kuhakikisha, wanakuwa waalimu kwa wingine, katika namna ya kutunza amani, iliyopo.

 

‘’Amani ndio yetu, kabla, wakati na baada ya uchaguzi, hivyo wasaidizi wa sheria, hilo endeleeni kulihubiri na muwafikishie na wingine,’’alifafanua.

 

Mapema Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Mwalimu Mohamed Hassan Abdalla, aliwaahidi wagombea hao, kuendelea kufanya nao kazi, kwa maslahi mapana ya wananchi.

 

Alisema, hata wasaidizi wa sheria wanahitaji amani katika kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria, hivyo atahakikisha, ujumbe huo anawafikishia na wingine.

 

Nao wasadizi wa sheria Jimbo la Chake chake, Wahida Kombo Khamis na Abeda Adi Seif, waliwatakia kila la kheir wagombea, hao na kurudi tena ofisini hapo.

 

Kwa upande wake, msaidizi wa sheria shehia ya Wesha Khadija Said Khalfan, aliwashauri wagombea, hao kuendelea kuhubiri amani, ili uchaguzi ufanyike kwa utulivu.

 

                               Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’