BODI CHAPO YANG'AKA UTORO, UVIVU WA WASAIDIZI WA SHERIA

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WAJUMBE wa Bodi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’, wamesema hawataki kusikia tena kuwa, wapo wasaidizi wa sheria, wamekuwa wavivu wa kufanya wajibu wao na kudharau vikao vinavyoitwishwa.

Walisema, kila mmoja anajua kuwa, CHAPO kama ilivyo wa jumuiya nyingine, ni eneo la kujitolea, sasa kama wako tayari kuendelea nayo, wahakikishe wanaendelea kuwahudumia wananchi.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo Safia Saleh Sultan, alisema wakati wanaomba kuingia kwenye sekta ya wasaidizi wa sheria, suala la kujitolea na kujitoa, ndio kigezo kikuu.

Alieleza kuwa, leo anashangaa kusikia kuwepo wasaidizi wa sheria ndani ya ‘CHAPO’, wamekuwa wavivu wa kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa jamii.

Alifahamisha kuwa, uvivu wao wa kufanyakazi na jamii, inaweza kupoteza mwelekeo kwa wananchi, na kuiangusha CHAPO, jambo ambalo akiwa Mwenyekiti, hataki kulisikia.

‘’Kila mmoja kuanzia sasa afanye wajibu wake, ambao ni kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria, kama ilivyokuwa sehemu ya vigezo vya kuwa msaidizi wa sheria hapo awali,’’alifafanua,

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Bodi, aliwataka wajumbe wa kamati tendaji ya CHAPO, kujenga ushirikiano wa utendaji miongoni mwao, ili wanachama wasiyumbe.

‘’Kamati tendaji ikiwa kitu kimoja, katika kutekeleza maagizo ya bodi pamoja na kuifuata katiba ya CHAPO, hata wale wanachama wenu watawaheshimu na kutekeleza wajibu wao,’’alisema.

Hata hivyo, aliwataka watunza fedha, kuhakikisha wanaweka ripoti zao sawa, na kufuatilia michango ya wanachama, ukiwemo ule wa kila mwisho wa mwezi.

Nae mjumbe wa bodi hiyo Kassim Ali Omar, alisema umoja na mshikamano wao, ndio utakaoifikisha mbali CHAPO, na kujenga uaminifu, kwa wananchi wa Chake chake.

‘’Wananchi wa Chake chake, wanaitegemea mno CHAPO kufikisha malalamiko yao ya kisheria, na kupatiwa ufumbuzi wa haraka,’’alifafanua.

Hata hivyo mjumbe huyo, nae aliwataka viongozi wa jumuiya hiyo, kuhakikisha kila mwanachama anafanyakazi yake kwa nia njema, ili kuwasaidia wananchi, hasa wasiokuwa na uwezo.

Kwa upande wake mjumbe Adam Abdalla, alisema hatojiskia vyema, CHAPO kufa yeye akiwa mjumbe wa bodi ya wadhamani.

Alifafanua kuwa, kama kuna mwanachama anajiona hawezi kuendelea na CHAPO akae pembeni, ingawa anaetaka kuendelea, afanye kazi zake bila ya kusimamiwa.

‘’Inawezekanaje msaidizi wa sheria, anakaa ndani ya shehia, mwezi mzima hajafanya kazi ya kutoa elimu wala msaada wa kisheria, lazima ajitathmini,’’alifafanua.

Mapema Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, alikiri kuyapokea maagizo ya bodi na kuyafanyiakazi, ili jumuia hiyo iendelee kuwategemeo kwa wananchi.

Aliwashukuru wajumbe hao, kwa kuwapa mwanga wa kufikia mafanikio ya CHAPO, kwani alikiri kuwa, kulikuwa na baadhi ya wanachama, wamesinzia kikazi.

Mkurugenzi Fedha wa CHAPO Riziki Hamad Ali, alisema amekuwa akijitahidi kuweka kumbu kumbu sawa, hasa malipo, ingawa utoro wa wajumbe, ndio changamoto.

Mratibu wa CHAPO Fatma Hilali Salum, alisema changamoto kubwa, ni wanajumuia kudharau vikao, na kusababisha wingine, kukosa maagizo na mipango inayoamuliwa.

‘’Wapo wanachama ni watoro, mnaweza kuamua jambo yeye hajui na wala haulizi, wakati wa utekelezaji ndio anaanza kulalamika,’’alifafanua.

Msaidizi wa sheria shehia ya Wesha Khadija Said Khalfan, alisema vikao kama hivyo, vinavyowahusisha wanachama na wajumbe wa bodi ni muhimu, katika kuiendeleza CHAPO.

Hata hivyo, aliwakumbusha wenzake, kuendelea kutoa michango yao, wanapokwenda kwenye mikutano na mafunzo, kupitia CHAPO.

CHAPO imekuwa na utaratibu wa kukutana na wanachama wake, kila mwisho wa mwezi, ili kupokea ripoti za utendaji kazi, pamoja na kuwasilisha ripoti ya fedha.

                           Mwisho   

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’