WASAIDIZI WA SHERIA WAWAREJESHA WANAFUNZI WATORO MASOMONI
NA MWANDISHI WETU, CHAPO@@@@
FAMILIA
mbili za shehia za Gombani na Ziwani wilaya ya Chake chake, wamewashukuru
wasaidizi wa sheria wilayani humo, kwa kufanikiwa kuwarejesha watoto wao
masomoni, baada ya kukatisha kwa zaidi ya miezi minne.
Walisema
tayari walishashindwa kuwanasihi na kuwatisha watoto wao ili kurejea masomoni,
ingawa hawakufanikiwa, na kuamua kuwatafuta wasaidizi hao wa sheria.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti wazazi hao, walisema walitumia
mbinu kadhaa ikiwemo kuwapeleka kwa askari wa ulinzi shirikishi, ingawa
hakuwafanikiwa.
Walisema,
waliwatumia askari wa shehia ili kuwanasihi na kisha kuwatisha, ingawa walikuwa
wanarejea masomoni kwa muda, kisha kuatisha tena.
Alisema,
walifika na kuzungumza nae, na sasa kijana wake amerejea masomoni skuli ya
Mbuzini kwa ajili ya kujiandaa na mitihani ya darasa la saba.
‘’Mtoto
wangu alishakaa nyumbani kwa zaidi ya miezi mitatu, alikuwa anaendelea kuvuna zao
la karafuu na tayari alishanunua simu, na ameshaniambia zaidi ya mara moja kuwa
hatorudi skuli, ingawa sasa nashukuru,’’alisema.
Mzazi
huyo, alisema kwanza anawashukuru wasaidizi hao wa sheria, kwa kufuata wito
wake wa haraka na kisha, kufanikiwa kumrejesga kijana wake masomoni.
‘’Kwa
sasa anaamka na kijihimiza mwenyewe kwenda masomoni, lazima niwashukuru
wasaidizi wa sheria kutoka CHAPO, kwa kazi hii,’’alisema.
Nae mzazi
Saada Abdalla Nassor wa shehia ya Gombani, alisema mtoto wake, aliacha masomo ya
darasa la 10, kwa zaidi ya miezi sita.
‘’Baada
ya kusikia kuwa, kuna wasaidizi wa sheria, niliwatafuta na niliwakabidhi mtoto wangu
na sasa amesharejea skuli ya Ng’ambwa,’’alieleza.
Mama
huyo, alisema kwa sasa ataendelea kuwa karibu na wasaidizi hao wa sheria hadi
hapo, mtoto wake atakapomaliza elimu yake ya lazima.
Msaidizi
wa sheria Fatma Hilali Salum, aliyefanikiwa kumrejesha mwanafunzi wa darasa la
saba skuli ya Mbuzini, alikiri kutumia mbinu za hali ya juu.
Alieleza
kuwa, baada ya kupata taarifa na wito ya mzazi huyo, jioni yake akiwa na baadhi
ya wasaidizi wa sheria walifika nyumbani kwa mtoto huyo, na kumnasihi na sasa
amerejea masomoni.
‘’Watoto
wingi ambao wamekatisha masomo ni wale ambao ndo za wazai wao, zimekatika, jambo
ambalo mzigo wa malezi humuangukia mama pekee,’’alisema.
Nae
msadizi wa sheria Haji Nassor Mohamed, aliyemrejesha mwanafunzi wa kidato cha
pili skuli ya Ng’ambwa, alisema nao wazazi wake, wameshaachana, na mama pekee kushindwa
malezi.
‘’Wajomba
wake wameshaingia kwenye nasaha, waalimu, Polisi na majirani lakini mtoto
alishindikana, hadi nilipofika na sasa amerejea skuli,’’alieleza.
Aidha Msaidizi
huyo wa sheria, alipofika skuli ya Ng’ambwa alioneshwa orodha ya wanafunzi zaidi
ya 35 wa madarasa tofauti, waliokatisha masomo skulini hapo.
Mkurugenzi
wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, aliwataka
wasaidizi hao wa sheria, kuendelea kuisaidia jamii, kwani ndio tegemeo lao.
Mkuu wa
wilaya ya Chake chake Mgeni Khatib Yahya, aliwataka wazazi na masheha kuendelea
kushirikiana na wasaidizi wa sheria, ili kutatua changamoto kadhaa.
Wakati hayo yakifanyika, upande mwingine
wizara ya Elim una Mafunzo ya Amali, imeongeza shilingi bilioni 11.5 kwa mwaka
2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 33.4 kwa mwaka 2024/2025.
Aidha ufaulu
wa wanafunzi vipawa na mchepuo kwa mitihani ya darasa la saba, umeongezeka
kutoka asilimia 5.5 mwaka 2020 hadi asilimia 27.5. kwa mwaka 2023.
Mwisho






Comments
Post a Comment