‘YALETENI MALALAMIKO YA KUVUNJIWA HAKI ZENU TUME’

  


NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WANANCHI wa shehia ya Mjananza wilaya ya Wete Pemba, wameshauriwa kuyafikisha malalamiko yao ya kisheria, yanayohusu uvunjwaji wa haki zao, kwa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora, ili kupata ufafanuzi.

Hayo yalieleza leo August 14, 2025 kijiji cha Mlalashi shehiani humo, na Mwanasheria kutoka Tume hiyo Pemba, Mohamed Massoud, wakati akielezea majukumu ya taasisi hiyo, kwenye mkutano wa wazi, ulioandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar.





Alisema, moja ya jukumu la tume hiyo, ambayo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kupokea, kusikiliza malalamiko mbali mbali ya uvunjifu wa haki wa binaadamu, tena bila ya malipo.

Alieleza kuwa, ofisi yao ambayo kwa sasa ipo Chake chake, inawakaribisha wananchi hao na wingine, ili kufika na kulalamikia, ikiwa wanaona kuna haki yao, iliyovunjwa.

‘’Kwa mfano umevunjiwa nyumba yako, kwa kupisha mradi wa kijamii kama barabara au ujenzi wa skuli na hakuna dalili ya kulipwa fidia, njoo na tutashirikiana,’’alisema.

Katika hatua nyingine, Mwanasheria huyo, aliwataka wananchi hao, wasiwe chanzo za kuvunjiana haki miongoni mwao, ikiwemo kuzifanyia sulhu kesi za jinai.



‘’Imekuwa ni kawaida, ikiwa kumetokezea ubakaji, hapo familia hukaa na kuanza kutafuta sulhu, ikiwemo kuwafungisha ndoa waliodhalilishana, jambo ambalo ni kosa jingine,’’aliafafanua.

Hata hivyo, aliipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria kwa kushirikiana na UNDP, kufanikisha mikutano hiyo katika baadhi ya shehia teule.

Kwa upande wake, Afisa sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Salma Bakar Abdulla, alisema mikutano hiyo ya wazi, lengo kuu ni kuwafikia wananchi na kuwafundish maana, chimbuko na zilikoanzia haki za binaadamu.



Alisema, imebainika kuwa, wananchi wamekuwa wakivunjiana haki za binaadamu, iwe kwa kujua ama kutokuelewa, na ndio maana, Idara hii na mshirika wake UNDP, imeamua kuwafikia wananchi moja kwa moja.

‘’Wananchi ni vyema fursa za mikutano kama hii, mkazitumia kwa kuuliza, kutaka ufafanuzi juu yao, ikiwa ni nachangamoto kadhaa, ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, migogoro ya ardhi na suala la fidia,’’alifafanua.

Mkuu wa divisheni ya Katiba na Msaada wa Kisheria Pemba, Bakari Ali Omar, alisema hata baada ya kumalizika kwa mikutano hiyo, wananchi wanatakiwa kuyafikisha malalamiko yao kwa wasaidizi wa sheria, ambao wamo katika shehia zao.



Alisema, kupitia kwa masheha unaweza kuwapata watendaji hao, ambao moja ya jukumu lao ni kutoa elimu, ushauri na msaada wa sheria bila la malipo.

Akifungua mkutano huo, sheha wa Mjananza Hamad Said Ali, alisema ujio wa wanasheria hao katika shehia yake, ni jambo jema, maana uwelewa wa sheria ni mdogo.





‘’Wananchi wa shehia hii, wingi wao uwelewa wa haki zao za kisheria uko chini, ingawa naamini mikutano kama hii, huwaamsha na kuwapa uwelewa zaidi,’’alifafanua.

Akitolea ufafanuzi suala lililoulizwa na wananchi, sheha huyo alisema ili mwananchi aingie kwenye mpango pensheni jamii, sio kwa ukongwe wake, bali vitambulishi vionyeshe amefikia miaka 70.

Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, ikishirikiana na ofisi ya Mwanasheria mkuu, Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora, pamoja na wasaidizi wa sheria, wameshawafikia wananchi wa shehia nane.

                   Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’