WANACHAPO WAPEWA MAFUNZO AKILI MNEMBA 'AI'

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WANACHAMA wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya akili ya kisayansi ‘akili mnemba’, baada ya watendaji wa wawili wa jumuiya hiyo, kumaliza mafunzo kama hayo, wiki iliyopita.

Kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, alisema utaratibu kwa sasa utakuwa kwa kila atakayerudi kwenye mafunzo, kuhakikisha anawapa na wenzake.

Alisema, mpango huo ulikuwepo zamani, ingawa katika siku za hivi karibuni, ulionekana kufa, na wakati umefika sasa kuufufua, ili kuona nguvu zinazotumiwa na washirika wao, zinaungwa mkono.

Akitoa mada ya mafunzo hayo ofisini kwao Chake chake jan August 17, 2025, alisema akili mnemba, ni mfumo wa kompyuta ambao umeshajazwa taarifa kadhaa, ambazo ni za ukweli, kwa ajili ya matumizi.

Alisema, utaalaamu baada ya kuendelea, mifumo hiyo hujazwa taarifa rasmi, na kisha kwa kutumia mifumo ya tovuti za ‘GPT’, unaweza kuipakua na kuuliza maswali au kutaka taarifa.

‘’Raha ya tovuti hii, unaweza kuiuliza taarifa ambazo zimeshachaktwa, na tayari kwa ajili ya matumizi ndani ya jamii,’’alisema.

Akizungumzia faida ya mifumo hiyo hasa kwa wasaidizi wa sheria katika kazi zao za kila siku, alisema ni pamoja na kujirahisishia wakati wanapoandaa mada.

Alifafanua kuwa, moja ya jukumu la wasaidizi wa sheria ni kuifikia jamii, na kutoa elimu iwe ya ardhi salama, mirathi, udhalilishaji, vyeti vya kuzaliwa na makundi ya watu maalum.

‘’Haya yote, kama huyajui kama yalivyo, unaweza kutumia mfumo huo wa ‘GPT’ na ukiomba unaweza kupata majibu halisi na kuyatumia ndani ya kazi zenu,’’alifafanua.



Mapema Mkurugenzi huyo, aliwapokea wasaidizi wapya wa sheria watano, ambao walimaliza mafunzo yao hivi karibuni, wakitokea shehia za Ng’ambwa, Mfikiwa, Ndagoni, Ziwani na Mjini Ole.

Hata hivyo aliwataka wasaidizi wa sheria wakongwe, kuwapa kila aina ya ushirikiano wenzao wapya, ili kuwafikia wananchi kuwapa elimu, ushauri na msaada wa kisheria.

Mapema Mkurugenzi fedha wa ‘CHAPO’ Riziki Hamad Ali, aliwakumbusha wasaidizi hao wa sheria, kuharakisha kuwasilisha ripoti kazi za utendaji wa kila mwezi.

Alisema wapo baadhi, wamekuwa hawawasilishi kazi zao kwa wakati, na kusababisha usumbufu wakati wa kuandika ripoti ya pamoja ya jumuiya.



Wakati huo huo, aliwapitisha kwenye fomu ya utoaji wa elimu na msaada wa kisheria, na kuwataka ikiwa watakwama, kuwasiliana na wenzao wakongwe kwa maelekezo.

Mapema wanachama wa CHAPO, walilipitisha jina la Fatma Hilali Salum, kushika nafasi ya Mratibu wa CHAPO, kuanzia August 17, ya mwaka huu.



Mara baada ya kupokea nafasi hiyo, aliomba ushirikiano wa karibu na watendaji wa CHAPO, ili kufikia malengo ya jumuiya yao.

Baadhi ya wasaidizi wa sheria akiwemo Jafari Abdalla Ali wa shehia ya Mgogoni na Abass Maalim Abeid wa Pujini, wamewahimiza wenzao, kuongeza juhudi za kuwafikia wananchi kuwapa elimu.

Hata hivyo, walipongeza kupatiwa mafunzo ya akili bandia, na kusema yatawasaidia kwa kiasi kikubwa, katika kazi zao kila siku, na hasa kuandika hati za madai.




Nae msaidizi wa sheria Saada Hamad Mbarouk wa Ole, alisema kuanzia sasa, atautumia mfumo huo wa kompyuta wa akili bandia, wakati anapotaka kuandaa mada zake.

CHAPO, imekuwa na utaratibu kila mwezi mara moja kukutana na watendaji wake, na kuelezeana mafanikio na changamoto za mwezi uliokwisha.

                       Mwisho  

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’