IDARA YA KATIBA NA MSAADA WA KISHERIA YAWAALIKA WANANCHI WAWI ELIMU YA KISHERIA LEO HII
NA HAJI NASSOR, PEMBA
WANANCHI wa shehia ya Wawi wilaya ya Chake
chake, wametakiwa kuitumia fursa ya kuhudhuria mkutano maalum wa elimu ya
kisheria, ulioandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, unaotarajiwa
kufanyika jioni hii ya leo shehiani humo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa Divisheni
ya Idara hiyo Pemba Bakari Omar Ali, alisema mkutano huo, ni maalum kwa ajili
ya wananchi hao, ili kuwapa elimu na msaada wa kisheria bila ya malipo.
Alisema, mkutano huo ambao utafanyika eneo la Kwa gerei
Wawi (Kwa Ali Haji) majira ya saa10:00 jioni, ni sehemu ya utendaji wa kazi wa kawaida wa Idara hiyo, katika
kuhakikisha jamii inapata muelekeo wa kutambua haki na wajibu wao kisheria.
Alieleza kuwa, zipo njia kadhaa za wananchi kujua haki zao
za kisheria, moja wapo ni kuwapelekea wataalam wa sheria ndani ya shehia, na
kuelezea changamoto zao za kisheria.
‘’Mkutano huu ambao unatarajiwa kufanyika jioni hii shehia
ya Wawi ni maalum, ili kuona wanapata uwelewa, lakini pia kuuliza na kutoa changamoto
zao za kisheria,’’alifafanua.
Mkuu huyo wa Divisheni ya Idara ya Katiba na Msaada wa
kisheria, alisema watalamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, watendaji wa Tume
ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora pamoja na wasaidizi wa sheria wa Chake
chake watajumika pamoja.
‘’Wataalamu hawa watahakikisha kila mwananchi atakaefika
kwenye mkutano wa leo, na akiwa anajambo lolote la kisheria atauliza na kupata
jawabu papo hapo,’’alisema.
Katika hatua nyingine, aliwahimiza wananchi hao, kuitumia
fursa hiyo, kwani kinyume chake wakiwafuata baadhi ya wanasheria watahitaji
fedha nyingi, ili kusikiliza na kuchambua changamoto zao.
Alisema, baada ya kupokea taarifa hiyo kutoka Idara ya
Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, alishakutana na kamati yake, na
wameshatoa taarifa kwa wananchi.
‘’Niliwatumia wajumbe wangu kutoa taarifa kwa wananchi wa makundi kadhaa, kama ya watu wenye ulemavu, watumishi wa umma, wakulima, waalimu wa vyuo vya qur-an na wanamichezo,’’alifafanua.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake
chake ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, alisema hiyo ni heshima kubwa kwa Idara
ya Katiba na Msaada wa Kisheria kuwapa fursa ya kuandaa mkutano huo.
Msaidizi wa sheria shehia ya Wawi, Fatma Hilali Salim,
aliwakumbusha wananchi wa shehia hiyo, kufika kwa wingi kwenye mkutano huo, ili
kupata ufafanuzi wa changamoto zao za kisheria.
Mjumbe wa sheha Nassor Rashid Said na Katiba wa sheha Sham
Haroub Said, waliipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, kwa uamuzi
wake wa kuandaa mkutano huo.
Mikutano kama hiyo, inatarajiwa kufanyika katika shehia za
wilaya ya Mkoani, Wete na Micheweni.
Mwisho



Comments
Post a Comment