WANANCHI 422,908 WAFIKIWA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA
NA HAJI NASSOR, UNGUJA@@@@
WANANCHI 422,908 wakiwemo wanawake 209,185 na
wanaume 213,723 wamefikiwa na elimu na msaada wa kisheria, kupitia kampeni ya msaada
wa kisheria ya Mama Samia, iliyomalizika hivi karibuni Zanzibar.
Kampeni hiyo, iliendeshwa katika mikoa yote mitano ya
Zanzibar, inayojumuisha wilaya 11, ambapo miongoni mwao kati ya waliofikiwa, ni
wanawake, watu wenye ulemavu, vijana, wazee na wanafunzi.
Hayo yalielezwa leo Julai 16, 2025 na Mwanasheria Mkuu
wa serikali ya Zanzubar, Mwinyi Talib Haji, kwenye hutuba yake, iliyosomwa kwa
niaba yake na Naibu Mwanasheria mkuu Shaaban Ramadhan Abdalla, kwenye kilele
cha maadhimisho ya jukwaa la tano, kilichofanyika Michenzani Mall.
Alieleza kuwa, serikali inafurahishwa mno kuona wananchi
walio wengi na wanyonge, wanaendelea kupata msaada, ushauri na elimu ya
kisheria bila ya malipo.
‘’Kwa hakika, uwepo wa kampeni hii, ni faraja kwa serikali
zote mbili, maana wananchi walio wengi wamekuwa wakikata tamaa, kupata haki
zao, ingawa kampeni kama hizi, husaidia kwa wananchi hao kupata haki zao,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mwanasheria huyo Mkuu wa serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema wakati wa kampeni hiyo, ipo migogoro 749 ilipokelewa
na 259 ikiwemo ya ardhi, mirathi, ndoa, ajira na talaka ilipatiwa ufumbuzi papo
hapo.
Aidha, aliipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria
Zanzibar, chini ya Mkurugenzi wake Hanifa Ramadhan Said, kwa kuendelea kusimamia
vyema upatikanaji wa haki.
Hata hivyo, aliipongeza UNDP na taasisi ya LSF, kwa
kuendelea kusaidia upatikanaji wa haki Zanzibar, jambo linaloleta faraja.
Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa
Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhann Said, akiwasilisha maazimio ya jukwaa hilo
kwa mwaka jana, alisema yapo ambayo yameshaanza kutekelezwa, ikiwemo azma ya
kuanzishwa kwa mfuko wa wasaidizi wa sheria.
Azimio jingime alisema, ni serikali na wadau wingine,
kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kuendelea majukwaa na wiki ya msaada wa
kisheria, jambo ambalo linaendelea kutekelezwa.
Alifahamisha kuwa, azimio jingine ni kuweka mazingira rafiki
ya upatikanaji wa elimu, kwa jumuiya, taasisi za msaada wa kisheria hasa suala la
uandishi wa miradi, ili kurahisisha upatikanaji wa fedha za kujiendesha.
‘’Lakini kupitia azma hii, niziombea hata jumuiya ya
wasaidizi wa sheria zote kutoka wilaya 11, zihakikishe zinawasilisha hadithi za
mafanikio kwetu, kwa ajili ya kuziingiza kwenye kitabu maalum,’’alifafanua.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka taasisi ya LSF ambae ni
Afisa Miradi Mwandamizi Bakar Hamadi, alisema wataendelea kuinga mkono Idara ya
Katiba na Msaada wa Kisheria, katika kuhakikisha jamii, inapata uwelewa na haki
zao.
Alieleza kuwa, kwa sasa ‘LSF’ inaendesha mradi wa ‘sauti
ya mwanamke’ ambao umejikita katika mapambano dhidi ya ukatili wa wanawake,
watoto na watu wenye ulemavu.
‘’Kwa mradi huu, kwa sasa unaendeshwa kwenye taasisi
mbili za Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Kaskazini Unguja ‘NAPAC’ na
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Micheweni ‘MIDIPAO’, kama eneo la majaribio,
ili baadaae inaweza kuzifikia taasisi zote.
Mapema akiwasilisha mada ya nafasi ya ufuatiliaji na
tathmini katika kuimarisha upatikanaji wa haki, Dk. Skujua Omar Hamdani, alisema moja ni kujua
mafanikio na changamoto za mradi husika.
Baadhi ya wachangiaji mada hiyo, walisema ufuatiliaji na
tathmini ndio kioo cha mradi, ili kujua kuwa wamefanikiwa wapi, na wamekosea
eneo gani.
Katika jukwaa hili la tano la mwaka la msaada wa kisheria
Zanzibar, ujumbe wa mwaka huu ni ‘Ufuatiliaji na Tathimini husaidia
kuimarisha ubora na ufanisi na huduma za msaada wa kisheria Zanzibar’.
Mwisho
Comments
Post a Comment