WANAFUNZI JIFUNZENI KUSEMA ‘NO’ MSIDHALILISHWE
WANAFUNZI wa skuli ya msingi na
sekondari ya kiislamu ya Amini, iliyopo Wesha wilaya ya Chake chake, wametakiwa
kujifunza kusema hapana, wanapoona kuna ishara za wao kutaka kudhalilishwa.
Ushauri huo, umetolewa leo Julai 14, 2025 na
Askari shehia Khamis Ali Khamis, wakati akizungumza na wanafunzi hao, kwenye
shamra shamra za wiki na jukwaa la msaada wa kisheria, mkutano ulioandaliwa na
Jumuiya ya wa saidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ na kufanyika
skulini hapo.
Alisema, wasiwe rahisi mno wanapoona kuna viashiria
vya udhalilishaji, hivyo wajifunze kwa vitendo neno la kukataa, ili kujikinga
na madhara makuwa zaidi.
‘’Niwaombe leo mkutano huu wa wazi ulioandaliwa na
wenzetu CHAPO, na tukiwa ndani ya wiki na jukwaa la msaada wa kisheria, ninawaomba
mjifundishe kusema hapana, mkihisi mazingira hayako salama,’’alisema.
Aidha, aliwataka wanafunzi hao, kuchukua muda mkubwa
wa kujisomea, kuliko jambo jingine lolote.
Nae Msaidizi wa sheria wa shehia ya Wesha Khadija
Said Khalfan, aliewataka wanafunzi hao, wanapokuwa na changamoto za kisheria,
wasisite kuwatumia wasaidizi wa sheria, kupata ufumbuzi bila ya malipo.
Alisema, karibu kila shehia, anakuwepo msadizi wa
sheria mmoja, na kwa kuanzia unaweza kumfika sheha na kurahisisha upatikanaji
wa watu hao.
‘’Sisi tupo kishehia, na tuko chini ya sheha, sasa
wewe mwanafunzi ukiwa umekumbana na mgogoro hata wa udhalilishaji, tutafute tusaidiane,’’alisema.
Mapema Msaidizi wa sheria mwalika kutoka shehia ya
Wawi Haji Nassor, aliwataka wanafunzi hao, kuwauliza wazazi wao, ikiwa
wanavyeti vya kuzaliwa ama laa.
‘’Ikiwa mzazi atakuambia huna, mwambie anzie kwa
sheha na kisha atafika wilayani, kwa ajili ya kupata haki yako hiyo ya lazima,’’alisema.
Hata hivyo, alisema cheti cha kuzaliwa, kwa sasa ni
jambo la lazima, kutokana na umuhimu wake, hasa kwa wanafunzi, ikiwemo kuombea
mikopo.
Akifunga mkutano huo, Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo Juma
Jumbe, aliishukuru ‘CHAPO’, kwa kuamua kuwafikia skulini hapo.
Alieleza kuwa, mikutano kama hiyo, inasaidia kuwapa
uwelewa wanafunzi, juu ya haki, wajibu wao kisheria.
Wakati huo huo Msaidizi wa sheria jimbo la Chake
chake Riziki Hamad Ali, aliwasisitiza wanafunzi wa skuli ya msingi ya Alswadiq,
kutojihusisha na vitendo viovu, kwani havina mwisho mwema kwao.
CHAPO, kwa sasa imo kwenye shamra shamra za jukwaa na
wiki ya msaada wa kisheria, baada ya kuzinduliwa na Julai 14, 2025 na Waziri wa
Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman.
Mwisho




.jpg)
Comments
Post a Comment