LSF: YATOA USHAURI WA BURE KWA JUMUIYA ZA WASAIDIZI WA SHERIA PEMBA
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MRATIBU wa taasisi ya ‘LSF’ kanda ya Zanzibar Hamisa Bakar Hamad, amesema kama jumuiya za wasaidizi wa sheria, hazikuungana wakati zinapotekeleza miradi, inaweza kuwa jambo gumu kufikia malengo ya miradi hiyo kwa jamii.
Alisema, jumuiya hizo zote ni zinamalengo yanayofanana ya kuisaidia jamii, hivyo ili kufikia malengo hayo hazinabudi, kushirikishana na kufanyakazi kwa pamoja.
Mratibu huyo wa kanda aliyasema hayo, ofisini kwake Madungu mjini Chake chake, kwenye mafunzo ya siku mbili kwa wanaasasi za wasaidizi wa sheria, katika kuutambulisha mradi wa suati ya mwanamke.
Alieleza kuwa, kama jumuiya zinaelekea kuisaidia jamii, hakunabudi moja inapotekeleza mradi husika, kushirikiana na nyingine.
Alifahamisha kuwa, sio busara kuona taasisi zilizojirani, moja inatekeleza mradi ambao mwenzake alishautekeleza miezi kadhaa iliyopita.
‘’Kwa mfano kama ‘CHAPO’ anatekeleza mradi wa afya ya mama, ni vyema na jirani yake ‘MDIPAO’, kuelekezana ili kusaidiana ushauri na maelekezo,’’alifafanua.
Akizungumzia mradi huo wa sauti yangu, Mratibu huyo wa ‘LSF’ kanda ya Zanzibar, alisema unalazimisha kuwepo kwa mshughulikiaji ‘focal person’ mmoja kutoka kila Jumuiya za wasaidizi wa sheria kisiwani humo.
Alisema lengo, ni kuona sauti ya mwanamke inanyanyuka iwe ni kwenye uchumi, kiukatili, udhalilishaji na kuongeza elimu.
Hata hivyo aliwataka wakurugenzi wa Jumuiya hizo za wasaidizi wa sheria, kuendelea kujenga ushirikiano na watendaji wao, ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.
Mapema Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, alisema mafunzo hayo yamewapa vitu vipya ikiwemo namna ya kujenga ushirikiano miongoni mwao.
‘’Ni kweli huwa kunautekelezaji mgumu wa baadhi ya miradi, ikiwa jumuiya moja na nyingine hazikuungana wakati wa utekelezaji,’’alifafanua.
Mussa Alawi kutoka ‘MDIPAO’, alisema bado vitendo vya udhalilishaji vipo ndani ya jamii, na kazi kubwa inahitajika kufanyika.
‘’Sisi wasaidizi wa sheria lazima tujengewe mbinu mpya na za kisasa, katika kukabiliana na janga hili na hasa kwenye utoaji elimu,’’alieleza.
Kwa upande wake Msaidizi wa sheria kutoka ‘WEPO’ Omar Abdalla Nassor, alisisitiza haja kwa wao, kujiendeleza kielimu, ili iwe rahisi kuvikabili vitendo hivyo.
Mafunzo mingine yanatarajiwa kufanyika kwa ajili ya Maafisa wa tathmini na ufuatiliaji wa jumuiya za wasaidizi wa sheria, ili kuelekeza namna ya ujazaji wa takwimu ndani ya fomu mpya.
Mwisho
Comments
Post a Comment