WASAIDIZI WA SHERIA, WAWI ZIWANI WACHANJA MBUGA
NA MWANDISHI WETU, PEMBA@@@@
JITIHADA za pamoja na endelevu zinahitajika, ili kuwajenga watoto katika mazingira ya malezi bora katika jamii, kwa lengo la kujinasua na majanga yanayowazunguruka.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Msaidizi wa Sheria kutoka shehiya ya Wawi Haji Nassor Mohamed, alipokuwa akiwasilisha mada juu ya haki za watoto na wajibu wao, kwa wanafunzi wa Almadrassatul- Muuminina Syyidat Aishaa, iliyopo Fletini shehia ya Wara wilaya ya Chake chake.
Alisema kila mmoja ana haki zake na wajibu wake katika maisha ya kila siku hivyo kukiwa na malezi ya pamoja, jamii itakuwa na mazingira bora ya kuishi kwa watoto wa leo na kesho.
”Haki zenu watoto moja wapo ni kupatiwa elimu kama hii ya Madrassa,skuli, pia kupewa majina mazuri, kupatiwa huduma nyengine mbali mbali ambazo haziharibu taratibu za mila na desturi,"alisema.
Katika hatua nyingine, Msaidizi huyo wa sheria shehia ya Wawi, Haji Nassor Mohamed, aliwataka wanafunzi hao kufuata maadili ya kujisomea kwa bidii, ili kuepuka vishawishi vitakavyo wahatarishia maisha yao na ndoto zao.
Kwa upande wake Msaidizi wa sheria wa shehia ya Wara Sabahi Abdalla, aliwaasa wanafunzi hao kuacha mara moja kutumia simu, kwani muda wao kwa sasa haujafika.
"Nyinyi kwa sasa hampaswi kuwa na simu, kwani hamna haja ya kutumia simu na wale ambao huwa wanazichukua simu za wazazi wao, wache tabia hiyo kwani haina faida kwao,"alifahamisha.
Nao wanafunzi wa Madrasa hiyo Nurdin Abdalla na Mudrik Mohamed, walisema wamefaidika na mada zilizotolewa na kuwata wanafunzi wenzao kuacha, yale yote ambayo yanakwenda kinyume na maadili.
Mapema Mwalim mkuu wa Madrasa hiyo Fatma Rashid, aliwashukuru wasaidizi hao wa sheria, kwa kufika katika Madrasa hiyo, kwajili ya kutoa elimu ya kisheria kwa wanafunzi.
Akifungua mkutano huo wa wazi, Msaidizi wa sheria kutoka shehia ya Mgogoni Jaffar Abdalla Ali, aliwakumbusha wazazi na walezi, wenye watoto katika Madrassa hiyo, kuongeza ushirikiano na waalimu.
Timu ya wasaidizi wa sheria ya kanda ya Wawi na Ziwani, chini ya Mwenyekiti wake Haji Nassor Mohamaed, inaendelea kuyafikia makundi ya kijamii, ili kutoa elimu, msaada na ushauri wa kisheria bila ya malipo.
Ambapo tayari, timu hiyo imeshafika vijiji vya Tondooni shehia ya Wesha, Fletini shehia ya Wara na Mgogoni shehia ya Mgogoni na Febuari 1, mwaka huu ni kijiji cha Fidel Castro shehia ya Wawi.
MWISHO
|





Comments
Post a Comment