CHAPO: ‘WASAIDIZI WA SHERIA ONGEZENI BIDII KUWAFIKIA WANANCHI’
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WASAIDIZI wa sheria wilaya ya Chake chake, wamekumbushwa kuongeza bidii ya kufikia jamii, ili kuwapa elimu, msaada na ushauri wa kisheria bila ya malipo, kwa vile ndio ahadi ya kazi yao hiyo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilayani humo Mohamed Hassan Abdalla, wakati akizungumza na watendaji hao, kwenye kikao cha mwezi cha kawaida, kilichofanyika ofisini kwao mjini Chake chake.
Alisema, kila msadizi wa sheria anaelewa wajibu huo, hivyo ni vyema kuendelea kuifanyia kazi kwa bidii, kwani wananchi waliokata tamaa ya kupata hazi za kisheria, wanawategemea wao, kutokana na kukosa uwezo wa kuwafikia wanasheria.
Alieleza kuwa, wajibu huo wakiuupuza na kuusahau wajue fika kuwa, wanawakosesha haki wananchi wingine hasa wale wenye kipato cha chini, ambao kwa kiasi kikubwa wananategemea wao.
Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa, ijapokuwa kazi kubwa kwa mwaka 2024 ilifanywa na wasaidizi wa sheria hao, lakini ni vyema wakaongeza juhudi ya kazi yao.
‘’Niwaombe sana wasaidizi wa sheria kuendelea kuongeza nguvu na jitahada za maksudi, ili kuona idadi ya wananchi waliofikiwa kwa mwaka 2024, ndani ya mwaka huu inakuwa kubwa zaidi,’’alieleza.
Katika hatua nyingine amewakumbusha wasaidizi hao wa sheria wakongwe, kufanyakazi kwa karibu na wale wapya, ili nao wavune uzoefu kutoka kwao.
Hata hivyo, alisema wakati umefika sasa kwa wasaidizi wa sheria, kuongeza elimu ya kisheria, ili iwe rahisi wanapokumbana na changamoto za utatuzi wa kisheria, kuzitatua.
Mapema Mkurugenzi fedha wa Jumuiya hiyo ya wasaidizi wa sheria wilaya hya Chake chake CHAPO, Riziki Hamad Ali, alisisitiza haja ya umoja na mshikamano miongoni mwao.
Nae Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka CHAPO Wahida Kombo Khamis, aliwakumbusha wasaidizi hao wa sheria, kuwasilisha mapema ripoti zao za kile mwezi.
‘’Suala la kuwasilisha ripoti ya msaidizi wa sheria mmoja mmoja, limekuwa ni changamoto, sasa tujitahidi kuhakikisha kila mwisho wa mwezi, ili kuandaa ripoti ya pamoja,’’alifafanua.
Nae msaidizi wa sheria shehia ya Mgogoni Jaffar Abdalla Ali, aliwakumbusha wasaidizi hao wa sheria, kuzingatia muda wanapopanga vikao kazi.
Nae Msaidizi wa sheria shehia ya Kilindi Juma Seif Haji, aliomba kuendelea kufanya kazi ya kutoa elimu kwa timu, ili kuwaoa uwezo na na uwelewa wingine.
Kwa upande wake msaidizi wa sheria kutoka shehia ya Wawi Fatma Hilali Salum, alipendekeza kuanza vikao kwa muda uliopangwa, ili kuwa watumiaji wazuri wa muda.
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba, CHAPO inaendelea kukutana na wananchi mbali mbali katika shehia zote 32 kwa ajili ya kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria bila ya malipo.
Mwisho





Comments
Post a Comment