CHAPO: 'WAZAZI ONGEZENI ULINZI KWA WATOTO KIPINDI HICHI CHA MAPUMZIKO'
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MKURUGENZI wa Jumuiya ya Wasaidizi wa
sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, amewataka
wazazi na walezi, kuwa makini na kufuatilia nyenendo za watoto wao, kwa kukinga
na majanga kama ya uudhalilishaji, hasa kipindi hiki cha mapunziko ya masomo.
Alisema, wahalifu waliowengi wamekuwa wakijisogeza na
maeneo ya watoto wanamopenda kucheza cheza, hivyo ni vyema kwa wazazi na walezi
wakaimarisha ulinzi mara dufu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi leo Novemba 15, 2024, Mkurugenzi huyo,
alisema wakati huu wa skuli zikiendelea na mitihani ya taifa, kundi kubwa la
watoto wapo majumbani, hivyo ni vyema ulinzi ukaimarishwa.
Alieleza kuwa, wadhalilishaji wanaweza kujichanganya
na watoto wakiwa kwenye michezo mbali mbali, hivyo ni wajibu ulinzi dhidi yao,
ukaongezwa.
‘’Nitowe wito na tahadhari kwa wazazi na walezi,
katika kipindi hiki wakiwa watoto hawaendi masomoni, na kutawanyika mtaani hovyo
hovyo, ni kuongeza ulinzi, ili tusiwape nafasi wahalifu,’’alieleza.
Mkurugenzi huyo wa ‘CHAPO’ alifafanua kuwa, wazazi
wasipendelee kuwaachia watoto kwa watoto wenzao, na badala yake, hali ikiruhusu
awepo mtu mzima.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo, alisema hata
ndani ya majumba ni vyema kila mmoja, akawa mlinzi kwa mwenzake, maana zipo
kesi za baba kumdhalilisha mtoto wake.
‘’Kesi hadi mahkamani zimeshafikishwa kwa baba,
kaka, mjomba na ami kumdhalilisha mtoto wake, sasa ulinzi uimarishe ndani ya
nje,''alishauri.
Hata hivyo aliwataka wasaidizi wa sheria wilayani
humo, wanapokutana na jamii, kulieleza hilo ili tahadhari hiyo ichukuliwe kwa
upana wake.
Sheha wa shehia ya Wesha Haji Mohamed Ali, aliwataka
waratibu wa shehia, kukutana na watoto waliomo ndani ya shehia zao, ili kuwapa tahadhari
hiyo.
Katibu wa sheha, shehia ya Wawi Sham Haroub Said,
aliwakumbusha watoto, kwenda madrassa na kurudi kwa kundi, ili isiwe rahisi kwa
mdhalilishaji, kutimiza malengo yake.
‘’Njia nyingine baada ya wazazi na walezi kuimarisha
ulinzi, ni watoto wasipendelee kwenda mmoja mmoja, na wafuatane wanapokwenda na
kurudi masomoni,’’alishauri.
Kwa upande wake Katibu
wa kamati ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji wilaya ya Chake chake,
Rashid Said Nassor, aliitaka jamii, kuendelea kuwalea watoto katika misingi yenye
maadili, ili wajiepushe na kujiingiza kwenye vitendo vibaya.
‘’Ni kweli skulini
nyingi zimeafungwa na watoto wako mtaani, lakini kwanza ni tahadhari kwao na
wadhalilishaji, pili tuendelee kuwapa elimu ya kujitambua, ili wawe raia wema,’’alipendekeza.
Mkuu wa Mkoa wa kusini
Pemba Mattar Zahor Massoud, aliendelea kuwataka masheha kutozitia mkono kesi za
udhalilishaji, na badalayake wazifikishe mbele ya vyombo vya sheria.
‘’Sheha yeyote atakaebainika
kuziingilia kesi za udhalilishaji, kwanza hana kazi pili vyombo ya sheria
vitakuwa vinamuhusu kwa njia moja ama nyingine,’’alieleza.
Mwanaharakati wa haki
za wanawake na watoto Pemba Tatu Abdalla Msellem, aliwataka akinababa kusaidia
malezi ya watoto, na sio kumuachia mwanamke kwa kisingizio cha kutafuta maisha.
Mjumbe wa baraza la
watoto shehia ya Wawi Omar Mohamed Hassan na mwenzake wa Wesha Asha Taimur Hussein,
walisema bado adhabu kwa wanaowadhalilisha watoto ni ndogo.
‘’Ndio maana kila
siku, tunaripotiwa kubakwa, kulawitiwa na kufanyiwa ukatili wa kipigo, maana
wanaotiwa hatiani, hawafungwi kifungo kirefu kama sheria ilivyo,’’walisema.
Akiwasilisha hutuba ya bajeti ya mwaka wa
fedha 2023/2024 Wiziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Riziki
Pemba Juma, alisema wameshaandaa mpango kazi mpya wa kupambana na vitendo vya
ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto.
Alifahamisha kuwa, mpango huo (NPA-VAWC
wa mwaka 2023/2028), unalengo la kuhamasisha na kuelimisha jamii, juu ya kupambana
na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto katika ngazi zote.
Jingine alisema ni kuandaa Sera ya
Maendeleo ya Jamii, pamoja na miongozo ya utoaji wa huduma za maendeleo ya
jamii, kuratibu na kuhamasisha utekelezaji wa ahadi za nchi juu ya kizazi chenye
usawa pamoja na kuhamasisha jamii kuimarisha malezi ya pamoja, yenye lengo la
kuwatenga na vitendo viozuvu.
Mwisho

Comments
Post a Comment