WANA 'CHAPO' WAPEWA RAI, KUMKUMBUKA ALIYEKUWA MKURUGENZI WAO
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANACHAMA wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria
wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’, wametakiwa kuendelea kumuombea dua kila wakati,
aliyekuwa Mkurugenzi wao Nassor Bilali Ali, na kisha kuiendeleza na kuisimamisha
jumuia yao.
Wito huo umetolewa leo Augost 17, 2024 na Mratibu Ofisi ya Mufti Pemba, sheikh
Said Ahmad Mohamed, kwenye hutuba yake iliyosomwa kwa niaba yake, na sheikh
Said Abdallah Nassor, mara baada ya kumalizika kwa dua ya kuombea marehemu huyo,
iliyofanyika ukumbi wa Manispaa ya jiji la Chake chake.
Alisema, mara baada ya mtu kufariki, yapo mingi yanaweza kumsaidia
na moja wapo ni dua za mara kwa mara, kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki zake.
Alieleza kuwa, huu sio wakati kwa wanacha CHAPO, kugawanyika
kufuatia kifo cha Mkurugenzi wao, bali waendelee kushikamana, huku wakimkubuka mwenzao
kwa dua.
Sheikh Said Ahmad Mohamed, alisema kifo cha Mkurugenzi huyo,
kamwe kisiwe sababu kwa wao, kufarikiana na kugawanyika makundi mawili, bali
sasa waoneshe umoja wao kwa vitendo.
‘’Mimi nilikuwa namfahamu mno marehemu Nassor Bilali Ali,
namna alivyokuwa akipambania haki za wanyonge, sasa kazi hiyo muendeleze mliopo,
huku mkikumbuka kumuombea dua kila wakati,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, Mratibu huyo wa Ofisi ya Mufti Pemba,
sheikh Said Ahmad Mohamed, alisema mfano wa jumuiya kama ya CHAPO, namna inavyopigiania
haki za waliozulumiwa, inafaa kuungwa mkono na kila mmoja.
Aidha aliwataka wanafamilia, CHAPO, ndugu na jamaa wa
marehemu, kuwa na moyo wa ustahamilivu katika kipindi hiki, kwani kifo ni haki
ya lazima isiyokuwa na muda maalum.
Akizungumza kwa niaba ya jumuiya za wasaidizi wa sheria
Pemba, Msaidizi wa sheria kutoka wilaya ya Mkoani Khamis Mohamed Yahya,
alimtaja marehemu kuwa aliwaunganisha watu wote.
‘’Pamoja na kwamba marehemu Nassor, alikuwa ni wa CHAPO
lakini, mara zote akipendelea zaidi kutuunganisha na kutupanisha pale penye mifarakano,’’alifafanua.
Hata hivyo, wameahidi kuwa, wataendelea kuwa karibu na wana CHAPO,
ili kuona hakuna jambo linalotetereka, kwa sababu ya msiba huo.
Nae Mjumbe wa bodi ya CHAPO, Adam Abdalla alisema kifo cha
Nassor Bilali Ali, hakikuleta mtikisiko kwa familia yake pekee, bali kwa kila
taasisi.
Alifahamisha kuwa, marehemu aliamua kujitoa kwa dhati ya moyo
wake, na alihakikisha siku zote, kila aliyenyimwa haki yake anaipata, tena kwa
wakati.
‘’Leo kila mmoja ni shahidi kuwa, wapo watu kadhaa ambao
walishakata tamaa, aidha mahakamani, Polisi au kwenye migogoro ya ardhi, na
walipofika kwake haki ilipatikana,’’alifafanua.
Hata hivyo aliwaahidi wanajumuiya hiyo ya wasaidizi wa
sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ kuendelea kuwa nao bega kwa bega,
ili jumuia hiyo isilale.
Baadhi ya wadau waliohudhuria dua hiyo, walisema marehemu
wanamkumbuka kwa mingi mazuri, likiwemo namna alivyokuwa, mstari wa mbele
kujitolea.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba ‘TUJIPE’ Tatu Abdalla
Msellem, alisema walifanikisha kazi nyingi na marehemu, kutokana na ujasiri
wake.
Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania
TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said, alisema kila mara walipokuwa
wanashughuli za kujitolea, hakuridhika kama hakumpata marehemu.
Marehemu Nassor Bilali Ali, ambae alikuwa Mkurugenzi wa
Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba CHAPO, alifariki
Augost 7, mwaka huu wakati akiwa uwanja wa ndege kwa safari ya kwenda
matibabuni Unguja, baada ya kuugua ghafla.
Kisha marehemu alizikwa kijijini kwao, Vikunguni wilaya ya
Chake chake siku hiyo hiyo, majira ya saa 11:15 jioni, Mwenye Muungu…. ailaze roho
ya marehemu pahala pema peponi aminaaa…
Mwisho
Comments
Post a Comment