MAMIA WAMZIKA MKURUGENZI 'CHAPO' SALAMU KILA KONA ZAMIMINIKA

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WASAIDIZI wa sheria wilaya ya Chake chake, wamesema wamepokea salamu za pole kutoka, maeneo kadhaa hapa nchini, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wao, Nassor Bilali Ali, kilichotokea Augost 7, kisiwani Pemba.

Akizugumza na waandishi wa habari, Mratibu wa Jumuiya hiyo Mohamed Hassan, alisema miongoni mwa salamu hizo ni kutoka Afisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utawala Bora Zanzibar.

Salamu nyingine, ni kutoka wafanyakazi wa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria wa Unguja na Pemba, kupitia Mkurugenzi wao Hanifa Ramadhan Said, taasisi za haki za binadamu za Tanzania bara na Zanzibar.

Maratibu huyo wa CHAPO alieleza kuwa, salamu nyingine za kuwatakia moyo wa ustahamilivu, zimetolewa na wakurugenzi na wajumbe wa bodi za jumuiya za wasaidizi wa sheria za Unguja na Pemba.



Aidha Hassan alisema kuwa, kufuatia kifo hicho, watetezi wa haki za binadamu Pemba, kutoka jumuia za PACSO, TAMWA, ZALHO, Jeshi la Polisi, Mahkama, Mawakili wa kujitegemea na wale wa serikalini, nao wametuma salamu zao.

Akizungumzia kifo cha marehemu Nassor Bilali Ali, alisema juzi alipata taarifa ya kuugua kwake na kukimbizwa hospitali ya wilaya ya Chake chake, iliyopo Vitongoji.

Alifafanua kuwa, baada ya hali kuwa mbaya, alipata uhamisho na kufikishwa hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani kwa matibabu zaidi, na kulazwa usiku mmoja.

Siku ya pili yake, (Augost 7), alipatiwa rufaa ya kimatibabu kwenda hospitali ya Mnazi mmoja Unguja, na wakati akiwa uwanja wa ndege wa Pemba, majira ya saa 3:50 hali ilibadilika na kufariki dunia.

Akizungumza kwa njia ya simu, Mkuu wa Divisheni ya Katiba na Msaada wa Kisheria ofisi ya Pemba Bakar Omar Ali, alimtaja marehemu kuwa, alikuwa mchapakazi kwa saa 24.

Alisema, moja ya wakurugenzi waliofanikiwa kuiinua jumuia ya wasaidizi wa sheria, alikuwa na Nassor wakati wa uhai wake, jambo lililochangia kupata tunzo kadhaa.

Mjumbe wa Bodi ya ‘CHAPO’ Zuwena Hamad Ali, alisema ni pengo kubwa, kifo hicho ingawa ni kazi Muumba, siku zote huwa haina makosa.



Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani ‘MIDIPAO’ Nassor Hakim Haji, akizungumza kwa niaba ya wakurugenzi wenzake, alisema marehemu alikuwa tegemeo sio tu kwenye ‘CHAPO’ lakini kwa jumuiya zote.

‘’Alikuwa mwenyeji, anaejiamini, anaejua mambo, aliyekuwa akipenda kujitolea na siku zote alikuwa anatuusia umoja, mshikamano, ukweli na ushirikiano,’’alifafanua.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu Tanzania (THRDC), nao umesema umepokea kwa mshtuko kifo hicho cha mwanachama wao, na kuitaka familia, ndugu, wana CHAPO kuwa wavumilivu katika kipindi hichi kigumu.

Mwenyekiti wa taifa wa Mtandao wa utetezi wa haki za watoto Tanzania’ MUHUWATA’, John Joseph Malale, wamewataka wanacha CHAPO na familia yake, kuwa wavumilivu katika kipindi.

‘Nassor alikuwa zaidi ya mwanaharakati wa haki za  watoto, alikuwa zaidi ya msaidizi wa sheria, daima alikuwa anatuongoza hata sisi viongozi na unapomka kazi hakuwa tayari kumshinda,’’inafafanua taarifa hiyo.



Marehemu Nassor Bilali Ali, alizikwa siku hiyo hiyo kijiji kwao Vikunguni wilaya ya Chake chake Pemba, ambapo viongozi kadhaa na watu maarufu, wasaidizi wa sheria, wanasheria na mawakili walishiriki kwenye mazishi hayo.

Kabla ya kukumbwa na umauti huo, Nassor alipata elimu ya usaidizi wa kisheria baina ya mwaka 2012/2013, na kisha baada ya kuanzishwa kwa CHAPO, alichaguliwa nafasi ya Mkurugenzi, kwa vipindi tofauti, kuanzia mwaka 2016 hadi umauti unamkuta.

                         Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’