CHAPO: 'WANANCHI UCHANGANI JENGENI URAFIKI NA WATOTO WENU MTAYAPATA MINGI '

 

 
NA MWANDISHI WETU, PEMBA@@@@


WANANCHI wa kijji cha Uchangani shehia ya Ndagoni wilaya ya Chake chake Pemba, wametakiwa kujenga urafiki endelevu na watoto wao, ili kugundua kwa haraka, ikiwa wanakumbana na changamoto zikiwemo za udhalilishaji.

Ushauri huo umetolewa Augost 6, 2024 na Msaidizi wa sheria wa shehia za Wesha na Ndagoni, Khadija Said Khalfan, wakati akizungumza na wananchi hao, kwenye mkutano wa wazi ulioandaliwa na Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria ‘CHAPO’.

Alisema, mbinu nzuri kwa wazazi na walezi, ya kugundua mazito wanayopitia watoto wao, wanapokuwa skuli au madrassa, ni kujenga nao urafiki endelevu.

Alieleza kuwa, kupitia mpango huo mzazi au mlezi, anaweza kumuuliza maswali kadhaa na majibu yake, yanaweza kumpa mwanga na kujua aina ya marafiki na mwenendo wa mtoto wake kwa ujumla.



Alifahamisha kuwa, sio kinga kwa wazazi na walezi, kulalamikia ugumu wa maisha na kuacha kuwatunza watoto na kuwa nao karibu, kwani mazingira yasiorafiki yanazidi kutawala kwa sasa.

‘’Ni kweli, wazazi sasa wako na harakati ngumu za maisha, lakini na watoto nao wanahitaji kutunzwa, na njia moja wapo ni kujenga urafiki, ambao utakuwezesha mzazi kugundua yaliojificha kwa mtoto wako,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, Msaidizi huyo wa sheria, aliwashauri wazazi hao, kutowaruhusu watoto wao kukogeshana wenyewe, bila ya mzazi kufanya kazi hiyo, kwa baadhi ya siku.

Mapema Askari wa shehia za Wesha na Ndagoni Khamis Ali Khamis, aliwatahadharisha wazazi na walezi, hao juu ya watoto wao kutumiwa na wasafirishaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya.



‘’Sasa wale wanaotumia dawa za kulevya, wameanzisha ujanja wa kuwatumia watoto, wakijua kuwa hata wakikamatwa nazo, hawawezi kutiwa hatiani, sisi wazazi tuwe makini na hili,’’alifafanua.

Nae Msaidizi wa sheria wa shehia ya Wawi Haji Nassor Mohamed, amewakumbusha wazazi kuwa, hadi sasa kwa mujibu wa sheria, mtoto anatambulika ni mtu yeyote aliyechini ya miaka 18.

‘’Kwa mantiki hii, tunaendelea kutahadharisha kwa wale wadhalilishaji, hakuna kinga kwa eti mtoto huyo, kaja mwenyewe kwenye nyumba, na kisha kufanya nae tendo la ngono, bado kisheria inaitwa ni ubakaji,’’alifafanua.



Aidha Msaidizi huyo wa sheria, amewatahadharisha wazazi na walezi, kutothubutu kuwafungisha ndoa watoto wao waliobakwa, kama njia ya kuyatengeneza.

Wananchi wa kijiji hicho, akiwemo Ali Sharif Khamis, alisema bado hukumu hazijakuwa kubwa, kama sheria inavyoelekeza, na ndio maana, matendo ya udhalilishaji yanaendelea kuripotiwa.

Nae ustadhi Salim Khamis Salim, alisema kama jamii haikuyarejesha malezi ya pamoja, suala la kupunguza majanga kwa watoto, litaendelea kuwa ndoto.








Mwananchi Fatma Hamad Khamis, alisema bado njia za kupitishiwa dawa za kulevya, hazijalindwa ipasavyo, na ndio maana vijana wanaendelea kuzitumia.

‘’Zanzibar dawa za kulevya hazizalishwi wala hazilimwi, sasa inakuaje wanaofanya biashara hii, wanatuletea, tusema ulinzi haupo vizuri katika bandari zetu na uwanja wa ndege,’’alihoji.

Akiufunga mkutano huo, Naibu sheha wa kijiji hicho Hazina Musheha Omar, alisema kazi zinazofanywa na wasaidizi wa sheria, na kama zitaungwa mkono, jamii inaweza kuondokana na changamoto mbali mbali.







Aidha aliwahakikishia wasaidizi hao wa sheria, kuyafanyia kazi maagizo walioyoyatoa, ikiwa ni njia moja wapo ya kuwalinda watoto wao na ukatili na udhalilishaji.

                                   Mwisho   

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’