‘WANAWAKE MSIONGOZE VIKAO VYA SULHU KESI ZA UDHALILISHAJI’
NA ALI KHAMIS, PEMBA@@@@
MJUMBE wa sheha wa shehia ya Wawi wilaya ya
Chake chake, Mwanajuma Bakar Mohamed, amewataka wanawake wa kijiji cha
Mchekeweni, wasikubali kuongoza vikao vya sulhu, inapotokeza changamoto ya udhalilishaji
wa watoto.
Alisema, imebainika wapo baadhi ya wanawake wamekuwa ndio
watandikaji majamvi na mikeka, ili kuandaa mchakato wa sulhu, kwenye kesi za
udhalilishaji.
Mjumbe huyo, aliyasema hayo jana kwenye madrassa ya wanawake
iliyopo kijijini hapo, wakati wa mkutano wa wazi, ulioandaliwa na Jumuiya ya
wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’, ikiwa ni mkutano wa kawaida
wa utoaji wa elimu.
Alieleza kuwa, ni vyema sasa wakakimbilia vituo vya
kisheria, ili kutoa taarifa haraka, mara tu inapotokeza changamoto ya ukatili
na udhalilishaji.
‘Sisi akinamama, ni kweli tumeumbwa na huruma kubwa,
lakini sio katika eneo hilo, na wala tusijihusishe na sulhu, kwani kufanya
hivyo, ni kumuuza mtoto wako kwa thamani ndogo,''alieleza.
Katika hatua nyingine, Mjumbe huyo wa sheha, aliwataka
wananchi wake, kuwatumia wasaidizi wa sheria waliomo shehia ya Wawi, ili kupata
ushauri na msaada wa kisheria bila ya malipo.
Hata hivyo alisisitiza haja, kwa wananchi kuhudhuria
kwenye mikutano kadhaa, inayoitishwa na wasaidizi wa sheria, ili kuongeza
uwelewa wao.
Mwalimu wa Madrassa hiyo ya wanawake kijijini hapo Snei Hamad
Khamis, alisema kazi inayofanywa na CHAPO, inasaidia kuibua changamoto za ukatili
na udhalilishaji kwa watoto.
Mapema Msaidizi wa sheria, shehia ya Wawi Haji Nassor
Mohamed, aliwakumbusha wananchi, kuacha kununua ardhi kiholela, ili kuepusha
miogoro.
‘’Huwezi kununua ardhi kama muuzaji, hujajiridhisha yeye
aliipataje ardhi husika na kama ana hati zinazokubalika za matumizi, vyenginevyo
unaweza kucheza mchezo wa kubahatisha,’’alifafanua.
Aidha, aliwaeleza wanawake hao kuwa, kuendelea kuwachunga
watoto wao wa kiume, kwani dunia ya sasa imakabiliwa na changamoto kadhaa,
ikiwemo ukatili na udhalilishaji.
‘’Hapa niwakumbushe kuwa, kisheria mtoto ni mtu yeyote
aliyechini ya miaka 18, sasa ni wajibu wa wazazi kisheria, kuhakikisha hakumbwi
na janga lolote,’’alisisitiza.
Hata hivyo Msaidizi huyo wa sheria, aliwakumbusha
wanawake hao, kuwatumia wasaidizi wa sheria wanapokumbwa na kesi za madai,
kabla ya kufika mbele ya vyombo ya sheria.
Akiufunga mkutano huo, Sheha wa shehia ya Wawi Sharifa
Abdalla Waziri, aliwaeleza wanawake hao, kuwa mfano bora ndani ya jamii yao,
kimaadili.
Aidha, aliwataka vijana wanaoishi shehia ya Wawi, kutoa
taarifa kwa wenzao, wanaotumia dawa za kulevya, au kuingiza na kusafirisha.
Baadhi ya wanawake hao, walisema bado migogoro ya ardhi
inawaumizwa kichwa, kwa kuwepo wavamizi wa maeneo yao, pasi na nyaraka
zinazotambulika.
‘’Inawezekana unalima sehemu kwa zaidi ya miaka 40, kisha
anakujia mtu ana karatasi, ambazo hazitambulika anakunyang’anya eneo lako,’’alifafanua
mwananchi Asha Ali Khamis.
Nae Saada Haroun Ali, alisema kama serikali haikuwalegeza
masharti ya usajili wa ardhi, wananchi wengi ambao ni wanyonge, watazikosa
ardhi zao.
Mwisho


Comments
Post a Comment