MJANE AIPA TANO ‘CHAPO’ KUMPA MTAJI


 NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

MJANE wa watoto watatu mkaazi wa shehia ya Uwandani wilaya ya Chake chake, ameishukuru Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilayani humo ‘CHAPO, kumuwezesha kwa mtaji wa shilingi 70,000 na kuanza biashara.

Alisema hakutarajia kua, ombi lake la shilingi 70,000 kwa uongozi wa ‘CHAPO’ lingejibiwa kwa haraka, ambalo alitamani kuanzisha biashara ya uji na mandazi, akiamini ndio itakayomsadia kimaisha.

Mama huyo aliyasema hayo, jana wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, kufuatia kutekelezewa ombi lake kwa CHAPO alilolitoa Juni 25, mwaka huu kwenye shamra shamra ya wiki ya msaada wa kisheria.

Alisema, tokea akabidhiwe mtaji wa shilingi 70,000 Juni 27, sasa anaendelea vizuri na kujipatia faida, kati ya shilingi 3,500 hadi shilingi 4,000 kwa biashara ya uji na mandazi kwa siku.

‘’Kwa hali yangu ya kipato, mimi nikipata shilingi 4,000 huwa shilingi 2,000 nazihifadhi na hadi sasa nimeshatimiza shilingi 32,000 kama faida, sio jambo dogo kwangu,’’alifafanua.

Aidha mama huyo mwenye watoto watatu, aliyeachika mwaka mmoja uliopita, akidai kutekelezwa kihuduma na aliyekua muumewake, alisema sasa anafikiria kuongeza biashara nyingine.

‘’Nimeshawishika kununua nazi mjini na kuja kuuza hapa nyumbani Uwandani, maana biashara ya uji na maandazi imeshanikubali,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, mama huyo alisema kama wanaume wataendelea kuyaacha majukumu yao, wanawake na watoto wataendelea kudhalilika.

‘’Mimi huyu aliyekuwa muume wangu, hadi sasa ni mwaka simjui alipo na wala kwa njia ya simu hapatikani, lakini sitoisahau ‘CHAPO’ kwa msaada wa mtaji na sasa nashukuru,’’alieleza.

Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema walipokuwa Uwandani kwenye mkutano wa wiki ya msaada ya kisheria, waliibuka wanawake kadhaa, wakilalamika ukosefu wa huduma kwa waliokuwa, waume zao.



‘’Wengi wao walitaka msaada na ushauri wa kisheria, lakini mmoja, alitupa mpango wake kazi, na tukamsaidia shilingi 70,000 na sasa anaendelea vizuri,’’alisema.

Hata hivyo alisema waliokwishawapa msaada unaofanana na huo, wapo wengi katika wilaya ya Chake chake, kwani ndio jukumu lao la msingi.

‘’Moja ya jukumu letu la msingi ni kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria tena bila ya malipo, ndio maana huwataka wananchi tunapokuwa na mikutano, wahudhurie,’’alifafanua.

Akizungumza kwenye kikao cha tathmini hivi karibuni, Mkuu wa divisheni ya Katiba na Msaada wa Kisheria Pemba Bakar Omar Ali, alisema mfano kama huo ni miongoni mwa mrejesho mzuri kwa jamii.

Alieleza kuwa, mikutano inayowafikia wananchi moja kwa moja, mara zote huzaa matunda, maana watu wamezungumkwa na changamoto na hawajui nani wamfikishie.

Wiki ya msaada wa kisheria kwa Pemba, ilianza Juni 25 hadi Juni 27, na kisha kuadhamishwa kwa kilele kilichofanyika Unguja Juni 28 na kuhutubiwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla.

                                Mwisho  

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’