JUMUIYA ZA WASAIDIZI WA SHERIA PEMBA: 'WIKI YA MSAADA YA KISHERIA ILICHAPUZA KAZI ZETU'

 

 
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WAKURUGENZI wa Jumuiya za wasaidizi wa sheria kisiwani Pemba, wamesema wiki ya msaada wa kisheria iliyomalizika mwezi uliopita kisiwani Unguja, ilichapuza utendaji wao wa kazi, kwa jamii.

Wakizungumza kwenye kikao cha tathmini kilichofanyika leo Julai 5, 2024 ukumbi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Chake chake, walisema waliongeza hamasa ya kutoa elimu kwa jamii.

Walieleza kuwa, ijapokuwa hilo ni jukumu lao la msingi, lakini kuanzia Juni 25 hadi 27, mwaka huu, waliwafikia wananchi wengi zaidi, kuliko ilivyozoeleka.




Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria Micheweni ‘MIDIPAO’ Saleh Hamad alisema kwa kushirikiana na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, walilifikia kundi la walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini, Micheweni.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani ‘MDIPAO’ Nassor Hakim Haji, alisema walipanga kuwafikia wandesha boda boda 65, ingawa walivuuka lengo hilo.




‘’Kwa mfano, sisi tulitarajia kukutana na waendesha boda boda 65, lakini kwa nguvu ya Idara, kwa kushirikiana na wadau wengine tuliwafikia 113, jambo ambalo lilikuwa kubwa,’’alieleza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake CHAPO, Nassor Bilali Ali, alisema hata wao walifikia wananchi 378 wa Uwandani, kuwapa elimu.




‘’Tulichagua wale waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini, na kwa hakika kwenye mkutano huo tulivuuka malengo yetu,’’alifafanua.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria Wete WEPO, Hemed Ali Hemed, alisema pamoja na changamoto ya bajeti, lakini wanafunzi wa vyuo vikuu walifikiwa kwa wingi wa aina yake.




Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa shughuli za wiki ya msaada wa kisheria, Mkuu wa Divisheni ya Katiba na Msaada wa Kisheria Pemba Bakar Omar Ali, alisema mafanikio makubwa yamefikiwa.

‘’Moja ni kufanikisha wiki ya tano ya msaada wa kisheria, kupatikana kwa bajaji kwa Jumuiya saba za wasaidizi wa sheria, pamoja na kuongeza idadi ya wasaidizi wa sheria wapya,’’alifafanua.



Aidha alieleza kuwa, jingine ni kufikiwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu 805 kwa Unguja na Pemba pamoja na waendesha boda boda 508, ambao baadhi yao wamefikiwa kwa ushirikiano baina yao na Jumuiya za wasaidizi wa sheria.

Akizungumzia changamoto za wiki ya tano ya msaada wa kisheria, alisema ni pamoja na ufinyu wa bajeti, uliosababisha uhaba wa washiriki kwenye kilele cha maadhimisho hayo kutoka kisiwani Pemba.

Hata hivyo, amewakumbusha wasaidizi wa sheria kuwatumia waandishi wa habari, wakati wanapotekeleza majukumu yao, ili na wengine waelewa wanachokifanya.

‘’Kama mkishindwa kuwatumia waandishi, basi hata mpige picha mziweke kwenye mitandao ya kijamii, ili watu wengine wajue, kwanza uwepo wenu pili kazi mnazozifanya,’’alifafanua.

Baadhi ya washiriki wakitoa maoni yao, akiwemo Safia Saleh Sultan, alisema kazi zinayofanywa na wasaidizi wa sheria ni kubwa, hivyo waendelee nazo kwa maslahi ya jamii yao.




‘’Msingi mkubwa wa kazi zenu ni wa kujitolea, sasa msivunjike moyo, maana jamii inawategemea mno katika kufanikisha hilo, mkirudi nyuma mmewapoteza,’’alieleza.

Wiki ya tano ya msaada wa kisheria Zanzibar, ilizinduliwa Juni 24, 2024 na Waziri wa Nchi Afisi, Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman na kilele kufanyika Juni 28 mwaka huu na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, alikuwa mgeni rasmi, katika ukumbi wa Idrissa Abdull Wakil na ujumbe wa mwaka huu, ulikuwa ni ‘tumia teknologia kurahisisha upatikanaji wa haki’’.

                                Mwisho

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’