CHAPO: 'WATUMIENI WASAIDIZI WA SHERIA WALIOMO SHEHIANI MWENU'
MARYAM SALUM, PEMBA@@@@.
WANANCHI wa shehia ya Mgogoni wilaya ya Chake Chake, wametakiwa kuvitumia vyombo vya sheria vilivyomo ndani ya shehia zao, wakiwemo wasaidizi wa sheria, ili kueleza changamoto zinazowakabili za kisheria kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi.
Kauli hiyo ilitolewa jana Julai 14, 2024 na Msaidizi wa sheria wa shehia hiyo Fatma Hilali Salim, wakati akizungumza na wananchi hao katika skuli ya maandalizi Ditia shehiani humo, ikiwa ni muendelezo ya mikutano ya wazi inayoendeshwa na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake Chake Pemba 'CHAPO'.
Alisema kuwa sasa hivi jamii, imekuwa ikikabiliwa na matatizo mengi yakiwemo ya udhalilishaji pamoja na migogoro ya ardhi, jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa jamii.
Alieleza kuwa, kutokana na changamoto hizo na nyengine kama hizo, kuna haja jamii kutumia vyombo vya sheria vilivyomo kwenye shehia zao, akiwemo sheha na wasaidizi wa sheria kueleza kero zao, ili kupatiwa ufumbuzi wa kisheria na si kwa njia vyengine, kama wanavyofanya baadhi ya watu.
"Kwenye jamii zetu yapo matatizo mbali mbali, ambayo yanapelekea familia kwa familia kutoelewana kwa namna moja ama nyengine, sambamba na vitendo vya uhalifu na migogoro ya ardhi, hivyo mkivitumia vyombo vya kisheria akiwemo sheha,wasaidizi wa sheria ambao sasa hivi wapo kila shehia kwa msaada wa kisheria, mtapunguza changamoto hizo,''alifafanua.
Alisema kuwa bado ndani ya jamii, zipo familia zina migogoro ya masuala mbali mbali hasa ardhi na hazijapatiwa ufumbuzi wowote, lakini wanashindwa kueleza changamoto hizo katika vyombo vya sheria, kwa sababu wanazozijua, jambo ambalo linazidi kupelekea kuongezeka kwa migogoro isiyoyalzima siku hadi siku.
"Migogoro mengine katika jamii, inaweza kupatiwa ufumbuzi na wasaidizi wakisheria, ambao wapo kila shehia bila ya kufikishwa Polisi au Mahakamani, lakini kutokana na baadhi ya jamii kutokuamini kwamba sisi wasaidizi wa sheria tunaweza, wanahiari kesi zao wapeleke Polisi moja kwa moja, jambo ambalo linazidi kutia gharama Serikali,''alifafanua.
Alifahamisha kuwa, wasaidizi wa sheria waliomo katika shehia wapo kisheria na wanatambulika Serikalini, na lengo la kuteuliwa kwenye nafasi hizo, ni kusaidia jamii kusikiliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi bila ya malipo kwa hatua za awali, kwa zile kesi amabazo zinastahiki kutatuliwa bila kufikishwa polisi ama mahakamani.
Aidha Msaidizi huyo wa sheria, aliitaka jamii kuelewe kwamba, Msaidizi wa sheria ama mwanasheria aliepo kwenye shehia wanaomsaada mkubwa wa kutatua changamoto za kijamii kwa hatua ya kwanza.
Mapema sheha wa shehia hiyo Suleiman Nassor Suleiman wakati akifungua mkutano huo, aliwataka wananchi wake kuwaamini wasaidizi wa sheria waliomo kwenye shehia yao, kwa kueleza changamoto zinazowakabili kwa msaada zaidi wa kisheria na sio kutafuta njia nyengine, wanazozijua ambazo hazipo kisheria.
Kwa upande wao wananchi hao, walieleza kuwa kwa vile wameshafahamishwa juu ya uwepo wa wasaidizi hao wa sheria, watahakikisha wanatoa ushirikiano kati yao na vyombo hivyo, ili kesi zao ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa hatua ya kwanza kisheria.
"Kwakweli wapo wanaofahamu kwamba kwenye shehia kuna wasaidizi wa sheria, wa masuala mbali mbali ya kijamii, lakni wapo, hawajui na hawajawahi kusikia, hivyo kwa vile tayari mumekuja kutuelimisha tutalifanyia kazi, kwani zipo kesi hazistahiki kupelekwa Polisi moja kwa moja,"walieleza.
Hata hivyo wananchi hao waliomba jumuia hiyo kuhakikisha angalau kwa mwezi wanafika kwenye shehia hiyo mara mbili, kwa ajili ya kuwapatia taaluma zaidi, kwani wapo watu wengine wanagombana tu kikawaida basi hukimbilia kupelekana Polisi, ingawa kumbe kuna uwezekano wa kukutana nai na ufumbuzi kupatikana.
Huu ni mkutano wa kwanza kwa mwezi huu kufanywa na wasaidizi wa sheria kutoka CHAPO kwa shehia hiyo, ingawa kwa mizi mitatu iliyopita kushawahi fanyika mkutano kama huo katika kijiji cha kwa sheha wa zamani shehiani humo.
MWISHO.





Comments
Post a Comment