BONANZA: WATOTO YARIPOTINI MAJANGA MNAYOFANYIWA

 


NA HASINA KHAMIS, OUT- PEMBA@@@@

MKURUGENZI Mtendaji wa Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba ‘TUJIPE’ Tatu Abdalla Msellem, amesema watoto wana haki ya kulindwa na kulijinda wenyewe, kutokana na majanga mbali mbali, yakiwemo ya udhalilishaji kwa kuyaripoti kwa wazazi na Serikali pale awapofanyiwa vitendo hivyo.

 

Alisema, kulingana na mazingira ya sasa baadhi ya wazazi wamekuwa mbali na watoto wao, na ndio chanzo cha udhalilishaji na ukatili wanaofanyiwa watoto hao.

 

Aliyasema hayo jana Julai 21, 2024 katika bonanza la Mabaranza ya watoto lililofanyika skuli ya Istikama Mkanjuni wilaya ya Chake Chake, lilioandaliwa kwa ushirikiano na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’.

 


Aidha aliwataka kujilinda, kusimamia na kujitetea katika suala la udhalilishaji na mazingira yao wanayoishi, ili kuepukana na vitendo hivyo.

 

"Kumekuwa na mtindo wa watoto kudhalilishana, hivyo ninawaomba kuacha mara moja kufanya vitendo hivyo, na ikitokezea, karipotini kwa waratibu wa mabaranza pamoja na wazazi wenu,"aliwashauri.

 

Aidha Mkurugenzi huyo wa TUJIPE, alisema uwepo wa waratibu katika mabaranza ya watoto, wanasaidia kupunguza woga na hofu kwa wahanga wa vitendo hivyo.

 


Alisema mabaraza hayo yanasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili watoto na familia, kwani bado baadhi ya watoto hawako salama, kwenye familia zao.

 

Nae Afisa Mradi Jumuishi kutoka Taasisi ya Save the Children, Maftah John Yohaness, alisema ni vyema kuwashirikisha watoto wenye mahitaji  maalum, katika masuala yote ya kijamii na kielimu.

 

‘’Watoto wenyemahitaji maalum, wana haki sawa kama wingine, hivyo kuwapenda, kuwashirikisha, kuwajali na kuwalinda ni jukumu letu sote,"alifafanua.

 

Aidha aliwakumbusha watoto hao, kuwa wazalendo wa taifa lao, kwa kuweka maslahi mbele ya taifa lao, wakijua kuwa wanao wajibu huo, ili baadae wawe viongozi wema.

 


Akisoma risala ya baranza la watoto wa mkoa wa kusini, Katibu mkuu wa Baraza hilo, shehia ya Msingini, Yunus Ali Mussa, aliwataka wazazi, walezi, wadau, serikali na jamii, kuwapatia haki ya elimu ya msingi, kwa kuwaandikishwa watoto wote wenye sifa.

 

Alieleza kuwa, wapo watoto hasa wenye mahitaji maalum, wamekuwa wakifungiwa ndani na kukoseshwa haki yao ya msingi, jambo linaloongeza ufinyu wa ufahamu wao.

 

‘’Sisi tunazochangamoto nyingi za kiafya, zinazosababisha maendeleo duni ya ukuaji wetu na kusababisha vifo, hivyo tunaomba wazazi kutekeleza majukumu yao ya msingi kwetu, ili tupate afya njema,’’alieleza.

 

Hata hivyo, aliishukuru wizara ya Afya Zanzibar, kwa kuendelea kuwapatia kinga za maradhi mbali mbali ikiwemo kichocho, minyoo pamoja na saratani ya shingo ya kizazi.

 


Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, katika hutuba yake iliyosmwa na Mratibu wa ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Ali, aliwaasa watoto kuachana na tamaa za kifedha na mali, ikiwa ni njia sahihi ya kushawishika kuingia katika mitengo ya watu waovu hasa wabakaji.

 

Hata hivyo Mkurugenzi huyo, alisema wataendelea kukutana na mabaraza ya watoto katika shehiz zote, 32 za wilaya ya Chake chake, ili kuwaelimisha na majanga yaliopo.

 


Katika hatua nyingine, aliwasisitiza wazazi na walezi, kuacha utamaduni wa kuzisuluhisha kesi za jinai zikiwemo za udhalilishaji, kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria.

 

‘’Kwanza tujilinde na udhalilishaji, lakini tunapoona kuna viashiria tunao wasaidizi wa sheria kwenye shehia zetu, tuwatumieni ili kupata elimu, msaada na ushauri wa kisheria bila ya malipo,’’alisisitiza.

 

Bonanza hilo, linalofanyika kila mwaka, limetayarishwa kwa pamoja kati ya Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto kwa kushirikisna na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba CHAPO.

 

Ambapo, kauli mbiu ya mwaka huu 'Mlinde, Mpende na Mshirikishe Mtoto kwa Maendeleo ya Taifa.’

 

            MWISHO 

 

 

 

 


Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’