KILELE WIKI YA MSAADA WA KISHERIA: MAKAMU WA PILI AAGIZA JUMUIYA ZA WASAIDIZI WA SHERIA ZIPATIWE OFISI

 



NA HAJI NASSOR, UNGUJA@@@@

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdull, amesema nia yake ni kuona jumuiya zote za wasaidizi wa sheria, zinakuwa na ofisi ambazo hazitolipa kodi, kwani msingi wa kazi zao, ni wa kujitolea.

Makamu huyo wa Pili, aliyasema hayo leo Juni 28, 2024 kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria, kilichofanyika ukumbi wa Idrisaa Abdull-wakil mjini Unguja.

Alisema, kama hatua zimeshachukuliwa kwa jumuiya za wasaidizi wa sheria wilaya ya Kusini na Kaskazini ‘A’ kuwa ofisi na jumuiya nyingine tisa zilizobaki, lazima hilo lifanyike.

Alieleza kuwa, kwa vile msingi mkuu wa wasaidizi wa sheria ni wa kujitolea, hakuna budi kwa serikali, kuhakikisha inajitolea na kuwapatia ofisi, ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.

‘’Nitawatuma wasaidizi wangu, kukutana na uongozi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, ili kukaa pamoja na kuona kila wilaya, imetoa jengo kwa ajili ya ofisi za wasaidizi wa sheria,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Makamu huyo wa Pili wa rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, alieleza kuwa, watoaji wa msaada wa kisheria wamekuwa wakombozi kwa jamii ya Zanzibar, na kuhakikisha wanapata haki zao.

Alifahamisha kuwa, Katika kufanikisha hilo, kuanzia kipindi cha mwaka 2020 hadi mwaka 2023, watoaji hao wa msaada wa kisheria, wamewafikia wananchi 419,401 ambapo kati yao 226,172 ni wanawake na 193,229 ni wanaume.

Alieleza kuwa, ndani yake wamo ambao waliokwishakata tamaa kupata haki zao na sasa wanaendelea kupata faraja, baada ya elimu, ushauri na kupata msaada wa kisheria.

Aidha Makamu huyo wa Pili, alifahamisha kuwa ni jambo la faraja kuona uratibu, usimamizi na uendeshaji wa masuala ya msaada wa kisheria hapa Zanzibar, yanaendeshwa katika ubora wa hali ya juu.

Wakati huo huo, Makamu huyo wa Pili wa Rais, akiabidhi bajaji saba, kwa ajili ya Jumuiya za wasaidizi wa sheria ikiwa ni ahadi ya Rais wa Zanzibar Dk. Husseinn Ali Mwinyi.





Aidha Makamu huyo wa Pili alizindua nambari ya simu ya bure 800710230 kwa ajili ya wataka huduma za kisheria, ambapo nambari hiyo hapo baadae, itawekewa kifaa maalum kitakachoruhusu kuweza kutumiwa na watu 15 kwa wakati mmoja

Mapema Waziri wa Nchi Afisi, Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Haroun Ali Suleiman, aliiagiza Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, kuangalia katika bajeti yake ijayo, kupatiwa sabuni kwa wasaidizi wa sheria.



Alieleza kuwa, wamekuwa wakifanyakazi kubwa ya kuwasaidia wananchi kwa njia ya kujitolea, hivyo ni vyema kwa sasa kuangaliwa, ili kupata sabuni kwa lengo la kuwapa hamasa na kujenga ari kwao.

‘’Kwa vile wasaidizi wa sheria, wamekuwa wakifanyakazi kubwa, natoa agizo kwa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, katika bajeti ijayo, kufikiria mara mbili jambo hilo,’’alifafanua.

Aidha Waziri Haroun, aliwashauri washirika wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria wakimo LSF, UNDP na wengine kuangalia uwezekano wa kusaidia, jambo hilo.

Mkurugenzi Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, alisema kabla ya kilele cha maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria, shughuli kadhaa ikiwemo makongamano ya vyuo vikuu, yalifanyika.

‘’Kwa shughuli zilizofanywa na Idara yetu pekee, wananchi 816, walifikiwa na elimu ya kisheria, ambapo kwa waliofikiwa na watoaji wa msaada wa kisheria kwa Unguja na Pemba ni wananchi 1,690,’’alieleza.



Aidha Mkurugenzi huyo, alisema ushirikiano uliopo kwa taasisi kama za skuli ya sheria, ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka, Jeshi la Polisi, Chuo cha mafunzo, Mahkama na wasaidizi wa sheria, wamekuwa wakifanikisha malengo yao.

‘’Hata hivyo kipekee, niwapongeze wenzetu wa LSF na UNDP kwa kuendelea kutushika mkono, katika mradi wa upatikanaji haki Zanzibar, jambo ambalo linawapa faraja watu wasio kuwa na uwezo,’’alieleza.

Akiwasilisha salam za LSF, Meneja Mawasiliano na Ushirikiano wa tasisi hiyo Jane Matinde, alisema kwa muda wa miaka mitano sasa, wamekuwa wakisaidia kufanyika kwa wiki ya msaada wa kisheria.

Aidha Meneja huyo, alisema kwa Tanzania bara na Zanzibar, wastani wa wananchi milioni 10, wameshafikiwa na elimu ya msaada wa kisheria kwa mwaka jana pekee.

Alifafanua kuwa, hilo linasaidia kupunguza kesi mahkamani na kupunguza migogoro ndani ya jamii, jambo ambalo linaimarisha utawala bora na utawala wa sheria.

‘’Hadi sasa tunaendelea kuyasaidia mashirika 184 Tanzania nzima, ambapo wanawafikia wananchi kuwapa elimu bure, na wastani wa mashauri 100,000 na asilimia 70 hutatuliwa na wasaidizi wa sheria,’’alifafanua.   








Wakitoa salamu zilizosomwa na Time Asaa Khamis, wasaidizi wa sheria Zanzibar, walimpongeza Waziri Haroun, kwa kufuta ada ya usajili ya shilingi 20,000 kwa wasaidizi wa sheria.

Aidha, alisema wamefarajika kuona, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  kutimiza ahadi yake ya kuwapatia bajaji.

Alieleza kuwa, kati ya bajaji zilizoombwa za jumuia za wasaidizi wa sheria 11 kwa Unguja na Pemba, tayari bajaji saba zimeshapatikana na kuamini kuwa kwa wilaya nyingine zitapatiwa hapo baadae.

Katika hafla hiyo, wasaidizi wa sheria kadhaa walikabidhiwa tunzo kwa utendaji wao bora pamoja na jumuiya bora ya wasaidizi wa sheria kwa mwaka huu.

Waliopata tunzo hizo ni Nassor Bilali Ali kutoka Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake CHAPO, kuwa masaidizi wa sheria bora wa mwaka.

Wengine ni Mwaka Mzee Mohamed, aliyeibuka msaidizi wa sheria bora kwa Unguja, katika haki za binaadamu ni masaidizi washeria kutoka Mkoani ‘MDIPAO’ Massoud Abdalla Massoud.

Aidha Omar Abdalla Nassor, alipata tunzo ya mazingira kutoka Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Wete ‘WEPO’ Nassor Bilali Ali, alipata tena kwa upande wa kupinga ukatili na udhalilishaji, wakati jumuiya bora ya wasaidizi wa sherua ni ya Magharibi ‘A’

Wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar ilizinduliwa Juni 24, 2024 na Waziri wa Nchi Afisi, Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Haroun Ali Suleiman.

Hii ni wiki ya tano wa Msaada wa Kisheria Zanzibar, ambapo ujumbe wa mwaka huu ni ‘tumia teknologia kurahisisha upatikanaji wa haki.

                                Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’