ZIARA YA ‘CHAPO’ YAFUFUA BARAZA LA WATOTO CHANJAANI

 

 NA MWANDISHI MAALUM, PEMBA@@@@

UONGOZI wa shehia ya Chanjaani wilaya ya Chake chake Pemba, umesema ujio wa wasaidizi wa sheria kutoka Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilayani humo, umewasaidia kutambua dhana ya baraza la watoto kisheria, kinyume na hapo awali.

 

Hayo yameelezwa juzi na Sheha wa Chanjaani Khatib Ali Vuai, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, baada ya kumalizika kwa kikao, kilichojumuisha wasaidizi wa sheria, wajumbe wa sheha na askari shehia na kufanyika Chanjaani Gereji.

 

Alisema, hapo awali hakuwa na uwelewa mpana, wa nini maana ya baraza la watoto, utataratibu wake, aina ya wajumbe, idadi, kazi zao, utambuzi wake kisheria, ingawa ujio wa wasaidizi wa sheria umemfungua macho.

 

Alieleza kuwa, alikuwa anasikia tu ndani ya shehia yake, kuwa kuna baraza la watoto, ingawa alidhani ni suala lisilotambuliwa kisheria, na hakuwa na hamu ya kulifuatilia kwa undani.



 

Alifahamisha kuwa, kikao hicho cha wasaidizi wa sheria kutoka ‘CHAPO’, kimempa mwanga mpana, na sasa amepanga kukutana na Mratibu wa baraza hilo na wajumbe wake, ili kujitambulisha rasmi.

 

‘’Ziara yenu wasaidizi wa sheria, imenisaidia mno mimi sheha na wajumbe wangu, juu ya dhana ya kisheria ya uwepo wa baraza hili, na sasa tunatamani kukutana na Mratibu na wajumbe wake, ili kulifahamu kwa upana,’’alisema.

 

Katika hatua nyingine sheha huyo, aliupongeza uongozi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ kwa kuandaa ziara hiyo, ambayo imewasaidia mambo kadhaa.

 

‘’Nimefurahishwa niliposikia kuwa, kupitia mabaraza hayo, sheria inakubali kwa watoto wenyewe, kuanzisha klabu kama za mazingira, kupinga udhalilishaji na ile ya maadili,’’alieleza.

 

Nae mjumbe wa sheha eneo la Vijijini Khadija Said Abdall, alisema ndio kwanza anasikia kutoka kwa wasaidizi hao wa sheria, kuwa kuna baraza la watoto, katika kila shehia za Unguja na Pemba.

         



     

Alisema, awali hakuwa na taarifa sahihi juu ya uwepo wa baraza hilo, hasa kwa vile katika kijiji anachokiongoza, hakuna mwanachama wala mjumbe.

 

‘’Kama lipo baraza la watoto hapa shehia ya Chanjaani, basi ni kwa baadhi ya watoto na kwenye baadhi ya vijiji, maana mimi ni mjumbe wa shehia, lakini sina taarifa, mpaka mlipokuja kutueleza.’’alifafanua.

 

Nae mjumbe wa sheha Rehema Juma Faki, alisema ziara hiyo ya wasaidizi wa sheria, imeamsha uwelewa kwao na sheha wao kwa ujumla, na kinachofuata, sasa ni kulifufua baraza hilo.

 

‘’Kwa Zaira yenu hii, inatubidi sasa tumfuatilie Mratibu wa baraza la watoto la shehia yetu, na kama baraza liko hai ni kuliendeleza na kama limefifia ni kulifufua,’’alisema.

 

Mapema Msaidizi wa sheria shehi ya Chanjaani Wahida Kombo Khamis, alisema nia ya ziara yao hiyo, ni kutaka uwelewa kwa sheha na wajumbe wake, juu ya uwepo wa baraza hilo.

 

Alisema, kisha Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’, ni kutaka kuanzisha klabu ya kupinga udhalilishaji ndani ya baraza hilo.

 

Alieleza kuwa, maana watoto wamekuwa ndio waathirika wakubwa katika janga la ukatili na udhalilishaji, sasa kupitia chombo chao cha baraza, wanalengo la kuanzisha klabu hiyo.

 

‘’Zipo shehia kama za Msingini, Wawi, Wesha mabaraza ya watoto yanafanyakazi vizuri, sasa lengo la ziara hii, ni kutaka kulifufua au kuliendeleza baraza la watoto shehia ya Chanjaani,’’alisema.

 

Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, akizungumza na wasaidizi wa sheria hivi kaibuni, alisema wameanza mpango madhubuti wa kuhakikisha kila shehia, inakuwa na klabu ya kupinga ukatili na udhalilishaji.

 

Alieleza kuwa, awali walikuwa na mpango wa kuzifikia shehia tano za Msingini, Kibokoni, Ng’ambwa, Matale na Wesha, ingawa sasa mpango ni shehia zote 32 za wilaya ya Chake chake.

 

‘’Tunachoamini, kila shehia inalo baraza la watoto, lakini tukibaini kuna shehia linalega lega, kwanza nikulifufua na kulisimamia na kisha kuanzisha klabu ya kupinga ukatili na udhalilishaji ndani yake,’’alisema.

 

Msaidizi wa sheria jimbo la Chake chake Riziki Hamad Ali, alisema klabu hizo ambazo zitawezeshwa kielimu na mbinu hapo baadae, ili kutambua viashiria vya ukatili na udhalilishaji.

 

Alieleza kuwa, kwa vile wasaidizi wa sheria ni wadau wa haki za binaadamu, ndio maana wameamua kuanzisha vilabu hivyo, na kisha kuvisimamia.

 

‘’Kama tunataka viongozi wazuri wa baadae, au wasaidizi wa sheria, wakuu wa wilaya na mikoa waliosalama, lazima tuchukue hatua sasa za kuwalinda watoto wetu,’’alieleza.

 

Msaidizi wa sheria shehia ya Wawi Haji Nassor Mohamed, alisema tayari kwa upande wa shehia yake, ameshakutana na uongozi wa baraza la watoto, na kutambua changamoto zao.

 

‘’Inaonekana haya mabaraza yanafanyakazi kwa uwepo wa miradi tu, bila ya kujali kuwa, suala la kutoa elimu na kusikiliza changamoto za watoto ni kazi ya kila siku,’’alisema.

 



Hata hivyo, amesema amepata moyo kuona uongozi wa shehia ya Chanjaani, kutaka kukutana na Mratibu wa baraza la watoto la shehia hiyo, kwa lengo la kutafuta namna ya kuliendeleza.

 

Tayari ziara hiyo ya wasaidizi wa sheria, imeshazitembelea na kufanya mikutano katika shehia za Wesha, Wawi, Chanjaani, Matale, Msingini, Ziwani kwa lengo la kuanzisha klabu za kupinga ukatili na udhalilishaji kwa watoto.

 

                            MWISHO

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’