WEPO, CHAPO: 'MKIFAUATA NJIA HIZI MIGOGORO YA ARDHI KWISHA KAZI'
NA MWANDISHI WETU, PEMBA@@@@
WANANCHI kisiwani Pemba, wametakiwa wasikurupuke wakati
wanapotaka kununua ardhi, na badala yake, wajiridhishe kwanza juu ya uhalali, wa
umiliki kwa muuzaji, ikiwa ni njia moja wapo ya kuepusha migogoro, isiyokuwa ya
lazima.
Hayo yameeleza leo Mei 21, 2024 na wasaidizi wa sheria kutoka
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Wete Pemba ‘WEPO’ na wenzao kutoka Jumuiya ya Wasaidizi wa
sheria Chake chake ‘CHAPO’, wakati wakitoa elimu ya sheria, juu ya njia za
kujiepusha na migogoro ya ardhi, kupitia kituo cha redio Istqaama kisiwani
Pemba.
Walisema, wapo wananchi wamekuwa wakikubali kuuziwa ardhi
kinyemela, pasi na mnunuzi kujiridhisha juu ya umiliki wa ardhi hiyo, kabla ya
kuanza mchakato huo.
Walieleza kuwa, ili kujiepusha na migogoro ya ardhi, hakuna budi
kwa mnunuzi, apate uthibitisho kutoka kwa muuzaji, kama vile nyaraka za matumizi
ya ardhi, urithi, huba, kuvunja pori ambapo nyaraka hizo zitakuwa ni sehemu ya
kielelezo kabla ya kununua.
Msaidizi wa sheria kutoka shehia ya Kangagani wilaya ya Wete, Hamad
Omar Mussoud, alisema kama ardhi inamilikiwa na watu zaidi ya mmoja, suala la
kupatikana kwa hati za wakala ni la msingi.
‘’Kama ukitaka kununua ardhi, lazima ujiridhishe, jee
inamilikiwa na mtu mmoja au zaidi, na kisha akukabidhi nyaraka zinazoonesha
uhalali kutoka kwa muuzaji, kabla ya kuanza kwa harakati za kunuanua,’’alifafanua.
Aidha Msaidizi huyo wa sheria, alisema katika ununuzi wa ardhi,
kisheria sheha wa shehia, hahusiki moja kwa moja kisheria, bali anahusika
wakati wa uhaulishaji wa ardhi utakapofika.
‘’Ingawa inashauriwa, moja ya vyanzo muhimu vya kujiridhisha kwa
mnunuzi, ni kuzungumza makundi mbali mbali kama vile sheha, watu maarufu, watu wenye
umri mkubwa na wanaopakana na ardhi husika,’’alishauri.
Katika hatua nyingine, amewataka wananchi kuhudhuria kwenye
mikutano yao ya wazi, wanayoiitishwa katika shehia mbali mbali, ili kuongeza
maarifa ya kisheria.
Kwa upande wake Msaidizi wa sheria kutoka shehia ya Kambini
wilayani humo, Tamim Ali Omar, alisema migogoro ya ardhi, husabishwa na vyanzo
kadhaa, ikiwemo uharaka wa wanunuzi.
‘’Mnunuzi anatoa fedha nyingi kununua ardhi, lakini kwanza haoni
umuhimu wa kuifanyia utafiti ardhi husika, na ndio maana baada ya muda mfupi, anazuka
mwingine akidai ni mali yake,’’alieleza.
Hata hivyo, amewataka wananchi wanapotaka kununua jambo lolote,
wasisite kuwashirikisha wasaidizi wa sheria, ili kupata ushauri na msaada wa
kisheria bila ya malipo.
Akizungumzia njia za umiliki wa ardhi, alisema ziko tano
kisheria, moja wapo ni kuvunja pori, ambalo ndani ya miaka 12, ikiwa
hajatokezea muhusika, unaweza kwenda serikalini, kuliomba eneo hilo, kwa lengo
la kukabidhiwa hati za matumizi.
Alieleza kuwa, njia nyingine ni kununua, kupewa zawadi, urithi, pamoja
na kupewa na serikali, kupitia wiziri husika wa ardhi, ambapo pia taratibu kisha
ni kupewa hati ya umiliki, baada ya kufanyika kwa uhaulishaji ‘land
transfer’.
Katika hatua nyingine, aliipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria
Zanzibar, kwa kuendelea kuwajengea uwezo kila wakati, jambo ambalo, huwapa ari na
uthubutu wa kufanyakazi.
Mapema Msaidizi wa sheria kutoka Jumuiya ya wasaidizi wa sheria
wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ Haji Nassor Mohamed, alisema kasoro kubwa iliyopo
ndani ya jamii, ni kudharau mikutano katika shehia zao.
Alieleza kuwa, wasaidizi wa sheria, wamekuwa na mikutano kila
siku katika shehia mbali mbali, wakitoa elimu ya sheria ya ardhi, mirathi,
udhalilishaji, dawa za kulevya lakini, shida ni wananchi kutohudhuria.
‘’Kwa mfano, kama wananchi wangekuwa wanahudhuria kwenye mikutano
yetu, hata migogoro ya radhi ingepunguwa, maana suala la matumizi
ya radhi, isiyo na migogoro hutolewa,’’alifafanua.
Baadhi ya wasikilizaji, wakitoa maoni yao, walisema mada
iliyowasilishwa ni nzuri, kutokana na kupata uwelewa juu ya njia za kujipepusha
na migogoro ya ardhi.
Mmoja wa wananchi hao, Ahmada Mbwana wa Wete, alisema ameelewa
njia ambazo kama mnunuzi wa ardhi akizifuata, anaweza kujiepusha na migogoro ya
ardhi.
‘’Ni kweli, wakati mwingine tunauziana ardhi kinyemela, bila ya
mnunzi kufanya uchunguuzi juu ya uhalali wa umiliki wa ardhi husika, kwa
muuzaji,’’alifafanua.
Nae Maryam Issa Khamis wa Pujini, alisema hakuwa anafahamu kuwa,
sheha sio sehemu ya kisheria moja kwa mioja, katika kuuza ama kununua ardhi,
bali sheria inamgusa zaidi yeye na Mkuu wa wilaya, wakati wa uhaulishaji.
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Wete Pemba ‘WEPO’
inaendelea kutoa elimu ya kisheria, ushauri na msaada wa kisheria katika shehia
zote 36, za wilaya hiyo kwa kuwatumia wasaidizi wa sheria 27, waliomo katika
shehia mbali mbali.
Mwisho






Comments
Post a Comment