CHAPO: YAWAPA MBINU WANAFUNZI WESHA KUKOMESHA UDHALILISHAJI
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANAFUNZI wa Almadrssatul Fatuhu-l-khair ya
kijiji cha Mchochani shehia ya Wesha, wilaya ya Chake chake Pemba, wametakiwa kuwaripoti
waalimu, wazazi, kaka, wajomba na watu wengine maarufu, ikiwa watawagundua wameanza mchezo wa kutaka kuwadhalilisha.
Ushauri huo umetolewa leo Mei 19, 2024 na wasaidizi wa sheria shehia ya Wara Sabahi Mohamed Abdalla
na mwenzake wa Wesha Khadija Said Khalfan, wakati wakitoa elimu ya kisheria,
kuhusu viashiria vya udhalilishaji kwa wanafunzi hao, kwenye mkutano wa wazi ulioandaliwa
na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’.
Walisema, wasijaribu
kuwaficha watu wa aina yoyote, ikiwa watawabaini wameanza tabia ambayo, sio ya
kawaida, kama vile kuwachezea sehemu zao za siri, hivyo wasisite kutoa taarifa.
Walieleza kuwa, katika
hilo waondowe woga na wasiwasi, kwani sheria zipo kwa ajili ya kuwalinda, hivyo
kama watahisi kuna mchezo wanachezewa, wasisite kutoa taarifa haraka.
Msaidizi wa sheria
shehia ya Wara Sabahi Mohamed Abdalla, alisema wakiendelea kuwaficha watu hao,
wanaweza kuwadhalilisha nyumba nzima, wakijua kuwa hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.
‘’Wanafunzi, mkihisi
kunadalili za kutaka kudhalilishwa, hata awe mwalimu au baba, tuweni taarifa
kwa mtu mwingine au kwa msaidizi wa sheria na sheha, ili hatua zichukuliwe,’’alieleza.
Nae Msaidizi wa sheria
shehia hiyo, Khadija Said Khalfan, amewakumbusha wazazi na walezi hao, kuwa
karibu na watoto, ili kuwagundua mapema, ikiwa wameanza ama laa, kufanyiwa vitendo
vya udhalilishaji.
‘’Njia moja nzuri ya
kumfuatilia mtoto, ni kujua marafiki zake, maeneo anayopenda kucheza, aina ya
michezo, muda wake wa kulala na kuamka, na hata suala la matumizi yake,’’alishauri.
Mapema Askari wa Jeshi
la Polisi kutoka wilya ya Chake chake anaefanyakazi shehia za Wesha, Ndagoni na
Michungwani Khamis Ali Khamis, aliwakumbusha wazazi na walezi, kuwaripoti
waingizaji, wasambaazaji na watumiaji wa dawa za kulevya, ili hatua
zichukuliwe.
Alieleza kuwa, kwa
miaka ya hivi karibuni, watu hao waovu huwatumia watoto katika kazi hiyo, kwa
kuwalaghai kwa fedha au zawadi, jambo ni hatari zaidi.
Aliongeza kuwa, sasa
ni wakati wa jamii kuwapiga vita watu wa aina hiyo, kwani madhara ya utumiaji
wa dawa za kulevya, haumuathiri mtu mmoja pekee, bali jamii kwa ujumla.
Akifungua mkutano huo,
Sheha wa shehia ya Wesha Haji Mohamed Ali, aliwataka wananchi hao, wasisite
kuwaripoti kwake au kwa Jeshi la Polisi, wahalifu mbali mbali.
‘’Sisi jamii tuungane,
kuukataa kwa vitendo uhalifu, ukiwemo udhalilishaji na dawa za kulevya, maana
athari ya haraka hutukumba sisi wakaazi wa eneo husika,’’alifafanua.
Mwalimu mkuu wa Almadrasatu Fatuhu-l- khaira ya kijiji cha Mchochani shehiani humo, sheikh Kassim Bakar Yussuf, aliutaka uongozi wa ‘CHAPO’ kuongeza juhudi zaidi za utoaji, elimu.
Wanafunzi
Asma Kassim Bakar na mwenzake Ibrahim Mohamed Rashid, walisema uamuzi wa ‘CHAPO’
kuwafuata kijijini kwao ni hatua nzuri, kwani wamepata kuuliza na kujibiwa maswali
yao.
Mzazi Aziza Omar Khamis, alisema ni vyema, ulinzi ukawepo kwa wananchi wanaotoa taarifa ya uwepo wa vitendo vya kihalifu, ili nao wapate ari na kasi ya kushirikiana na jeshi la Polisi.
Mkutano huu, ni muendelezo
wa mikutano ya wazi, inayofanywa cha ‘CHAPO’ kwa kushirikiana na masheha na
askari shehia, kwa lengo la kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria bila ya
malipo.
Mwisho
Comments
Post a Comment