CHAPO YAANZA MAANDALIZI WAWI UANZISHWAJIA KLABU YA KUPINGA UDHALILISHAJI BARAZA LA WATOTO

 

NA ASHA ABDALLA, PEMBA@@@@ 

           

JUMUIYA ya wasaidizi washeria wilaya ya Chake chake Pemba, ‘CHAPO’ imesema inampango wa kuanzisha klabu maalum ya kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji ndani ya baraza la watoto la shehia ya Wawi, kwa lengo la kulijengea uwezo, ili kutambua viashiria ya vitendo hivyo. 

 

 

Hayo yameelezwa wasaidizi washeria wa shehia za Wawi, Wesha, Waram Mgogoni na Kibikoni wilayani humo, wakati wakizungumza na wajumbe wa baraza hilo, kwenye mkutano maalum wa wazi, wenye lengo la kupanga mikakati ya kutokeza vitendo hivyo.

 


Walisema kuwa CHAPO, inalojukumu kubwa la kuhakikisha kila shehia ya wilaya ya Chake chake, imefikiwa na elimu inayostahiki katika kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa watoto, ikiwemo kuanzisha klabu hizo.

 

Mmoja kati ya wasaidizi wa sheria hao kutoka shehia ya Wesha, Khadija Said Khalfan, alisema kuwa, wasaidizi wa sheria kazi yao ya msingi ni kutoa elimu na msaada wa kisheria bure, ikiwemo kuyapitia makundi kama ya mabaraza ya watoto.

 



Alieleza kuwa, suala la uanzishwaji wa klabu ndani ya mabaraza ya watoto, itakuwa rahisi sasa kwa watoto hao, kupata jukwaa la kuelezea matendo wanayofanyiwa katika maisha yao.

 

‘’Chapo kupitia wasaidizi wa sheria, na kupitia mabaraza ya watoto tutaanzisha klabu maalum, zenye lengo la kupinga ukatili na udhalilishaji, na kisha watoto watajengewe uwezo wa kuzungumza na kuibua viashiria vya ukatili na udhalilishaji,’’alieleza.

 


Mapema Msaidizi wa sheria wa shehiya ya Wawi Haji Nassor Mohamed alisema kuwa, watoto wawe tayari kupinga udhalilishaji kwa njia moja ama nyingine, pale tu wanakapoona viashiria ambavyo watafanyiwa.

 

"Watoto mnatakiwa kuwa makini, wakati munapoona viashiria vya ukatili na udhalilishaji, ikiwemo kupewa zawadi ovyo ovyo, kuoneshwa picha chafu kwa simu, kuitwa vichochoroni au hata kuchezewa miili yenu na kila mtu,’’alifafanua. 

 



 

Hata hivyo aliwataka watoto hao, kuawa tayari kutoa taarifa, pale wanapofanyiwa udhalilishaji au kutoa ushahidi popote hata kama mtendaji huyo ni baba mzazi, kaka au kiongozi wowote kutoka katika taasisi au serikalini.

 

 

Katika hatua nyingine, aliwaomba watoto hao kua mabalozi kwa wenzao ambao hawakuhudhuria katika mkutano huo, kuwapa elimu, ili kujua mambo muhimu ambayo waweze kujitenga nayo.

 

Akizungumzia umuhimu wa kuanzishwa kwa klabu ya kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji, alisema vitakuwa ndio jukwaa kwa watoto hao la kupashana habari na kuelezana madhila wanayopitia.

 

 

Kwa upande wake Msaidizi wa sheria wa shehiya ya Wawi Fatma Hilali Salim, alisema kua watoto wanapodhalilishwa kwa njia yoyote ile, iwe ni kuadhibiwa, kulawitiwa, kubakwa, kupewa majina wasiyoyataka, wahakikishe hawakai kimnya.

 




 Nae Msaidizi wa sheria wa shehiya ya Kibokoni Haitham Hamad Khamis, aliwaomba watoto wasisite kutoa taarifa kwa wale ambao wanafanyiwa udhalilishaji, kwa kuhofia vitisho.

 



Wakizungumza kwenye mkutano huo, Mratibu wa wanawake na watoto ambae ni mratibu wa baraza la watoto shehia ya Wawi Fatama Kassim Mohamed na Mwenyekiti wa baraza hilo Abuubakar Masoud Juma, walipongeza hatua ya Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ kwa  kuonesha nia ya kupinga vitendo hivyo.

 

Walisema, mabaraza hayo yamekuwa wakati mwingine yakikosa msaada kama wa elimu, ingawa aanamini baada ya ujio wa wasaidizi wa sheria, sasa watoto watatambua haki na wajibu wao kwa jamii.

 



‘’Sisi hiyo klabu tunahamu nayo mno, maana hata watoto wa shehia ya Wawi, nao hawako salama na vitendo vya ukatili na udhalilishaji, njooni tusaidiane kuwalinda watoto wetu,’’alisema Mwenyekiti.

 

 CHAPO kwa sasa imo katika utekelezaji wa mradi wa upatikanaji haki, unaofadhiliwa na taasisi ya LSF, ambapo moja ya shughuli katika mradi huo, ni kuanzishwa klabu za kupinga udhalilishaji kupitia mabaraza ya watoto, katika shehia teule za Kibokoni, Wesha, Ng’ambwa, Matale na Msingini.

                      MWISHO

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’