'CHAPO' YAZINDUA VILABU VYA KUPINGA UDHALILISHAJI MABARAZA YA WATOTO
AFISA Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto wilaya ya Chake chake Salma Khamis Haji, amewataka
watoto wilayani humo, kutoa taarifa, pindi wanakapoona viashiria vya ukatili na
udalilishaji dhidi yao, ikiwemo kuanza kuchezewa sehemu zao za siri.
Hayo
ameyasema leo April 28, 2024, skuli ya Maandalizi Madungu, wakati akieleza wajibu wa mabaraza
hayo, kwenye mkutano wa uzinduzi wa vilabu vya kupinga ukatili na udhalilishaji
wa kijinsia, kupitia mradi wa upatikanaji haki, unaoendesha na Jumuiya ya
wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’.
Alisema moja
ya malengo ya vilabu hivyo, ni kuwawezesha watoto hao, kutetea mambo
yanayohusu, huku jambo la mwanzo likiwa ni kutokukaa kimnya wanapoona viashiria
vibaya kwao.
Alieleza kuwa, kiashiria kimoja wapo ambacho wanatakiwa kukiripoti ni kuanza kuchezewa sehemu za miili yao, kupewa zawadi na fedha zisizo na sababu maalum, pamoja na kuitwa maeneo yasio rasmi (vichakani).
Alieleza kuwa,
wapo watu ambayo wanatabia mbaya, na wanaweza kuwatengenezea mazingira ya
kuwaharibu, ikiwemo kuanza kuwapa fedha na kuwashika shika miili yao.
Alifafanua,
wakiona kuna mtu wa kando, au wa ndani ya familia na hata mwalimu wake, ameanza
na tabia hizo haraka sana watoe taarifa iwe kwa familia, mratibu wa wanawake na
watoto au mwalimu wao.
“Watoto
mkiona kuna mtu ameanza kukuita, kukupa fedha, zawadi anza kutoa taarifa
nyumbani au skuli, kwani wapo wengine huwa huo ndio mwanzo wa kutaka
kuwadhalilishaji,’’aliwatahadharisha.
Akizungumzia vilabu hivyo, Afisa huyo aliesema kuwa, jambo lililoibuliwa na ‘CHAPO’ ni jema, maana litawasaidia watoto hao kuwa na sehemu muhimu, ya kutoa malalamiko yao.
Alieleza kuwa,
wapo watoto wamekuwa wakikumbana na vitendo mbali mbali, lakini wakati mwingine
hawajui pa kukimbilia, ingawa anaamini vilabu hivyo vitakuwa sehemu sahihi
kwao.
Katika hatua
nyingine, Afisa huyo, alisema hivi karibuni wizara itayapitia upya mabaraza
yote ya watoto, ili kuyaendeleza upya, ikiwemo kufanya chaguzi, baada ya
wajumbe wa awali, wengi wao, kupindukia umri wa utoto.
Akifungua
mkutano huo, Mkurugenzi wa CHAPO, Nassor Bilali Ali alisema ‘CHAPO’ imeamua
kuanzisha vilabu vya kupinga ukatili na udhalilishaji, kupitia mabaraza hayo, kwani
watoto ndio waathirika wakubwa.
Alieleza
kuwa, ili kuhakikisha vilabu hivyo vinakuwa endelevu, kila msaidizi wa sheria
hapo baadae, atakuwa ndio msimamizi mkuu wa vilabu hivyo.
‘’Wasaidizi
hawa wa sheria pamoja na majukumu yao ya kila siku, lakini watakwenda
kuwajengea uwezo wa kielimu watoto hao, ili wazidi kujitambua kwa lengo la kuibua
chamgamoto zinazowakabili,’’alifafanua.
Akitoa mada
ya njia za kujikinga na vitendo vya ukatili na udhalilishaji, Mratibu kutoka ‘CHAPO’,
Mohamed Hassan Abdalla, alisema moja wapo ni kwa watoto hao, kufuatana kwa
makundi wanapokwenda na kurudi masomoni.
Njia
nyingine alisema, ni kwa wazazi na walezi, kukubali kuleleana watoto, ili kila
mmoja awe na nguvu ya kuripoti matendo atakayoyaona ya mtoto wa jirani yake.
Wakizungumza
kwenye mkutano huo, watoto hao wamesema kupitia vilabu hivyo, watapata jukwaa
sahihi la kuelezea kero na changamoto wanazopitia katika maisha yao.
Mwenyekiti wa
baraza la watoto shehia ya Msingini Said Hassan Khamis, aliwashauri wazazi na
walezi, kupunguza matumizi ya nguvu kwa watoto wanapowaadabisha, kwani kufanya
hivyo kunaweza kukasababisha ukatili.
‘’Lakini pia
niwashauri wazazi na walezi wasiwe wakali kupindukia pale wanapotaka taarifa
kutoka kwa watoto, kwani wengine wanaweza wasitowe ushirikiano na kukosekana
kwa taarifa sahihi,’’alifafanua.
Msaidizi wa sheria
Jimbo la Chake chake Riziki Hamad Ali, amewasihi watoto hao, kuhakikisha
wanakaa na wenzao wasiopata elimu hiyo, ili kuwaelekeza.
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake
chake Pemba ‘CHAPO’ katika utekelezaji wa mradi huo wa upatikanaji haki,
unaofadhiliwa na taasisi ya ‘LSF’ unafanyakazi katika shehia tano za Wesha, Ng’ambwa,
Kibokoni, Msingi na Matale.
mwisho
Comments
Post a Comment