ALIYEUPASUA MPIRA WA WATOTO WESHA ULIOTOLEWA NA CHAPO AAHIDI KUULIPA

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@


MWANAMKASI Mikidadi Maeda (38) wa shehia ya Wesha wilaya ya Chake chake, amekubali ushauri wa wasaidizi wa sheria wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilayani humo, ‘CHAPO’ kulipa gharama za mpira mmoja wa miguu, alioupasua baada ya kumgonga kwa bahati mbaya, wakati timu ya ‘kaza buti’ inyomilikiwa na baraza la watoto la shehia hiyo, walipokuwa wakifanya mazoezi.

Mpira huo awali, ulikabidhiwa kwa uongozi wa baraza hilo ukitoka CHAPO, Machi 20, mwaka huu, kwa ajili ya timu hiyo, ikiwa ni ahadi ya wasaidizi wa sheria, walioitoa kwa watoto hao, mwishoni mwa mwaka jana.

Kwenye kikao cha sulhu kilichofanyika nyumbani kwa sheha wa shehia ya Wesha, mwananchi huyo alikiri kosa la kujichukulia sheria mikononi, mara baada ya tukio hilo la yeye kugongwa mpira wa uso.

Alisema siku ya tukio hilo, alikuwa nyumbani kwake, kando kando ya uwanja huo, wakati akiwa kwenye harakati zake, alishtukia mpira ukienda usoni mwake, na kumsababisha maumivu, jambo ambalo lilimsababishia kujawa na hasira.

‘’Baada ya kunipiga mpira, wachezaji wengine walinizomea na mimi kutokana na maumivu niliyopata nilichukua uamuzi ambao sio sahihi wa kuuchana mpira kwa kisu, ingawa nakiri kosa,’’alisema.

Aidha mwananchi huyo alikiri kuwa, nyumba yake iko kando kando ya uwanja mpira unaotumika na hata kwa mashindani ya wilaya, na upo zaidi ya miaka 100 kwa sasa.



‘’Mimi pamoja na maumivu niliyoyapata, lakini nakiri kuwa, nilitakiwa niwafuate wazazi wa watoto ama niripoti kwa sheha, kwa kosa walilonifanya, lakini nilijichukulia sheria mikononi, sasa naahidi kuwa Arpili 28, mwaka huu nitawasilisha fedha hizo kwa sheha,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, mwananchi huyo, alishauri kuwa ni vyema michezo inapofanyika katika uwanja huo, wachezaji wawe na tahadhari, ya hali ya juu, kwani kwa eneo ulipo uwanja wanaweza kusababisha maafa kwa wazee na watoto.




Akizungumza kwa niaba ya baraza la watoto, Mratibu wa baraza hilo Waride Seif Mohamed, aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kuripoti kwa sheha, wanapokoseana katika jamii.

Alieleza kuwa, hakuna kinga ya kuwa na hasira na kujichukulia sheria mikononi, kwani kwa sasa vipo vyombo kdhaa ngazi ya shehia ikiwemo wasaidizi wa sheria, askari shehia, mratibu wa wanawake na watoto na sheha mwenyewe, kwa ajili ya kupokea malalamiko mbali mbali.


‘’Mimi niwashukuru wasaidizi wa sheria kutoka ‘CHAPO’ kwa kufanikisha kikao cha sulhu, maana kwa upande wa baraza, lilikuwa limeshashindwa juu ya mgogoro huo,’’alieleza.

Kwa upande wake Msaidizi wa sheria wa shehia ya Wesha, Khadija Said Khalfan, alisema watoto au kundi jingine lolote linapokosea, ni vyema taratibu za kisheria zifuatwe.

‘’Sisi wasaidizi wa sheria kutoka CHAPO, kila siku tunaelimisha jamii, juu ya namna ya kuvitumia vyombo vya kisheria, inapotokezea shida yoyote, lakini sio kujichukulia sheria mikononi,’’alifafanua.


Hata hivyo amewataka wachezaji wa klabu hiyo ya ‘kaza buti’ ya baraza la watoto la shehia ya Wesha, kuwa waangalifu wanapokuwa mazoezini, kwani uwanja wao, uko katikati ya makaazi ya wananchi.

‘’Ni kweli wananchi ndio waliofuata uwanja hapa, lakini hiyo haiwi sababu ya kutoangalia watu wanapopita, maana kila mmoja ana haki yake katika nchi,’’alieleza.

Sheha wa shehia ya Wesha Haji Mohamed Ali, alimtaka mwananchi huyo kuhakikisha analipa fedha hiyo kwa siku aliyoahidi mwenyewe, ili kuepussha mingine ya kisheria.

Alieleza kuwa, shehia yake inavyombo tofauti kama waratibu, kamati ya maadili, watu maarufu, wasaidizi wa sheria ambapo mote humo unaweza kuwasilisha malalamiko.

‘’Hakuna sheria yoyote hata kama watoto walikuzomea na kisha ukapandwa na hasiri juu ya suala la kujichukulia sheria mkononi, hapo ukifanya unanunua kosa jingine kisheria,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, sheha huyo, alisema watoto wanazo haki zao mbali mbali ikiwemo kucheza, kusoma, kupewa majina mazuri, matibabu, chakula na mavazi.

Hata hivyo, ameutaka uongozi wa timu hiyo ya kaza buti, kuwa makini wanapokuwa kwenye michezo yao, kujenga heshima kwa watu wote pamoja kuwathimini wapiti njia.

Mapema kiongozi wa timu ya Kaza buti ya baraza la watoto shehia ya Wesha, Ahmed Issa Adam, alisema baada ya tukio hilo, walimuomba radhi mwananchi huyo, ingawa alikataa.




Hata hivyo, aliwapongeza wasaidizi wa sheria kutoka ‘CHAPO’ kwa kuumaliza mgogoro huo, na kuahidi kuwaangalifu wanapokuwa kwenye mazoezi yao.

Timu ya baraza la watoto la shehia ya Wesha wilaya ya Chake chake, itarejea tena uwanjani kuanzia Aprili, 28 mwaka huu, kuendelea na mazoezi, baada ya kusita kufanya mazoezi, kufuatia mpira waliokuwa wakitumia kupasuliwa wiki tatu zilizopita.

                               Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’