CHAPO YAPOKEA WASAIDIZI WA SHERIA WAPYA, YAWAPA NENO
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
JUMUIYA ya wasaidizi wa
sheria wilaya ya Chake chake Pemba CHAPO, imewapokea wasaidizi wa sheria wapya
na kuwahakikishia ushirikiano wa hali ya juu, ili kufikia malengo ya kuihudumia
jamii, wilayani humo.
Hayo yalielezwa leo Machi 30, 2024
na Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, wakati wa ukaribisho na mapokezi ya
wasaidizi wapya watatu wa sheria, kutoka shehia za Michungwani, Kibokoni na
Mgelema, hafla iliyofanyika ofisi ya CHAPO, mjini Chake chake.
Alisema, C HAPO inafarajika mno
kuona sasa inaongeza idadi ya wasaidizi wa sheria 21, kutoka 18 wa awali, jambo
ambalo linaendelea kupunguza ukakasi kwa shehia 11, zitakazobakia bila ya kuwa
na wasaidizi wa sheria, kati ya zote 32 za wilaya hiyo.
Alieleza kuwa, wasaidizi hao wa
sheria wapya, watapewa kila aina ya ushirikiano, wakati huu wa miezi mitatu wakiwa
kwenye majaribio na hata baada ya kumaliza na kuanza kazi rasmi shehiani mwao.
Mkurugenzi Nassor alifafanua kuwa, wananchi
wa vijiji wanavyotoka wasaidizi hao wa sheria, kwa sasa wakae mkao wa kula kwa kuwatumia,
kwani wapo baadhi ya wananchi, wameshakata tamaa katika kuzipata haki zao.
‘’Kwanza nyinyi wasaidizi wa sheria
karibuni ‘CHAPO’ kwenye kazi ya kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria kwa
njia ya kujitolea, na tumefarajika kwa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria,
kutupatia watendaji hawa,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi
huyo wa CHAPO, aliwataka wasaidizi hao wa sheria wapya, kuhakikisha wanajenga ngome
imara ya ushirikiano na wenzao, kabla na wakati wanapotaka kutoa elimu ya
kisheria.
Hata hivyo, aliwakumbusha kuongeza
elimu ya sheria hatua kwa hatua, kwani changamoto za kisheria na mabadiliko
yake, yanakuja kila kila siku hapa Zanzibar.
Akizungumzia kuhusu kuhudhuria
kwenye vikao, aliwataka wasaidizi hao wa sheria wapya na wingine, kuhakikisha
wanafuatilia vikao hivyo, kwani ni muhimu kwa maendeleo ya CHAPO na wananchi wa
Chake chake kwa ujumla.
Wakati huo huo Mkurugenzi huyo, aliipongeza taasisi ya LSF kwa kuendelea kuwabeba na kuwawezesha katika mradi maalum wa miezi tisa wa upatikanaji haki, ambao umeshaanza mwezi Fubauri, mwaka huu.
Mapema Mratibu wa ‘CHAPO’ Mohamed Hassan
Abdalla, alisema mbinu ya kufikia malengo ya utoaji wa msaada wa kisheria,
inachangiwa na mambo kadhaa ikiwemo ubunifu, ushirikiano, kujituma na kukubali
kujifunza kila siku.
Akizungumzia suala la usajili kwa
wasaidizi wa sheria, aliwataka ambao bado, kuharikisha kufanya hivyo, hasa kwa
vile ada ya mwaka ya shilingi 20,000 ilishaondolewa na Waziri husika, tokea
mwaka jana.
Mkurugenzi fedha wa ‘CHAPO’ Riziki
Hamad Ali, aliwakumbusha wasaidizi wa sheria, kuendelea kuihudumia jamii,
katika kushughulikia changamoto zao, wakijua kuwa hiyo ni kazi ya kujitolea.
Msaidizi wa sheria, shehia za Wawi,
Mgogoni na Ziwani Fatma Hilali Salim, alisema ikiwa kuna upangwaji wa makundi ya
wasaidizi wa sheria, ni vyema kukaangaliwa jiografia, baina ya msaidizi wa
sheria mmoja na mwingine.
Nae Msaidizi wa sheria Abeda Abdi Seif, alisema moja ya mafanikio ya msaidizi wa sheria, ni kuhakikisha
anafanyakazi kwa karibu mno na sheha wake, ili kuona anapata nguvu ya
kushirikishwa.
‘’Inawezekana Msaidizi wa sheria
anamlalamikia sheha wake, kwamba hamshirikishi, lakini pengine mwenyewe anakuwa
ametingwa na kazi zake, kisha akamuangushia sheha lawama,’’alieleza.
Kwa upande wake msaidizi wa sheria
mpya kutoka shehia ya Mgelema Asha Juma Ali, alisema atahakikisha anayafanyia
kazi kwa vitendo, mafunzo aliyopewa hivi karibuni.
Nae Msaidizi wa sheria kutoka
shehia ya Kibokoni Haitham Hamad Khamis, alisema anachoomba ni ushirikiano wa
hali ya juu, kwa wale wenzake, waliomtangulia katika kazi hiyo.
Mkutano huo ambao ni wa kawaida
kila mwisho wa mwezi, kwa leo uliambatana na mafunzo ya ujazaji wa fomu za
elimu na msaada wa kisheria, kutambulishwa kwa wasaidizi wa sheria wapya waliomaliza
mafunzo hivi karibuni na utambuzi wa mradi wa upatikanaji haki.
Mwisho







Comments
Post a Comment