CHAPO YAMALIZA SIUTAFAHAMU MATUMIZI UWANJA WA SOKA WESHA

 



NA ABDALLA MBAROUK, PEMBA @@@@

WASAIDIZI wa sheria kutoka wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ wamemaliza siutafahamu ya matumizi ya uwanja wa mpira wa miguu, baina ya timu ya watoto ya Baraza la watoto la shehia ya Wesha na wachezaji wa vilabu vikubwa shehiani humo.

Itakumbukwa kuwa, Disemba 17, mwaka 2023, wasaidizi hao wa sheria, walipokea lalamiko la kusitishwa kwa matumizi ya uwanja uliopo Wesha kwa sheha, timu ya kazabuti inayomilikiwa na baraza la watoto la shehia hiyo, wakielezwa kuwa, hawana haki ya matumizi ya uwanja huo.

Ambapo baada ya malalamiko hayo, wasaidizi wa sheria kutoka CHAPO, wakiongozwa na Msaidizi wa sheria mwenyeji wa shehia ya Wesha, Khadija Said Khalfan, waliahidi kulitafutia ufumbuzi lalamiko hilo.

Msaidizi wa sheria huyo akiwa na wenzake watatu, waliahidi kukutana na uongozi wa vilabu vikubwa vinavyotumiwa uwanja huo, ili kuona na timu ya kaza buti ya baraza la watoto la shehia ya Wesha, nao wanautumia uwanja huo kufanya mazoezi.




Ndipo leo Machi 16, 2024, wasaidizi hao wa sheria, walikuwa na kikao cha wazi kati ya uongozi wa baraza la watoto, mwakilishi wa timu wanaotumia uwanja huo, askari shehia na wananchi wengine, na kukubaliana juu ya matumizi ya uwanjua huo.

Akizungumza kabla ya kufikia makubaliano hayo, Msaidizi wa sheria wa shehia Wawi Haji Nassor Mohamed, alisema moja ya haki ya msingi za mtoto, ni kucheza michezo kadhaa.

Alieleza kuwa, kama uwanja uliopo shehia ya Wesha ni mmoja, ni vyema kwa timu kubwa kupangiana zamu, ili na timu ya watoto ya Kaza buti, nayo ipate haki ya matumizi ya uwanja huo.





‘’Hii timu kubwa ya Wesha, ambayo sasa inaendelea kufanya vizuri, chanzo chake ilikuwa kama ilivyo hii ya watoto, ambapo kwa wakati huo, ililelewa na watu wazima waliokuwepo, na sasa ndio inatamba,’’alieleza.

Hivyo amewanasihi wachezaji wa timu kubwa, kuangalia uwezekano wa haraka, ili kuvilea vipaji vya watoto wao, kwani ndio wanapoanzia kutoka kwa wachezaji wa vilabu vya timu za Simba, Yanga na kisha timu ya taifa.

Awali Msaidizi wa sheria kutoka shehia ya Wara Sabah Abdalla Mohamed, alisema, watoto wanazo haki nyingi, moja wapo ni kusoma, kulindwa na kucheza.





‘’Sisi wasaidizi wa sheria, leo tumeshawakabishi mpira mmoja na filimbi, sasa ni wajibu wazazi, walezi, wamiliki wa uwanja na wachezaji wa timu kubwa, kupanga nao ratiba, ili wakuze vipaji vyao kupitia uwanja huo,’’alieleza.

Kwa upande wake Mkagauzi wa Polisi, anayeshughulikia shehia hiyo, Khamis Ali Khamis alisema, kukabidhiwa kwa mpira huo na ruhusa ya kucheza kwao, isiwe chanzo cha kukatisha masomo.

‘’Wakati mnautumia uwanja huu kukuza vipaji vyenu, mkumbuke kuwa, bado wajibu wenu wa kutafuta elimu na kusoma kwa bidii, ipo pale pale, sasa michezo isiwe chanzo cha kuacha masomo,’’alifafanua.



Mapema kiongozi wa timu ya Kaza buti ya baraza la watoto shehia ya Wesha, Ahmed Issa Adam, alisema watautumia muda wa ziada kufanya mazoezi katika uwanja huo.

Hata hivyo, aliwapongeza wasaidizi wa sheria kutoka CHAPO, kwanza kwa kutimiza ahadi ya kuwanunulia mpira na filimbi, kama ambavyo waliwaahidi wakati walipokutana nao mwishoni mwa mwaka, jana.




‘’Lakini tuendelee kuwashukuru kwa kulipatia ufumbuzi suala la matumizi ya uwanja, kwani timu kubwa, walidhani sisi hatuna haki ya matumizi ya uwanja, lakini leo, tunashukuru wameshakubali,’’alisema.

Mwakilishi wa vilabu vikubwa wanaotumia uwanja wa Wesha Kassim Yussuf Ali, alisema kuanzia sasa uwanja huo, utatumiwa na rika zote, ikiwa ni njia moja yapo ya kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji.

‘’Ni kweli hata sisi ambao leo tunaitwa timu kubwa, miaka 25 iliyopita tulikuwa wadogo na kuruhusiwa kucheza, na ndio maana sasa tunaiwakilisha hata Pemba, kwenye mpira wa miguu,’’alieleza.

Mratibu wa Baraza la watoto shehia ya Wesha Waride Seif Mohamed, alisema atahakikisha timu hiyo inafika mbali, kwani kwa sasa michezo imekuwa ikizaa ajira na kujenga uhusiano mwema.




Hata hivyo, alisema watajipanga vyema ili kuhakikisha wanalifanyia kazi wazo la kutafuta fedha nusu na kisha kuziwasilisha kwa wasaidizi wa sheria, kwa ajili ya ununuzi wa jezi kwa timu hiyo.

Wasaidizi wa sheria kutoka Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba CHAPO, wanaendelea na kutekeleza mpango wao kazi, wa kukutana na makundi mbali mbali, ili kusikiliza changamoto zao za kisheria.

                          Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’