USHAURI WA KISHERIA WA 'CHAPO' WAZAA MAKAAZI YA KUDUMU KWA MJANE




 HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

ZAKIA Rashid Baraka (36) wa Chanjamjawiri wilaya ya Chake chake, anaetgemewa na watoto sita, sasa amejengewa makaazi ya kudumu na aliyekuwa muume wake, baada ya kunufaika na ushauri wa kisheria, aliyopewa na wasaidizi wa sheri wilaya ya Chake chake.

Mjane huyo, alisema baada ya kuachika na aliyekuwa muume wake na kisha kumtaka ahame ndani ya nyumba waliokuwa wamejenga pamoja kijiji cha Tundaua shehia ya Kilindi wilayani humo, alimua kufuatilia haki yake kwa wasaidizi wa sheria.

Alisema, kisha mwanamme huyo alikutanishwa nae, na kutakiwa kunijenga chumba kimoja, kwa vile alishakataa kumpa chumba kimoja katika nyumba walipokuwa pamoja kindoa.





Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, nyumbani kwake Chanjamjawiri, alisema katika ujenzi wa nyumba hiyo anayoishi muume wake kwa sasa alitumia nguvu kazi na fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 1.

Alisema kuwa, alitegemea sana baada ya kuchwa aidha engerejeshewa fedha ama kupewa haki yake ya chumba kimoja, ingawa yote hayo hayakufanyika.

‘’Baada ya kufuatilia haki zangu kuanzia kwa sheha na ofisi ya Mufti Mkuu Pemba, mote nilikwama, lakini nilipopewa ushauri wa kisheria, nilifanikiwa na sasa naishi ndani ya chumba kimoja,’’alieleza.

Zakia alifafanua kuwa, kwa vile mama yake mazazi alishapiga fondesheni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya familia, ilikuwa rahisi kusimamisha matofali na kuezeka chumba chake kimoja, alichokubaliana na aliyekuwa muume wake.

‘’Ijapokuwa nilizaa nae mtoto mmoja, kati ya sita nilionao, lakini nilihitaji nipate haki yangu, na kwa sasa ameshanikabidhi chumba kimoja kikiwa kimeezekwa,’’alifafanua.

Hata hivyo amewashukuru wasaidizi hao wa sheria, kwa umakini wao wa kufuatilia lalamikoa lake, hadi kulipatia ufumbuzi, ambao ulishindikana katika taasisi nyingine.

Wakati huo huo Zakia, amewataka wanawake wenzake, wasikubali kuchangia wa nyumba au kununua kitu cha thamani pasi na kuandikiana na waume zao.

Sheha wa shehia ya Kilindi Nassor Mohamed Khamis, alisema anaifahamu vyema kesi ya mjane, ambayo anasema hata kamati ya shehia, ilishindwa kumnasihi na kukubaliana na ushauri wa aliyekuwa muume wake.

‘’Baada ya kumuona Mohamed Mohamed (muume), ni mzito wa kutuelewa, nilimataka Zakia (mjane), awasiliane na ofisi ya Mufti Mkuu, ingawa alirudi tena, kwamba hajafanikiwa na kumuelekeza kwa wasaidizi wa sheria,’’alieleza.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ ambae ndie aliyempa msaada wa kisheria mjane huyo, Nassor Bilali Ali, alisema awali, muume huyo alitaka kuwa mzito wa kufahamu, ingawa baadae alikiri na alihadi kumjengea.



‘’Huu unaweza ukawa mfano wa kwanza na mkubwa ndani ya wilaya ya Chake chake, lakini walionufaika na msaada wa kisheria katika maeneo mingine, wapo zaidi ya watu 7,000 kwa mwaka 2023,’’alifafanua.

Hata hivyo, alisema CHAPO inaendelea kumuangalia mjane huyo kwa karibu, na inatarajia kumsaidia zaidi, kumuwekea saruji chini na kumsaidia fikra ya kujenga banda ya vyumba viwili, kando ya chumba hicho, ili kutanua makaazi yake.

Mratibu wa LSF zoni ya Pemba, Hamisa Bakar alisema, LFS ikishirikiana na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, imekuwa ikiwawezesha kimafunzo na mbinu, wasaidizi wa sheria, ili kukabiliana na changamoto kama hizo.

Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, alisisitiza kuwa kusema kuwa, ni vyema wasaidizi wa sheria, wanapoibua changamoto, kuzifuatilia hadi upatikane ufumbuzi.

Sheria ya Msaada wa Kisheria Zanzibar nambari 13 ya mwaka 2018, ambayo imekuja kuanzisha Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, moja ya majukumu yake, ni kumtaka mtoa msaada wa kisheria, kutoa huduma ya msaada wa kisheria, kwa mtu asiyekuwa na uwezo.

                      Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’