CHAPO: NA MIAKA SABA YA MAPAMBANO YA UKATILI, UDHALILISAJI CHAKE CHAKE

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

CHAPO, ni kifupi cha Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba.

Ukiwa mtaalamu wa lugha sema ‘Chake chake Paralega Organization’ kwa ufupi ni CHAPO.

CHAPO, sio neno geni masikioni mwa wakaazi wa wilaya ya Chake chake, wanaoishi ndani ya shehia 32, ikiwemo za Vitongoji, Wesha na Chanjaani, inayobebwa na majimbo ya Chake chake, Ole, Ziwani, Chonga na Wawi.

Kwamba, humu ndio eneo la CHAPO inapofanyakazi, tena kupitia wanachama wake, ambao ni wasiaidizi wa sheria tena waliosajiliwa na kutambuliwa.

Kwa sasa, si haba kuanzia mwaka 2018, serikali imeshapitisha sheria rasmi, iliyokuja kuweka mambo yawe ‘shega’ mazuri ya wasaidizi wa sheria.

Maana, ipo sheria maarufu ya Msaada wa Kisheria Zanzibar nambari 13 ya mwaka 2018, ambayo awali ilitanguliwa na sera ya mwaka 2017, ambayio imekuja kumueleza nani Msadizi wa sheria?

Kwamb, ni yeyote aliyepata mafunzo ya awali ya sheria, na kisha kusajiliwa, na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, na kuanza kufanyakazi.

Kwani kazi zake zilizotajwa na sheria hiyo, ni kutoa elimu, ushauri na msaada lakini wa kisheria, tena bila ya malipo ya aina yoyote, kutoka kwa mwananchi.

Mkuu wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria ofisi ya Pemba, Bakar Omar Ali anasema, tena walengwa wakuu wa jambo hilo ni wananchi maskini, vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na wale wanaoishi katika mazingira magumu.



‘’Idara inaendelea kuwasimamia na kuwawezesha kimafunzo kila siku wasaidizi wa sheria, ili wakawasaidie wananchi wasiokuwa na uwezo wa kutafuta Wakili katika kutafuta haki zao,’’anasema.

Hata Mkurugenzi wa Idara hiyo, Zanzibar Allhajjjat Hanifa Ramadhan Said, anasema Idara ilibaini kuwepo kwa kundi kubwa la wananchi, wanaokosa haki zao na kisha kushindwa gharama za kuwalipa Mawakili.

‘’Ndio maana sasa, serikali ililazimika kuwa na sheria maalum ya Msaada wa Kisheria Zanzibar ya mwaka 2018, ambayo sasa itawatambua watoa msaada wa kisheria Zanzibar,’’anasema.

Kisha wasaidizi wa sheria, waliamua kuanzisha Jumuia zao, ili wawe wanafanyakazi kwa nguvu moja, na ndio maana kuanzia mwaka mwaka 2015 wazo la kuanzisha CHAPO lilianza kuzaliwa.

CHAPO NI IPI

Ni Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake CHAPO, ambayo yenyewe iliasisiwa na kutiwa roho mwaka 2016, kwa wakati huo, wakiwa na wanachama (wasaidizi wa sheria) 19.

Mkurugenzi Fedha wa CHAPO Riziki Hamad Ali, anasema moja ya malengo ya ‘CHAPO’ ni kuhakikisha wananchi na hasa waliokwisha kata tamaa, wanapata haki zao.



‘’Tukiwa sasa ndani ya miaka saba ya uzawa wa CHAPO na siku hizi 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji, tunayomengi ya kujivunia, ikiwa ni pamoja na watu kupata haki zao,’’anasema.

Anasema kesi kama ya shehia ya Kichungwani, ambayo baba wa kambu alimbaka watoto wake, ni moja ambayo wasaidizi wa sheria kutoka CHAPO waliibua.

Kesi hiyo ilishaanza kutaka kufifia, kwa vile familia zilishaanza kupasuka pande mbili, moja ikionekana kutokuwa tayari kesi hiyo kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Anasema zipo kesi kadhaa za watoto wenye ulemavu, ambazo wazazi walishasamehe kutokana na mazingira wanayoyakuta vituo vya Polisi, ingawa wasaidizi wa sheria walifufua matumaini.

‘’Hivi tunavyozungumza wako washtakiwa wanatumikia miaka 20 na wengine 25 chuo cha Mafunzo, kwa kesi ambazo sisi wasaidizi wa sheria tuliziibua na kisha kushirikiana na wahusika, kufikishwa mahkamani,’’anasema.

Mkurugenzi wa CHAPO Nassor Bilali Ali, anasema katika eneo ambalo CHAPO imekuwa bingwa mno kwa wilaya ya Chake chake, na hasa kwa ushirikiano wanaoupata kwa wadau wao.

‘’Nguvu na umadhubuti wa wasaidizi wa sheria wa wilaya ya Chake chake, imetokana na ushirikiano tunaoupata kuanzia Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, Jeshi la Polisi, wizara husika na jamii,’’anasema.

Zipo kesi nyingi kama vile eneo la Vikunguni na Ng’ambwa waathirika na familia zao zilishakata tamaa, kwamba aliyewadhalilishi ni mtu maarufu, lakini haki mwisho ilipatikana,’’anaeleza.

Msaidizi wa sheria Ali Salim Ali, anasema ujasiri wa kuziibua kesi za udhalilishaji na kisha kuzifikisha mbele ya vyombo vya sheria, ni kule Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria pamoja na taasisi ya LSF kuwawezesha kimafunzo.

‘’Kila baada ya muda, tunapewa mbinu mpya za mapambano haya na mingine, sasa sisi wasaidizi wa sheria wa ‘CHAPO’ tumekuwa bora kuliko taasisi nyingine kama hizi,’’anasema.

Anaona ndani ya siku hizi 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji na miaka saba ya CHAPO yapo mafanikio, ambayo wananchi wameyapata na walishakata tamaa.

Wasaidizi wa sheria Abeida Ali Seif, Mgeni Kombo Khamis, Khadija Said Khalfan na Mashavu Juma Mabrouk, wanasema hadi kufikia mafanikio hayo, wameshavuuka mabonde yenye mamba na mashimo.

Wanasema, zipo kesi wanapozifuatilia hutishiwa hata maisha yao na wakati mwingine, kuonekana kama vile hawafanyi jambo la maana kwa upande mwingine, laki kazi inaendelea.

‘’Sisi kwa upande wa watu wenye ulemavu, ndio hasa ambapo CHAPO imekuwa ikitusaidia, maana tunakotokea, ilikuwa hata kesi moja ya mtu mwenye ulemavu huikuti mahkamani,’’anasema Mashavu.

Ndani ya siku hizi 16 za kampeni ya kupinga Ukatili na Udhalilishaji zilizoanza Novemba 25 na zikitarajiwa kumalizika Disemba 10, pamoja na changamoto za watu wenye ulemavu, lakini mafanikio yapo.

Anatoa mfano kuwa, wameshazisimamia kesi kadhaa ikiwemo ya msichana aliyepwa ujauzito na Askari wa Chuo cha Mafunzo Kengeja, kwamba ile kufika mahakamani kesi hiyo ni hatua kubwa.

Katika maisha yake, CHAPO ilishahangaika huku na kule, kuwasaka wafadhili na kujipatia miradi kadhaa, ambayo ilikuwa ya kukoleza mwendo wa kasi wao.




Kwa mfano, kupitia washirika wao wa The Foundation for Civil Socity ya Tanzania, iliwahi kuwapa mradi wa ujenzi wa amani, ambao hapa wanawake wa wilaya ya Chake chake, walijifunza mingi.

Mradi mwingine, ambao nao ulikuja kuinua ufahamu wa wanawake wa wilaya hiyo ni wa ‘Uwezeshaji wa umiliki ardhi kwa wanawake’ ambapo ulitoa mwelekeo.

Maana Mkurugenzi wa CHAPO Nassor Bilali Ali, anasema miradi yote ni muhimu kwao, lakini huo wa ardhi uliwazindua wanawake kujua haki yao ya kumiliki ardhi.

‘’Hasa ulikuwepo kwenye shehia za eneo la Pujini, wananchi waliufurahia maana, wengi wanasema hawakuwa wakijua kuwa wana haki hiyo, kama ilivyo kwa wanaume,’’anafafanua.

Mkurugenzi Fedha wa ‘CHAPO’ Riziki Hamad Ali, anasema mradi ambao ulikuja hata kuwaamsha wananchi na wasaidizi wao wa sheria ni wa ‘Upatikanaji haki’ unaofadhiliwa na tasisi ya LSF.

‘’Kwa hakika mradi huu, lazima tuwapongeze wenzetu wa LSF, maana uliwasaidia mno wasaidizi wa sheria hata kujua wajibu wao kwa undani na namna ya kuwahudumia wananchi,’’anasema.

WADAU/WASHIRIKA WA CHAPO

Mwakilishi wa taasisi ya LSF, Zanzibar wakili Alphonce Gura, anasema CHAPO ni moja taasisi zinazofanya vizuri Tanzania, katika kutetea haki za binaadamu.

Anasema wamekuwa wakijituma hata kama hakuna maradi wa kusaidia huduma za kifedha kwa wasadizi wa sheria.

Mkuu wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Pemba Bakar Omar Ali, anasema lazima jumuiya nyingine ziige mfano wa CHAPO katika mbinu za utendaji kazi.

‘’Kwa mara ya kwanza CHAPO iliandaa mafunzo ya uwelewa wa sheria ngazi ya shehia, na walianzia shehia ya Wawi, hili ni jambo jema na ni mafanikio yao ya miaka saba,’’anaeleza.




Mkurgenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani Nassor Hakim Haji, anasema kazi zinazofanywa na CHAPO ni njema na wakati mwingine, wanasoma kutoka kwao.

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini y CHAPO Kassim Ali Omar na Mjumbe wa bodi hiyo Zuwena Hamad Ali, wanasema sasa jumuiya imekuwa daraja la upatikanaji haki.




‘’Watu wengi wenye kesi zao za udhalilishaji na hata ukatili, wanawatumia wasaidizi wa sheria kupata elimu, ushauri na msaada wa kisheria, jambo ambalo hapo kabla, ilikuwa shida,’’anasema Zuwena.

Sheha wa shehia ya Wawi Sahrifa Wazir Abdalla, anasema sasa CHAPO na wasaidizi wake wa sheria wamezaliwa upya, katika mampambo dhidi ya udhalilishaji.

‘’Kwa mfano katika shehia yangu, tunao wasaidizi wa sheria wawili, na wamekuwa masaada mkubwa kwangu, katika kuziibua kesi za udhalilishaji,’’anasema.

Sheha wa shehia ya Mkoroshoni Khamis Iddi Songoro na mwenzake wa Wesha Haji Mohamed Ali, wanasema wasaidizi wa sheria kutoka CHAPO, wamekuwa wakiwasaidia kwa kiwango kikubwa.

‘’Kwa mfano, sasa wanamikutano kwa ushirikiano kutoka shehia moja hadi nyingine, na hili sasa linawafanya wananchi waone kuwa, jambo la udhalilishaji ni mapambano ya wengi,’’anasema sheha wa shehia ya Wesha.



Katibu Mkuu wizara ya Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Abeida Rashid Abdalla, anasema asasi za kiraia zimekuwa na msaada mkubwa, katika mapambano ya ukatili na udhalilishaji.

Mkuu wa wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, anaeleza kuwa, taasisi za Jumuiya ya wasaidizi wa sheria, kama MDIPAO na CHAPO zimekuwa mstari wa mbele, kutoa elimu ya kujiepusha na janga hilo.

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said, anaeleza kuwa, lazima taasisi ziongeze ushirikiano katika mapambano hayo.

CHAPO ambayo ilianza na wasaidizi wa sheria 19, kwa sasa wanaowanachama 23, ingawa walio hai kwa maana ya kulipa ada na kufanyakazi ni 18, wakizihudumia sheria 32 za wilaya ya Chake chake.

                              MWISHO.

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’