BARAZA LA WATOTO WESHA, LAWATUNISHIA MISULI WASHUGHULIKIAJI KESI ZA UDHALILISHAJI
BARAZA la watoto wa shehia ya Wesha wilaya ya
Chake chake Pemba, wamesema vitendo vya ukatili na udhalilishaji vitaendelea kuwepo
na kuwaathiri, kwa vile watendaji, washughulikiaji, watoaji hukumu, wapelelezi
na madaktari ni watu wazima na sio katika kundi lao.
Walisema, wapo watoto wenzao wamedhalilishwa na wengine
kupata ulemavu wa kudumu na hata kusababisha vifo, ingawa kesi hizo,
zinapopelelezwa na kufikishwa mahakamani, watuhumiwa huachiwa huru.
Hayo wameyasema Disemba 17, 2023 kwenye mkutano wa wazi
ulioandaliwa na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’
na kufanyika uwanja wa mikutano nyumbani kwa sheha wa shehia ya Wesha, wilayani
humo.
Wamesema, inashangaaza kuona kesi zinazowahusu watoto
kudhalilishwa au kufanyiwa ukatili, zinapelelezwa na kutolewa ushahidi, ingawa
kisha hufutwa na kuwaacha wao na maumivu.
Katibu wa Baraza hilo Zainab Kassim Juma, alisema kwa
vile watoto ndio wanaodhalilishwa na watu wazima, kisha wanapofika mahkamani, huachiliwa
huru na watu wenzao.
‘’Sisi watoto tunadhalilishwa wakati mwengine na wazazi
wetu, waalimu na hata watu wingine, lakini kesi hiyo ikifikishwa mahakamani,
huachiana na kutuongezea sisi maumivu,’’alisema.
Nae mjumbe wa Baraza hilo Said Mohamed Ali, alisema, lazima
wanaotetea haki za watoto wasimame imara, ili udhalilishaji wanaofanyiwa,
ulipwe kupitia njia ya mahakama.
‘’Inauma kuona mtoto ameharibiwa mbele na nyuma na
mtuhumiwa amepatikana, lakini ikitokea kasoro ndogo kwenye ushahidi, mtuhumiwa
anaachiwa na sisi kuishi na kilema na maumivu ya kudumumu,’’alieleza.
Kwa upande wake, mtoto Samir Magessi, alisema watoto
wakati mwingine wamekuwa wakitumiwa katika usafirishaji wa dawa za kulevya.
Akifungua mkutano huo, Mratibu wa wanawake na watoto wa
shehia ya Wesha Waride Seif Mohamed, alisema suala la kupiga vita vitendo vya
ukatili na udhalilishaji, linahitaji nguvu ya pamoja.
‘’Kama walivyofanya wenzetu hawa wasaidizi wa sheria
kutoka CHAPO, kufika hapa shehia ya Wesha kuonana na watoto, ni vyema na kila
mmoja, kuiga mfano huu,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mratibu huyo wa wanawake na watoto
shehia ya Wesha, aliwataka wazazi na walezi, kuwawekea muda wa kucheza watoto
wao, ili ubongo wao upate kukua.
‘’Isiwe kila wakati watoto wanafanyishwa kazi za
majumbani, wakati mwingine waachiwe kujichangamsha na wenzao, ili wapate
kubadilisha uzoefu na kuendeleza ukuaji wao,’’alifafanua.
Mapema Msaidizi wa sheria wa shehia ya Wesha Khadija Said
Khalfan, aliwatahadharisha watoto hao, kuacha mtindo wa kujificha vikani,
wanapoamua kutohudhuria masomoni.
Aidha aliwataka watoto hao, kujitenga mbali na kupokea zawadi
ovyo ovyo, na kukubali kupanda baiskeli au vyombo vya moto bila ya sababu ya msingi.
‘’Wengine wanaweza kuwapa msaada wa boda boda, kuwaonesha
picha chafu au kuwapa pesa na pipi, jihadharini na ikitokezea hivyo kwa mmoja
wenu, toweni taarifa,’’alieleza.
Nae Msaidizi wa sheria Jimbo la Wawi Haji Nassor Mohamed,
alisema moja ya njia ya kujikinga na vitendo vya ukatili na udhalilishaji, ni
kutoa taarifa za awali.
‘’Kama mtamuona mwenzenu ameanza tabia hatarishi, mfano
kuchezewa chezewa sehemu zake za siri au anapewa pesa na msaada hata wa basikeli
kwa mtu asiyekuwa wa kawaida, msikae kimnya,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, Msaidizi huyo wa sheria, aliwaahidi
watoto hao, kushughulikia changamoto yao ya kukatazwa matumizi ya uwanja wa
mpira wa miguu na timu kubwa ya Wesha nyakati za jioni.
Huu ni mkutano wa saba, kuendelea kufanywa na timu ya
wasaidizi wa sheria kutoka shehia za Wesha, Wawi, Wara na Mgogoni wilaya ya Chake
chake, kwa kukutana na makundi tofauti, kutoa elimu ya sheria.
Mwisho
Comments
Post a Comment