WANAKONGAMANO: ‘RUSHWA MUHALI ITAENDELEA KUTUTAFUTA MAPAMBANO DHIDI YA UDHALILISHAJI’
WAATHIRIKA
wa matendo ya ukatili na udhalilishaji kisiwani Pemba, wamesema pamoja na
juhudi za serikali kuweka mazingira ya kupungua matendo hayo ikiwemo kuweka
adhabu kali, bado rushwa muhali ni kikwazo katika jamii.
Wakizungumza
kwenye kongamano la siku moja la kuelekea siku 16 za kupinga ukatili na
udhalilishaji, lililoandaliwa na Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake
chake Pemba CHAPO, na kufanyika ofisi ya TAMWA Chake chake, washiriki hao walisema
bado rushwa muhali ni changamoto.
Walisema bado
katika jamii, suala la rushwa muhali linaendelea kujitokeza, hali inayosababisha
kuimarika kwa matendo ya ukatili na udhalilishaji.
Hidaya Mjaka
Ali kutoka Umoja wa watu wenye Ulemavu UWZ, alisema, serikali imezirekebisha
sheria, kwa kuongeza adhabu ya kuanzia miaka 30 na kuendelea.
Alieleza kuwa
kama hilo lipo, ni wajibu sasa kwa mahakim na majaji kuzifuata sheria hizo, wakati
wa kutoa hukumu, waathirika wapate imani na vyombo vya sheria.
Kwa upande
wake, Mratibu wa Jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake CHAPO,
Mohamed Hassan Abdalla, alisema kama sheria ya Mtoto nambari 6 ya mwaka 2011, itatekelezwa
ikiwemo ujenzi wa nyumba salama, inaweza kusaidia kupunguza matendo hayo.
Mshiriki
Andikalo Juma Bilali wa Chanjamjawiri, alisema bado katika vyombo vya sheria,
kuna dalili ya rushwa na kusababisha wadhalilishaji kurejea makosa.
Aidha mshiriki
Bakar Haji Bakar kutoka TAMWA, alishauri kuwa wakati umefika sasa, kuwepo kwa
mabadiliko ya sheria, na kusababisha waliobakwa, ikiwa wametengeneza mazingira,
nao kupewa hukumu.
‘’Kama sasa
na wanawake waliobakwa, itaonekana wamechangia kwa njia moja ama nyingine, basi
sheria iwaangalie, ili sasa kupunguza matendo hayo,’’alieleza.
Akifungua kongamano
hilo, Mjumbe wa bodi ya wadhamini wa ‘CHAPO’ Zuwena Hamad Ali, alisema kila
mmoja ni muathirika wa matendo hayo, hivyo lazima nguvu iwe ya pamoja.
Alieleza,
iwe ni wasaidizi wa sheria, wanasheria, jamii, viongozi wa dini na wanaharakati,
ni vyema tukaunganisha nguvu za pamoja katika kuzuia viashiria vya
udhalilishaji.
‘’Majanga ya
ukatili na udhalilishaji yapo kila eneo, sasa ni wajibu wetu sisi jamii,
kushirikiana ili kuwashinda wadhalilishaji, maana kwa bahati nzuri, wamo katika
jamii zetu,’’alifafanua.
Akizungumzia
kuhusu elimu, alisema bado inahitajika hasa suala la ushahidi na haki za
watuhumiwa, ikiwemo dhamana jambo ambalo lipo kwa mujibu wa sheria.
Mwanasheria kutoka
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba, Asiya Ibrahim Mohamed, aliwashauri
wahanga wa matukio ya udhalilishaji, kuendelea kutumia ofisi yao, wanapoona kesi
zao, haziendi vyema.
‘’Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka, ipo kwa ajili ya kusimama na wahanga wa jinai, hivyo
wananchi hawanabudi kuendelea kufikisha malalamiko yao, ili kupatiwa ufumbuzi unaofaa,’’alifafanua.
Kuhusu idadi
ya mashahidi, alisema hakuna haja ya kuwa na idadi ya kundi la mashahidi, bali
muathirika na mtendaji wakati mwingine inatosha kumaliza kesi.
‘’Wazazi,
madaktari, Polisi mpelelezi na watu wa karibu ni kama kuongeza nguvu ya
ushahidi, katika mambo mbali mbali, ikiwemo umri, suala la ruhusa na muda wa
tukio husika,’’alifafanua.
Mkurugenzi
wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba, CHAPO Nassor
Bilali Ali, alisema lengo la siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji, ni kujadili
changamoto na mafanikio katika mapambano hayo.
Alieleza kuwa,
CHAPO imekuwa ikikutana na makundi mbali mbali kama wanafunzi, watu wenye
ulemavu, viongozi wa dini, wahanga wa matukio ya udhalilishaji na wasaidizi wa
sheria.
Mwisho
Comments
Post a Comment