CHAPO: ‘WAZAZI WALINDENI WATOTO NA MVUA ZINAZONYESHA’
UONGOZI wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya
Chake chake Pemba ‘CHAPO’ umewakumbusha wazazi na walezi, kuwalinda kwa nguvu
watoto, hasa katika kipindi hichi cha mvua, ili kuwaepushia na kukumbwa na
ajali kutokana na madimbwi ya maji.
Akizungumza na waandishi
wa habari ofisini kwake mjini Chake Chake, Mkurugenzi wa CHAPO Nassor Bilali
Ali, alisema wakati huu mvua zikiendelea kunyesha, ni vyema kwa wazazi na
walezi, kuwa makini na watoto wao.
Alieleza kuwa, Pemba inayomilima mikubwa iliyotengeneza misingi
yenye kupita maji kwa nguvu kuelekea baharini, hivyo ni vyema wazazi wakaongeza
ulinzi kwa watoto wao, ili kuepukana na majanga hayo.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa, zipo baadhi ya familia kwa
kujua ama kutokujua, wameanzisha makaazi maeneo ya mabondeni, ambako maji
yanakuwa na nguvu, hivyo kwa kipindi hichi cha mvua za vuli, wakawa makini na
jambo hilo.
‘’Sisi CHAPO tunatoa tanbihi ya kuwataka wazazi na walezi,
kuhakikisha wanawatunza watoto wao, maana mvua hizi zimekua na maji yenye nguvu
na kasi ya aina yake,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa CHAPO Nassor Bilali
Ali, amewataka wananchi kuendelea kufuatilia kwa karibu vyombo vya habari, ili
kuwasikiliza watabiri wa hali ya hewa wanavyoelezea.
Wakati huo huo Mkurugenzi huyo, amewataka wasaidizi wa sheria
wa wilaya ya Chake chake, wasisitishwe na mvua na badala yake, waendelee
kuwahudumia wananchi wanaohitaji elimu, ushauri au msaada wa kisheria.
‘’Hata mvua ikinyesha kubwa kiasi gani n ahata jua litoke leye
ujazo wa juu, bado kazi na wajibu wa wasaidizi wa sheria upo pale pale,’’alisisitiza
Mkurugenzi huyo wa CHAPO.
Kwa upande wake Mkuu wa Program za Mtandao wa Kupinga Utumikishwaji
wa Watoto Tanzania ‘TCACL’ Adam Matiko Charles, alisema mvua upande mmoja ni
neema, lakini kama wazazi watajisahau, inaweza kugeuka janga.
‘’Wapo watoto wamekuwa wakibururwa na maji, wakati mvua
inaponyesha, sasa niwaase wawe makini na jambi hilo, maana watoto waliowengi
wanapenda kucheza kwenye mitaro,’’alieleza.
Nae Mratibu wa Jumuiya kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa
akili Zanzibar ‘ZAPDD’ ofisi ya Pemba Khalfan Amour Mohamed, alisema mkazo kwa wazazi
uwekewe wa kuwalinda watoto, ingawa zaidi kwa wale wenye ulemavu wa akili.
‘’Watoto wote wanapaswa walindwe kwa kuacha kucheza mvuani,
kuchezea maji machafu, lakini wale wenye ulemavu hasa wa akili, waangaliwe
maara mbili,’’alifafanua.
Hata hivyo Mratibu huyo, amerejea kauli yake, ya kuwataka
wazazi na walezi, kutorubuniwa na watuhumiwa, mara wanapobainika kuwafanyia
udhalilishaji watoto wa kundi hilo.
‘’Wapo baadhi ya wazazi na walezi, wamekuwa rahisi kuchukua
fedha au kitu cha thamani kutoka kwa mtuhumiwa, akielezwa kuwa kesi ya mtoto mwenye
ulemavu wa akili, haiwezekani kushinda mahakamani,’’aliwakumbusha.
Mapema Afisa Elimu na Mafunzo
ya Amali wilaya ya Chake chake, Bur-han Khamis Juma, akizunguma hivi karubuni,
aliwataka wazazi kwa wale wanafunzi wanaolazimika kuvuuka mito na daraja, aidha
kuwasindikiza ama kuwazuia wanapoona mvua kubwa.
‘Wapo baadhi ya wanafunzi, ili wafike na kurudi skuli au madrassa,
lazima wavuuke mito au daraja zisizo za uhakika, sasa ni wajibu wetu sisi
wazazi, kuhakikisha usalama wa mtoto hao,’’alifafanua.
Mwalimu mkuu wa skuli msingi ya Dk. Philip Mpango Halima Khamis
Salim, alisema wamekuwa na utaratibu wa kuwataka baadhi ya waalimu, wanaokaa
maeneo yenye hatari kwa wanafunzi, kufuatana nao.
Sheha wa shehia ya Wawi Sharifa Abdalla Waziri, alisema wazazi
na walezi wana wajibu wa kuwachunga mno watoto, hasa katika kipindi hichi cha
mvua.
Wazazi Issa Nassor Issa na Time Vuai Mjengo, walisema lazima
mamla husika zitilie mkazo uwekaji imara miundombinu ya michirizi, ili maji
yapite kwa haraka na sio kukimbilia kwenye makaazi ya watu.
Mwanzoni mwa mwezi uliopita, mtoto mmoja mkaazi wa kijiji cha
Msingi wilaya ya Chake chake, aliripotiwa kufarikia dunia, baada ya kushindwa
kuvuuka msingi uliokuwa na maji yenye kasi, kwa kubururwa masafa marefu.
Mwisho




Comments
Post a Comment