‘TCACL’: ELIMU IWE NYUNDO YA KUVUNJIA VIKWAZO VYA MTOTO WA KIKE’

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA

MKUU wa Program za Mtandao wa Kupinga Utumikishwaji wa Watoto Tanzania ‘TCACL’ Adam Matiko Charles, amesema wakati Afrika, ikiadhimisha siku ya haki za binaadamu, lazima jamii iondokane na mawazo pekee kuwa, elimu ni haki ya msingi, na waifanye kuwa nyundo ya kuvunja vikwazo kwa mtoto wa kike.

Alisema, jamii bado inamtazamo wa zamani juu ya elimu, kama haki ya kawaida ya msingi kwa mtoto, lakini wakati umefika sasa, kuifanya nyundo yenye kuvunja na kupasua vikwazo, vinavyomzungumka mtoto wa kike.

Mkuu huyo wa Program, aliyasema hayo skuli ya msingi ya Dk. Philipi Mpango, Gombani Chake chake kisiwani Pemba, wakati akizungumza na wanafunzi, waalimu, wazazi na watetezi wa haki za binaadamu, kwenye maadhimisho ya siku ya haki za binaadamu Afrika.

Alisema, siku hiyo ni muhimu kwa jamii, kuangalia ikiwa kuna vikwazo mbali mbali kwa mtoto wa kike, na kuangalia uwezekano kwa kuviondosha kupitia elimu wanayoipata.





‘’Kwa sasa, lazima elimu bora na yenye manufaa kwa mtoto wa kike, isiwe kama anasa, bali iwe msingi mkuu wa kumuwezesha kijinasua na majanga mbali mbali kama ya udhalilishaji, ukatili wa kingono,’’alieleza.

Kataika hatua nyingine alisema, wakati umefika sasa kwa asasi za kiraia, mashirika pamoja na serikali kuu, kuunganisha nguvu za pamoja, ili kupinga utumikishwaji wa watoto Tanzania.

‘’Kwa mfano utumikishwaji, ajira za utotoni, ukatili wa kijinsia, kukoseshwa haki za elimu, matunzo, afya bora na makuzi na malezi ambayo ndio msingi mkuu wa maisha yao baadae,’’alieleza.

Kuhusu Mtandao huo, Mkuu huyo wa Program alisema, kuwa wanaowanachama 40 kwa Tanzania bara na Zanzibar, ambapo wamekuwa wakihakikisha watoto wanakuwa salama, katika nyanja mbali mbali za maisha yao.

Mapema Afisa Elimu na Mafunzo ya Amali wilaya ya Chake chake, Bur-han Khamis Juma, aliwataka watoto, kuweka pembeni anasa na kushughulikia zaidi elimu, ambayo ndio mkombozi wao wa baadae.

Alieleza kuwa, wakati huu wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali ikiendelea kuweka miundombinu rafiki ya kujipatia haki ya msingi ya elimu, ni vyema wanafunzi wakakaza kamba, wanapokuwa masomoni.





‘’Wizara imekuwa ikijenga miundombinu ya kisasa ya elimu, pamoja na upatikanaji wa vitabu, sasa ni wajibu wenu wanafunzi kusoma kwa bidi, ili ufaulu uongezeke,’’alieleza.

Akizungumzia kuhusu siku ya haki za binaadamu barani Afrika, alisema ni siku ya kutafakari juu ya haki za binadamu, zinavyovunjwa na baadhi ya watu, jambo linahatarisha maendeleo katika sekta mbali mbali.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jumuiya za wasaidizi wa sheria Pemba ‘JUWASPE’ Nassor Bilali Ali, alisema kama jamii haikuweka mkazo katika kuzilinda haki za binaadamu, kunaweza kukaendelea kuripotiwa visa kadhaa.




‘’Kila mmoja, na kwa nafasi yake anayonafasi ya kuzilinda haki za binaadamu, na wala hakuna sheria au kanuni, inayohalalisha watu kujichukulia sheria mikononi, maana vyombo husika vipo,’’alieleza.

Mwalimu mkuu wa skuli hiyo Halima Khamis Salim, alisema maadhimisho hayo kufanyika skulini kwake, kumesaidia kuwaasha watoto, namna bora ya kudai haki zao mbali mbali.




Sheha wa shehia ya Kwale Khamis Salim Ali, alisema vyombo vya sheria vinawajibu wa kutoa adhabu kali, kwa washtakiwa wa makosa mbali mbali ya ukatili wa kijinsia.






Hii ni mara ya kwanza kwa Mtandao wa kupinga utumikishwaji wa mtoto Tanzania ‘TCACL’ kufanya maadhimisho ya siku ya haki za binaadamu Afrika, ambapo ujumbe wa mwaka huu ‘haki ya elimu bora kwa wote na haki kwa Afrika’, awali kulitanguliwa na matembezi ya wanafunzi, waalimu na watetezi wa haki za binaadamu.

                             Mwisho    

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’