CHAPO YAACHA UJUMBE KWA WANAOWAFUNGIA NDANI WATU WENYE ULEMAVU
NA MWANDISHI
MAALUM, CHAPO@@@@
JUMUIYA
ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba CHAPO, imewataka wananchi wa
kijiji cha Tondooni, shehia ya Wesha wilayani humo, kujua kuwa, kumfungia ndani
mtu mwenye ulemavu, ni kosa kisheria kwa vile kumkosesha haki zake za
binaadamu.
Wito huo
umetolewa na Msaidizi wa sheria jimbo la Wawi Haji Nassor Mohamed, wakati,
akiwasilisha mada ya haki za binaadamu, kwa wananchi wenye ulemavu, kwenye mkutano
wa wazi, ulioandaliwa na ‘CHAPO’ na kuendeshwa na wasaidizi wa sheria.
Alisema,
hakuna sababu ya mzazi, mlezi kumfungia ndani mtoto mwenye ulemavu, kwa sababu
ya ulemavu wake, hivyo kisheria anatakiwa kupelekwa kwenye vituo vya elimu,
bila ya kujali aina ya ulemavu aliyonao.
Alisema,
serikali kwa upande wake imeshaweka mazingira rafiki kiasi, kwa wanafunzi wenye
ulemavu na mahitaji maalum, ikiwemo kuanzisha madarasa mjumuishi, kuweka vitengo
pamoja na kuanzisha sheria ya kuwalinda.
‘’Kwa mfano
ipo sheria mpya ya watu wenye ulemavu Zanzibar nambari 8 ya mwaka 2022, baada
ya kufutwa ile ya mwaka 2016, sasa ni wajibu wa wazazi na walezi, kuona wanawapatia
elimu na haki zao nyingine kundi hilo,’’alieleza.
Akitaja miongini
mwa haki za binaadamu kwa watoto au watu wenye ulemavu alisema ni elimu,
matunzo, mavazi, matibabu, kushirikishwa, kuoa na kuolewa, malazi na chakula
bora.
Hata hivyo,
aliwataka wazazi kuwatoa nje watoto waliowafungia na kuwaandikisha skulini, ili
wapate haki zao za elimu, na kuacha visingizio vya hali baya waliyonayo watoto
hao.
Kwa upande
wake, Msaidizi wa sheria Jimbo la Chake chake Wahida Kombo Khamis, amewatahadharisha
watoto, kutokubaliwa kurubuniwa kwa kupewa zawadi au fedha na watu wasiowajua.
Alisema, kwa
sasa wadhalilishaji hutumia fedha kidogo au kuwaonesha watoto picha chafu
kupitia simu janja, na kisha kupata mwanzo wa kuwadhalilisha kingono, jambo
ambalo, huwaharibia maisha yao.
‘’Pendeleeni
sana mnapokwenda na kurudi skuli ama madrasaa, muwe mnafuatana kwa kundi na
anapopata shida mwenzenu, kimbilieni kutoa taarifa kwa wazazi, walezi, waalimu
au watu wengine wa karibu,’’alieleza.
Akieleza lengo
la mikutano hiyo ya wazi Msaidizi wa sheria Jimbo la Ziwani Khadija Said
Khalfan, alisema CHAPO imekuwa ikiwafikia wananchi katika maeneo yao, ili kuhakikisha
wanapa uwelewa wa masuala la kisheria.
Alieleza kuwa,
pamoja na kuwa na jukumu la kutoa elimu kwa wananchi wanaofika ofisini kwao mjini
Chake chake, lakini wameona ni bora kwenda katika vijiji mbali mbali kuwafuata.
‘’CHAPO
ambayo ni taasisi ya kiraia, inawakaribisha kuja ofisini kwetu kupata elimu,
ushauri na msaada wa kisheria, kwa kesi yeyote tena bila ya malipo, maana hilo
ndio jukumu letu kuu na la msingi,’’alieleza.
Mapema sheha
wa shehia ya Wesha Haji Mohamed Ali, alisema mpango ulioandaliwa na CHAPO,
unasaidia mno kuwaamsha wananchi hasa wanaozikalia haki za wengine.
‘’Ni kweli
wapo wananchi, wamewafungia ndani watoto wenye ulemavu na wamekuwa wakiwakosesha
haki zao kama za chanjo, elimu na hata kuwashirikisha, imekuwa ni vigumu,’’alieleza.
Baadhi ya
wananchi wa kijiji cha Tondooni akiwemo Khadija Mohamed Salim, walisema, ipo
tabia ya kufungiwa ndani watoto wenye ulemavu, wazazi wakidai kuwa hawana uwezo
wa kusoma.
Hata hivyo,
alisema bado baadhi ya madrassa za Qur-an zinakabiliwa na ukosefu wa vyoo na maji
safi na salama, jambo linalowafanya wanafunzi kujisaidia vichakani.
Mkutano huo
wa wazi, ni muendelezo wa watendaji wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya
Chake chake CHAPO, kukutana na wananchi, ili kusikiliza kero zao kisheria.
Mwisho






Comments
Post a Comment