WASAIDIZI WA SHERIA 'CHAPO' WATOA UJUMBE KWA WANAFUNZI
Na,
Hassan Msellem, Pemba
WANAFUNZI
skuli ya Sekondari ya Dk. Salim Ahmed Salim iliyopo Wara wilaya ya Chake -chake
Pemba, wametakiwa kujiepusha na vitendo vya udhalilishaji na utumiaji wa dawa
kulevya, ili kufikia malengo waliojiwekea.
Akitoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wanafunzi
hao Septemba 11, 2023, Msaidizi wa
Sheria shehia ya Wawi Haji Nassor Mohamed, alisema tafiti zinaonesha kuwa, waathirika
wakuu wa vitendo hivyo, ikiwemo ubakaji, ulawiti na ukatili wa kijinsia, ni
wanafunzi skuli.
Aidha amewasihi wanafunzi hao, kuwatumia wasaidizi
wa Sheria, ili kupata ufumbuzi juu ya changamoto mbali mbali za kisheria,
zinazowakabili.
"Udhalilishaji ni
kumfanyia mtu kitendo chochote, ambacho kitamuathiri kimwili, kiakili au
kisaikolojia, hivyo ni vyema mkajiepusha na hili,’’alieleza.
Nae Msaidizi wa Sheria Jimbo la Wawi Fatma Hilal,
amesema miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya wanafunzi kushindwa
kuendelea na masomo na kutokutimiza ndoto walizojiwekea ni pamoja utumiaji wa
dawa za kulevya.
"Kuna
athari nyingi sana za utumiaji wa dawa za kulevya na miongoni mwa athari hizo,
ni mabadiliko hasi ya kitabia ambayo mabadiliko hayo yanapelekea wizi, ubakiji,
ulawiti kama ni mwanafunzi unapotumia tunaweza kushindwa kuendelea na masomo,’’alifafanua.
Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi
kutoka Shehia za Wawi na Wara Inspekta Issa Ahmada Iddi, amewasihi wanafunzi
hao, kuachana na dhana kuwa, mwanafunzi hawezi kuchukuliwa hatua za kisheria,
pindi anapofanya kaso, jambo ambalo sio sahihi.
Akifunga mkutano huo mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Khamis
Said Othman, amewasihi wanafunzi hao kuwa karibu zaidi na walimu wao, ili
kufahamu changamoto zinazowakabili na kuweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
"Mimi ni wasihi tu
kuwa licha ya kupata elimu hii ya kupinga udhalilishaji na athari za matumizi
ya dawa za kulevya, bado muelewa kuwa, mshauri wenu mkuu ni waalimu kabla ya
kuzifikisha popote,’’alifafanua.
Sheha wa shehia ya Wara, Massoud
Mohamed Khamis aliwakumbusha wanafunzi hao, kuwaripoti kwenye vyombo vya sheria
wazazi na walezi, ambao wanajihusisha na vitendo viovu ikiwemo, vya ulevi na udhalilishaji.
"Tunafahamu kuwa
wapo baadhi ya wazazi na walezi wenye tabia mbaya, ikiwemo ya ulevi, wizi
pamoja na kuwadhalilisha watoto kingono, naomba niwaambie kuwa musiwavumilie watu
wa aina hii, na msisite kutoa taarifa kwa walimu wenu,’’aliwakumbusha.
Nao baadhi ya wanafunzi hao wameahidi kuifanyia
kazi elimu hiyo, ili kufanya vizuri katika masomo sambamba na kutimiza ndoto
walizojiweke.
"Kwakweli leo
tumejifunza mambo mengi sana, kuhusu udhalilishaji na athari ya matumizi ya
dawa za kulevya, na tunaahidi kuitumia elimu hii katika kipindi chote cha
maisha yaetu,’’walisema wanafunzi hao.
Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria Wilaya ya Chake
Chake (CHAPO), kwa sasa imo katika mkakati maalum wa kukutana na makundi
kadhaa, kutoa elimu, ambapo hivi karibuni ilikuwa shehia za Mvumoni, Wesha,
Kilindi, Ole, Ziwani na Uwandani.
|
MWISHO |
|








Comments
Post a Comment