CHAPO: ‘WARIPOTINI WAZAZI, WAALIMU, WAJOMBA WANAOTAKA KUWADHALILISHA''

 



NA MWANDISHI WETU, PEMBA

WANAFUNZI wa chuo cha Kur-an cha Kichangani shehia ya Mgogoni Jimbo la Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba, wamekumbushwa kuwaripoti wazazi, waalimu, walezi na watu wengine, wanapoona dalili za wao, kutaka kudhalilishwa.

Walieleza kuwa, moja ya dalili hiyo ni mtu huyo kuongeza mapenzi ya kupindukia, kumpa zawadi zisizotarajiwa na kumshika shika sehemu nyeti za mwili wake, ikiwemo kifuani na makalio.

Ushauri huo umetolewa na Msaidizi wa sheria, Jimbo la Wawi Fatma Hilali, wakati akizungumza na wanafunzi hao na waalimu, kwenye mkutano wa wazi, wa utoaji elimu, juu ya namna ya kujikinga na majanga yakiwemo ya udhalilishaji.

Aliwaambia wanafunzi hao kuwa, dalili nyingine ni kupigwa mabusu sehemu tofauti za mwili, kupewa fedha na hasa na mtu asiyemjua pamoja na kupakatwa.

‘’Wanafunzi mkiona kuna dalili za kawaida, mtu anakushika kwenye mashavu, makalio, kifuani, mbavuni, anakupa pesa na hasa kwa mtu wa nje, pipi toweni taarifa kwa waalim au wazazi,’’alisema.

Katika hatua nyingine, Msaidizi huyo wa sheria, alisema moja ya athari za udhalilishaji kwa watoto, ni kupata athari ya viungo vya uzazi, kiakili, kupoteza mwelekeo wa masomo.



Kwa upande wake Msaidizi wa sheria wa shehia ya Wawi Haji Nassor Mohamed, aliwataka wanafunzi hao, kuacha michezo inayopelekea kugusana sehemu zao nyeti, ikiwemo makalio.

‘’Kuna michezo hasa kwa wanafunzi wa kike, ya kupigana makofi kwenye makalio na kisha kufukuzana, na kwa wanaume kuchezeana chezeana ovyo, michezo hii inaweza kuzaa janga, iacheni,’’alieleza,

Akizungumzia haki za watoto kwa mujibu wa sheria ya Mtoto nambari 6 ya mwaka 2011, alisema ni pamoja na kupewa jina zuri baada ya kuzaliwa, matibabu, elimu, matunzo, kulindwa pamoja na kusikilizwa.

Aidha aliwaeleza wanafunzi hao kuwa, wajibu wao kwa jamii, ni kuwatii wazazi, walezi, waalimu, kushiriki kwa mambo yanayowahusu, kushughulikia masomo na kutoa taarifa zinazoweza kusababisha madhara kwao.




Mapema Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Mgogoni Khadija Ramadhan Mbwana, aliwataka wanafunzi hao, kuacha tabia ya kujificha vikachakani.

‘’Wapo wanafunzi wanaondoka nyumbani, lakini wanaishia vichakani na ikifika wakati wenzao wanarudi madrassa nao huungana pamoja, jambo sio zuri,’’alikemea.

Katika hatua nyingine, Mratibu huyo alipongeza utaratibu wa ‘CHAPO’ wa kuunda timu ya wasaidizi wa sheria, kupita katika makundi ya jamii, kutoa elimu ya majanga mbali mbali.

Akifungua mkutano huo, Mwalimu mkuu wa Madrassa hiyo Mohamed Ali Omar, alisema njia ya ushirikiano katika kuwalinda watoto na majanga, inaweza kuwasaidia kuwaweka salama.

‘’Kama wazazi, walezi, waalimu, wasaidizi wa sheria na serikali tukiungana kuwalinda watoto, wahalifu wanaweza kukoma, kwani kwa sasa mashambulizi yanaelekezwa kwao,’’alieleza.




Mwalimu Zaina Jongo Juma, alisema lazima msisitizo mkali wa kisheria uwepo, kwa watakaobainika kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji watoto.

Wanafunzi katika Madrassa hiyo, wameahidi kuyafanyiakazi maagizo na makatazo waliyoelezwa, pamoja na kuifikisha elimu hiyo kwa wenzao.

Utafiti uliofanywa na Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar miaka mitatu iliyopita, umewaibua baba wazazi13, waliowafanyia ubakaji watoto wao wa kuwazaa, kati ya hao tisa (9) Unguja na watatu (3) kisiwani Pemba.

 

Ilibainika pia kuwa, baba walezi na wakambo 25, Unguja wakiwa 13 na Pemba 12 waliowabaka watoto wao wa kuwalea katika mazingira tofauti.

 

                             Mwisho

 

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’