MVUMONI CHAKE CHAKE WAOMBA KUONANA NA DK. MWINYI

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WANANCHI wa shehia ya Mvumoni wilaya ya Chake chake, wameomba kuonana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ili kumfikishia kilio chao cha ya kucheleweshewa fidia zao, katika utanuzi wa uwanja wa ndege Pemba.

Walisema, walifanyia tathmini za nyumba, miti na vipando vyengine tokea mwaka 2015, juu ya utanuzi wa uwanja wa ndege Pemba, ingawa hadi leo, hawana taarifa rasmini juu ya tathmini hiyo ilipofikia.

Wakizungumza mbele ya watendaji wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ waliofika shehiani hapo, kutoa elimu na msaada wa kisheria, walisema sasa uvumilivu umewashinda.

Wananchi hao walisema, kwa sasa hakuna kiongozi ambae anaweza kuwapa maelekezo na wakayakubali, isipokuwa awe ni Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi pekee.

Walisema kiongozi huyo amekuwa mkweli na mtendaji kwa vitendo, hivyo wameziomba mamlaka husika, kuzungumza nae ili awasili shehiani humo, na kumpa kilio chao.



Mmoja kati ya wananchi hao, Abdalla Seif alisema ni vyema kwa Rais wa Zanzibar kuwafika, ili kumuelezea changamoto wanazopitia kwa sasa.

‘’Sisi kwa sasa hatujengi, hatuendelezi vipando vya kudumu kwa zaidi ya miaka saba sasa, tunamuomba sana Rais wa Zanzibar atufike, ili atupe mrejesho wa tathmini zetu,’’alisema.

Nae mwananchi Alei Seif Said, alisema wamekuwa hawajui hatma ya maisha yao, baada ya kufanyiwa tathmini zaidi ya mara moja, juu ya utanuzi wa uwanja wa ndege Pemba.

Kwa upande wao Abdalla Ali Said, Khamis Jama na Yahya Said Seif, walisema ni vyema sasa kwa serikali ikaanza kuwalipa fidia zao, ili wakaanze maisha mapya, katika maeneo mengine.

Walieleza kua, wanashindwa kupanda vipando, kuendeleza ujenzi wa nyumba zao kutokana na kuchelewa malipo ya faidia zao.

Mapema Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, aliwataka wananchi hao, kushirikiana na CHAPO, ili kujua changamoto.




‘’Njooni CHAPO tuangalie wapi kuna mkwamo, ili tufuatile kwa pamoja, suluhisho ya upatikanaji wa fidia zenu kwa haraka,’’alieleza.

Aidha Mkurugenzi huyo, aliwataka wananchi hao kusubiri kwanza, hadi serikali iingize fidiai zao kwenye akaunti, ambapo kisheria wanaweza kukata rufaa hapo baadae, ikiwa hakuridhika.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo alisema, tayari tathimi zao, zimeshakuwa kwa mthamini mkuu wa serikali, kwa ajili ya hatua nyingine ya malipo yao.

Afisa Mipango wa Shirika la Msaada wa Kisheria na Haki za Binaadamu Zanzibar ‘ZALHO’ ofisi ya Pemba Siti Habib Mohamed, aliwataka wananchi hao kurudi, kwao ikiwa kutajitokeza changamoto za fidia zao hapo baadae.

‘’Jamani jambo la serikali lazima lifuate taratibu zote, ili kuhakikisha hakuna mwananchi amekoseshwa haki yake, na ndio maana ukaona kama mnacheleweshwa,’’alifafanua.





Mwanasheria kutoka Idara ya Ardhi Pemba, Asha Suleiman Said, alisema hakuna mwananchi atakayehamishwa, pasi na kulipwa fidia yake kisheria.

‘’Serikali haijawahi kufanya hata mara moja, kumuondoa mwananchi katika eneo husika, pasi na kumlipa fidia, na hataka kama ikiwa ndogo unaweza kukata rufaa,’’alifafanua.

Tayari Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, imeshasaini Mkataba wa Ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba, kupitia Kampuni ya PROPAV/MECCO JV ya Hispania.

Ambapo kwa mwaka wa 2022/2023, Mradi ulipangiwa kutumia zaidi ya shilingi bilioni 134.100, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 8,000,000,000 ni kutoka Serikalini na shilingi bilioni 126.100 ni kutoka kwa mfadhili, ingawa hadi mwezi Machi, 2023 hakuna fedha iliyopatikana.



Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba, CHAPO imo katika utekelezaji wa mpango wake kazi, wa kuwafikia wananchi mbali mbali, ili kuwasikiliza changamoto zao kisheria.

                  Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’