‘’MLIOPEWA MAFUNZO WA SHERIA WAWI WAHAMASISHENI WANANCHI KUDAI HAKI ZAO’' CHAPO
KAIMU Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini
wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba, ‘CHAPO’ Kassim
Ali Omar, amewataka wahitimu wa mafunzo ya sheria, kutoka shehia ya Wawi, kuwahamasisha
watu kudai haki zao mbali mbali.
Wito huo aliutoa leo Juni 19, 2023 Vikutani shehiani humo, kwenye ufungaji wa mafunzo ya siku ya tano, ya sheria
kwa wajumbe wa kamati ya sheha na kamati nyengine, za shehia ya Wawi.
Alisema, anaamini
kwa mafunzo hayo, washiriki hao watakuwa waalimu wazuri kwa wenzao, katika
kuwahamasisha kudai haki zao mbali mbali badala ya kuwakatisha tamaa.
Alieleza kuwa,
ndani ya mafunzo hayo wamejua mambo ambayo yanaweza kusababisha kesi kufutwa, kuondolewa
au mtuhumiwa kutumikia kutiwa hatiani.
‘’Mimi naamini
kwa mafunzo haya mliopewa ya sheria ngazi ya shehia, mtakuwa na uwezo
kuwahamasisha wale waliokata tamaa, kwenda kudai haki zao, mbali mbali,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Kaimu Mwenyekiti huyo wa Bodi ya wadhamini wa CHAPO Kassim Ali Omar,
alisema wakati umefika sasa, wa kuunganisha nguvu katika mapambano dhidi ya
dawa za kulevya na udhalilishaji.
‘’Jamii yetu inazungumkwa na udhalilishaji, dawa za kulevya, migogoro ya ardhi, ndoa hivyo mafunzo haya sasa, yatuunganishe pamoja kuyashinda majanga hayo,’’alieleza.
Akizungumzia
kuhusu uwepo wa wasaidizi wa sheria katika shehia ya Wawi, alisema hiyo ni
faraja na kuwataka wananchi kuendelea kuwatumia.
‘’Kwa hakika,
hili la wasaidizi wa sheria shehia ya Wawi na uongozi wa ‘CHAPO’ kubuni mafunzo
haya, ni jambo linalofaa kuendelezwa, katika shehia nyingine,’’alieleza.
Alisema kuwa,
lengo kuu la kuanzishwa kwa wasaidizi wa sheria kwa kila shehia, ni kuona
kwamba ile migogoro isiyokuwa ya lazima kwa wananchi, inapungua.
Mapema
Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake Chake Pemba ‘CHAPO’
Nassor Bilali Ali, alisema mafunzo hayo, wanakusudia kuyasambaaza katika shehia
zote 32 za wilaya hiyo.
Alieleza
kuwa, lengo la kufanya mafunzo hayo, ni kuona wanatatua ile migogoro ambayo siyo ya lazima, kwa
jamii ili kwenda sambamba na upatikanaji wa haki zao.
“Tunalengo
la kuibadilisha jamii katika kutatua migogoro hasa kwa ile isiyokuwa ya lazima,
ikiwemo ya mirathi, ardhi, matunzo ya watoto, hivyo ni imani yangu kuwa,
mafunzo haya yatazaa matunda,” alieleza.
Hata hivyo
aliupongeza uongozi wa shehia ya Wawi wilaya ya Chake chake, kwa kushirikiana
vyema na CHAPO, hadi kufanikisha mafunzo hayo ya kwanza kwa Zanzibar.
Kwa upande
wake Mratibu wa mafunzo hayo, ambae pia ni Msaidizi wa Sheria Jimbo la Wawi
Chake Chake, Haji Nassor Mohamed alisema kuwa mafunzo hayo, yalengo la
kuelimisha jamii, juu ya upatikanaji wa haki.
Hivyo aliwataka
washiriki hao kuyatumia vyema mafunzo waliyopewa, kwa kuyafanyia kazi, ikiwemo kuwapatia
wengine, ili yaweze kuleta matunda hapo baadae.
Sheha wa Shehia
ya Wawi Sharifa Waziri Abdalla, alieleza kuwa wanaimani kwamba mafunzo hayo,
yatakuwa chachu ya maendeleo katika shehia yao.
‘’Kwa hakika
mpango wa kuwepo kwa wasaidizi wa sheria katika shehia, umekuja kuimarisha
upatikanaji wa haki na utatuzi wa migogoro, na mfano mzuri ni hapa Wawi,’’alieleza.
Mmoja wa
washirikia hao Juma Mohamed Tamimu alisema kuwa, mafunzo hayo yataleta tija
katika shehia yao ya Wawi.
“Kuna mambo
mengi tulikuwa hatuyafahamu, baada mafunzo haya ya kisheria, tumelewa njia za
kutafuta haki, tumeweza kujua mengi na tutahakikisha tutawapatia na wenzetu ili
waondokane na migogoro mbali mbali,” alieleza.
Nae Mtama
Mohamed Mohamed, alisema kazi iliyobakia mbele yao ni kuyanfanyia kazi mafunzo
hayo, ili yalete tija kwa wananchi mbali mbali hasa wasiokuwa na uwezo.
‘’Miongoni
mwetu wamo pia wajumbe wa kamati ya sheha ambao wamekuwa wakipokea migogoro
kila siku, sasa mafunzo haya yatakuwa chachu ya kufanikisha kazi zetu,’’alieleza.
Nao Fatma
Kassim na Khamis Mwinjaa, walisema mafunzo hayo ni vyema, yakawa endelevu kwa
makundi mengine ndani ya shehia, ili kuhakikisha kila mmoja amepata uwelewa.
Mafunzo hayo ya siku tano, yameandaliwa kwa
pamoja kati ya Jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake Chake Pemba ‘CHAPO’
na uongozi wa shehia ya Wawi, ambapo mada 12 zilifundishwa ikiwemo Mirathi,
sheria ya mtoto, sheria ya aradhi, sheria ya Ushahidi pamoja na aina za ukamati
kisheria.
MWISHO.





Comments
Post a Comment