WASAIDIZI WA SHERIA 'CHAPO' WAKUMBUSHWA JAMBO MUHIMU

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WASAIDIZI wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba, wakumbushwa kuwahudumia wananchi kwa kuwapa elimu, ushauri na msaada wa sheria, ili iwe rahisi kupata ufumbuzi wa haki zao.

Ushauri huo umetolewa leo Mei 7, 2023 na Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, wakati akizungumza na wasaidizi hao wa sheria, kwenye kikao maalum cha mwezi, kilichofanyika ofisini kwao.

Alisema, lazima wasaidizi hao wa sheria waelewa kuwa, wajibu wao kwa jamii, ni kuendelea kuwahudumia kila siku na kila wakati, kwani wamekuwa wakiwategemea katika kuapata haki zao.

Alieleza kuwa, ndio maana CHAPO kwa kushirikiana jumuiya nyingine, imekuwa ikiwapatia mafunzo ya kuwajengea uwezo wasaidizi hao wa sheria, ili wawe na uweledi wanapokutana na jamii.



Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa, wapo wananchi ambao wameshakata tamaa ya kupata haki zao, hivyo ni wajibu wa wasaidizi wa sheria, kuwapa ushauri ili kutimiza ndoto zao.

‘’Kwanza niwashukuru kwa kazi mnayoendelea kuifanya, lakini endeleeni kukaza kamba, katika kuwahudumia wananchi, hasa suala la kuwapa elimu na msaada wa kisheria,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa CHAPO, alisema wameshajipanga, ili kuhakikisha wananchi wa shehia ya Wawi, kama eneo la majaribio kuwezesha kielimu.

‘’Wawi tumeichagua kama eneo la majaribio, kwa kuanzisha darasa maalum la kuwafundisha wanajamii sheria mbali mbali, na kisha mpango huo utaendelea kwenye shehia nyingine,’’alieleza.

Akizungumzia juu ya umoja na mshikamano, amewakumbusha wasadizi hao wa sheria, kuendelea kusaidiana, kushirikiana katika shughuli zao mbali mbali, za kuwafikia wananchi.

Mapema Mratibu wa ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Ali, aliwakumbusha wasaidizi wa sheria, wanaopata mafunzo mbali mbali, kuwashirikisha na wengine.



‘’Kwa mfano, hivi karibuni tulipata mafunzo ya mabadiliko ya sheria, sasa kama kuna wenzetu hawakupata, lazima tuwaelekeze,’’alifafanua.

Aidha amewahimiza wasaidizi hao wa sheria, kuhudhuria na kwa wakati, wanapokuwa na vikao vyao ndani, kwani huwa wanamambo kadhaa ya kuyajadili.

‘’Kwanza tupunguze utoro na dhararu, maana sisi wasaidizi wa sheria, ndio tegemeo la wananchi wa wilaya ya Chake chake, katika eneo la utoaji wa elimu, msaada na ushauri wa kisheria,’’alieleza.

Msaidizi wa sheria Jimbo la Ziwani, Khadija Said Khalfan, alisema anaunga mkono wazo la kujipangia ratiba na kuhudhuria ofisi ya ‘CHAPO’ kwa ajili ya kutoa huduma.

‘’Ni kweli, lazima tujangie utaratibu wa kuja ofisini kila siku, ili kuwapokea wananchi ambao wanahitaji ushauri, msaada au elimu ya kisheria,’’alipendekeza.




Nae Msaisizi wa sheria, Jimbo la Chake chake Rikizi Hamad Ali, amesema, umoja na mshikamano ndio ambao utepelekea ‘CHAPO’ kuwa juu kiutendaji.

‘’Tufanyeni kazi kwa timu, ili tukienda sehemu moja kutoa elimu tunakwenda kwa wingi, kwani wengine watapata kujifunza na wengine, kuongeza uweledi,’’alishauri.

CHAPO imekuwa na utaratibu wa kukutana na wanachama wake kila mwisho wa mwezi, ambapo pamoja na mambo mengine, ni kuwasilisha ripoti za mwezi za utoaji elimu na msaada wa kisheria.

                                 Mwisho    

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’