‘CHAPO’ YAWAKOSHA WANANCHI KILINDI ELIMU YA SHERIA
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa kijiji cha Kuungeni
shehia ya Kilindi wilaya ya Chake chake Pemba, wamesema mfumo uliofanywa na
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ kuwafuata
kijijini kwao na kuwapa elimu ya kisheria, inafaa kuendelezwa.
Walisema,
mfumo huo unafaa kuendelezwa na kuwa imara zaidi, kwani umewasaidia katika
kukuza uwelewa wao, hasa masuala la haki na fursa zao kisheria.
Wakizungumza
kwenye mkutano wa wazi, uliofanyika Mei 14, 2023 kijijini hapo, walisema wamepata uwelewa wa
mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na maana ya wizi kisheria.
Wananchi hao
walisema, wamejua njia ambazo mwananchi anaweza kuingia kwenye kosa la wizi,
ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya wizi, kuficha taarifa pamoja na kumpa
mawasiliano.
Mwananchi Massoud
Juma Khamis, alisema ujio huo wa watendaji wa CHAPO, umewaamsha katika ufahamu
pia wa masuala ya udhalilishaji, ule ambao sio maarufu kwa jamii.
Alieleza
kuwa, kutopeleka huduma za kibinadamu ambazo zinaweza kuwasababishia watoto
kubakwa, kudhalilishwaji ni mambo ambayo hawakujua madhara yake.
‘’Tukiona tu
kuwa, kama hakuna huduma athari kubwa ni familia kulia njaa, lakini sasa
tumeelewa kuwa, kumbe watoto wanaweza kujiingiza kwenye udhalilishaji, kwa kule
kutafuta huduma,’’alieleza.
Nae Yussuf
Bakar Khamis, alisema mpango huo wa ‘CHAPO’ lazima uwe endelevu kwa vijijini
vyengine, ili wananchi wapate uwelewa.
‘’Kwanza,
niwapongeza sana wasaidizi hawa wa sheria kutoka CHAPO, maana leo (jana),
mmetufumbua macho, na tunawaomba msikae tena sana mje,’’alieleza.
Akifungua
mkutano huo, Sheha wa shehia ya Kilindi wilaya ya Chake chake Nassor Mohamed
Khamis, alisema ni wajibu wa wananchi, waliopata taaluma ya kisheiria,
kuwafikishia wenzao.
‘’Inawezekana,
yupo mwanakijiji mwenzetu hapa Kuungeni hakuwahi kufika, sasa ni wajibu wetu
kuhakikisha anafikishiwa elimu hii ya kisheria,’alifafanua.
Katika hatua
nyingine, sheha huyo aliwataka wananchi kuendelea, kuwaripoti wahalifu na
wadhalilishaji mbali mbali, ili serikali kwa upande wake, ichukuwe hatua.
Mapema Mkurugenzi
wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor
Bilali Ali, alisema wamekuwa wakitoa msaada wa kisheria, bila ya malipo.
Alieleza
kuwa, ni wajibu wa wananchi sasa kuwatumia wasaidizi wa sheria waliopo
shehiani, kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa masuali mbali mbali ya haki zao.
Akizungumzia
kuhusu kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, alisema inalenga kukuza uwelewa kwa jamii, juu
ya sheria msaada wa kisheria.
Mratibu wa ‘CHAPO’
Mohamed Hassan Abdalla, alisema moja ya jambo ambalo wananchi wanashindwa
kutofautisha, ni kati ya kesi kumalizika na mtuhumiwa kupewa dhamana.
‘’Mkimuona
mtuhumiwa ambae mmepeleka Polisi anaranda mtaani, wakati mwengine amepata dhamana,
ambayo ni haki ya mtuhumiwa, hili lazima tulijuwe,’’alifafanua.
Msaidizi wa
sheria Jimbo la Chonga Juma Seif Haji, alisema jamii isipokuwa makini kwenye
dawa za kulevya, vijana wanaweza kupoteza mwelekeo wa maisha yao.
‘’Moja ya
jukumu letu, ni kutoa taarifa kwenye mamlaka husika, ikiwemo Jeshi la Polisi,
maana athari zake huikumba jamii ikiwemo vitendo vya wizi na udhalilishaji,’’alieleza.
Msaidizi wa
sheria Jimbo la Ziwani Khadija Said Khalfan, amewataka wanaume, kutekeleza majukumu
yao, kwa kina ili kutowaingiza wanawake kwenye majaribu ya maisha.
CHAPO
inaendelea na mpango wake wa kupita katika shehia kadhaa za wilaya ya Chake
chake, kwa ajili ya kukutana na wananchi kusikiliza changamoto zao, za
kisheria.
Mwisho

.jpg)







Comments
Post a Comment